Chanzo cha picha, EPA
- Author, Victoria Bourne
- Nafasi, BBC News
Dakika 31 zilizopita
Donald Trump ametia saini marufuku ya kuwazua raia wa mataifa 12 kuingia nchini Marekani kwa kile anachokitaja kuwa tishio kwa usalama wa kitaifa kulingana na Ikulu ya White House.
Trump amesema orodha hiyo inaweza kutathminiwa upya endapo "maboresho ya msingi" yatafanywa basi nchi zaidi zinaweza kuongezwa huku "vitisho vikiibuka kote ulimwenguni".
Hii ni mara ya pili kwa rais huyo kuamuru marufuku dhidi ya raia wa nchi tofauti.
Alitia saini agizo kama hilo mnamo 2017, wakati wa muhula wake wa kwanza ofisini.
Ni mataifa yapi yaliyoathiriwa?
Trump ametia saini agizo la kuwawekewa marufuku ya usafiri raia wa mataifa 12 ikiwa ni pamoja na:
- Afghanistan
- Myanmar
- Chad
- Jamhuri ya Congo
- Equatorial Guinea
- Eritrea
- Haiti
- Iran
- Libya
- Somalia
- Sudan
- Yemen
Mataifa mengine saba ambayo raia wake wamewekewa vikwazo vya usafitri ni:
- Burundi
- Cuba
- Laos
- Sierra Leone
- Togo
- Turkmenistan
- Venezuela
Marufuku hiyo itaanza kutekelezwa Jumatatu ijayo ili kuzuia msongamano wa wasafiri katika viwanja vya ndege vya Marekani kama ilivyoshuhudiwa miaka minane iliyopita hatua sawa na hiyo ilipochukuliwa na utawala wa Trump.
Ikulu ya White House ilisema "hivi ni vikwazo vya kawaida" "vitawalinda Wamarekani dhidi ya vitisho kutoka nje".
Katika video iliyotumwa kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump alisema shambulio la hivi majuzi linalodaiwa kuwa la kigaidi huko Boulder, Colorado "lilidhihirisha tishio kubwa" linaloletwa na raia wa kigeni ambao "hawajachunguzwa ipasavyo".
Watu 12 walijeruhiwa mjini Colorado Jumapili iliyopita wakati mwanamume mmoja aliposhambulia kundi lililokuwa likiunga kuachiwa kwa mkono mateka wa Israel
Mtu anayetuhumiwa kutekeleza shambulizi hilo amebainishwa kuwa ni raia wa Misri.
Marufuku imepokelewaje?
Agizo la hivi punde la Trump, ambalo linatarajiwa kukabiliwa na changamoto za kisheria, lilikosolewa ndani na nje ya nchi.
Somalia iliahidi kufanya kazi na Marekani kushughulikia masuala yoyote ya usalama.
Katika taarifa, balozi wa Somalia nchini Marekani, Dahir Hassan Abdi, alisema nchi yake "inathamini uhusiano wake wa siku zijazo" na Marekani.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Venezuela Diosdado Cabello alionya kwamba "kuwa nchini Marekani ni hatari zaidi kwamtu yeyote, sio tu kwa raia wa Venezuela".
Wanachama wa chama Democratic wamelaani hatua hiyo.
"Marufuku hii ni muendelezo wa marufuku ya Trump dhidi ya Waislamu katika muhula wake wa kwanza, itatutenga zaidi ulimwenguni," Pramila Jayapal, mbunge wa Democrat kutoka Washington, anasema katika chapisho la mtandao wa kijamii.
Mwanasiasa mwingine, mbunge Don Beyer, anasema Trump "alisaliti" maadili ya waanzilishi wa Marekani.
Nini kilitokea mara ya mwisho?
Trump alitangaza marufuku ya awali wakati wa muhula wake wa kwanza madarakani mwaka 2017.
Mataifa ambayo raia wake walipigwa marufuku kuingia marekani wakati huo yamejumuishwa yamejumuishwa tena katika marufuku ya sasa. Mataifa hayo ni pamoja na Iran, Libya na Somalia.
Wakisoaji wanaitaja marufuku hiyo kuwa "marufuku dhidi ya Waislamu" kwa sababu orodha ya awali ilijumuisha mataifa yaliyo na waumini wengi wa Kiislamu.
White House ilifanyia marekebisho sera hiyo, na kuongeza Korea Kaskazini na Venezuela.
Amri hiyo ilidumishwa na mahakama ya juu zaidi mwaka 2018.
Rais Joe Biden, ambaye alimrithi Trump, alifuta marufuku hiyo mnamo 2021, na kuiita "doa kwenye dhamiri yetu ya kitaifa."