Bingwa mpya ZPL ni KVZ au Mlandege

1 day ago 7

By  Mwandishi Wetu

Mwananchi Communications Limited

BINGWA mpya wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) anatarajiwa kujulikana leo wakati Mlandege na KVZ zitakaposhuka viwanja viwili tofauti kusaka pointi za kufungia msimu wa ligi hiyo.

Mlandege inayoongoza msimamo wa Ligi hiyo kwa tofauti na mabao ya kufunga na kufungwa ikiwa na pointi 59 kama ilizonazo KVZ, itakwaruzana na New City iliyoshuka daraja mapema kwenye Uwanja wa Mao A mjini Unguja.

Maafande wa KVZ wanaochuana na Mlandege kuwania taji hilo lililotemwa mapema na waliokuwa watetezi, JKU iliyomaliza msimu ikishika nafasi ya tano ikivuna pointi 49, wenyewe watakuwa Uwanja wa Mao B pia mjini Unguja kuvaana na Kipanga inayoshika nafasi ya 10 kwa sasa.

Mlandege inaongoza kwa kufunga mabao 63 na kufungwa 19 na kuwa na uwiano wa mabao 44, wakati KVZ ikifunga 34 na kufungwa 12, ikiwa ndio timu iliyoruihusu mabao machache kwa msimu huu, huku ikiwa na uwiano wa mabao 22, hali inayowapa ugumu kutoboa mbele ya wapinzani wao.

Ili KVZ ibebe ubingwa huo ikiwa ni mara ya kwao kwao ni lazima ishinde mbele ya maafande wenzao wa Kipanga, lakini ikiiombea Mlandege itoke sare au ipoteze mechi dhidi ya New City inayoshika nafasi ya 14 na ikiwa imeshashuka daraja kama ilivyo kwa Tekeleza, Mwenge na Inter Zanzibar.

Matokeo ya ushindi au sare kwa timu zote hizo mbili za juu, itakuwa na maana Mlandege ambao ni mabingwa wa Kombe la Mapinduzi wa misimu miwili mfululizo itakuwa bingwa kwa tofauti na mabao, kwani imeizidi KVZ mabao 22.

Tayari Bodi ya Ligi ya Zanzibar imetoa tahadhari kwa timu zote zinazocheza leo kufunga msimu wa ZPL 2024-2025 juu ya kuepuka upangaji wa matokeo ili kuhakikisha bingwa wa ligi hiyo anapatikana kihalali na kukabidhiwa taji laoe baadae leo hii ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita.

Mlandege inasaka taji la nane katika historia ya Ligi hiyo, ili kuisongelea mabingwa wa kihistoria, KMKM iliyotwaa mara tisa, wakati KVZ inasaka taji la kwanza kwani kabla ya hapo haijawahi kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Katika mechi za kufungia msimu zilizopigwa jana watetezi JKU ilipoteza kwa bao 1-0 mbele ya Uhamiaji, bao pekee likiwekwa kimiani ya Yahya Haji dakika ya 72, huku Malindi ikiizima Mwembe Makumbi kwa mabao 2-1.

Mabao ya Malindi yaliwekwa kimiani an Omar Thani dakika ya 67 na Feisal Hilal dakika 89, wakati bao la kufutia machozi la Mwembe Makumbi lilifungwa na Robert Pius kwa mkwaju wa penalti dakika 65.

Read Entire Article