Mwananchi Communications Limited
Muktasari:
- Mashabiki kutoka kila kona ya dunia wanajiandaa kwa safari ya kipekee kusafiri kwenda kushuhudia michuano hiyo ya kibabe kabisa duniani.
FLORIDA, MAREKANI: KOMBE la Dunia la Klabu la Fifa mwaka huu litaweka historia mpya kwa mara ya kwanza likishirikisha klabu 32 kutoka mabara yote.
Mashabiki kutoka kila kona ya dunia wanajiandaa kwa safari ya kipekee kusafiri kwenda kushuhudia michuano hiyo ya kibabe kabisa duniani.
Kwa wengi, hiyo siyo tu safari ya burudani, bali pia ni ndoto ya maisha. Hata hivyo ili kufanikisha safari ya namna hiyo yanahitaji maandalizi makini kuanzia gharama za tiketi za ndege, malazi, usafiri wa ndani hadi tiketi za mechi na matumizi ya kila siku ikiwamochakula.
Katika makala hii inachambua kwa kina gani hali halisi mashabiki watakaosafiri kwenda Marekani kwa ajili ya Kombe la Dunia la Klabu la kihistoria kuanzia gharama za hoteli, vyakula, usafiri na tiketi za mechi.
GHARAMA ZA HOTELI
Marekani ina miji mingi ya kitalii yenye viwango tofauti vya gharama za hoteli. Kwa mashabiki, malazi ni mojawapo ya gharama kubwa zaidi katika safari.
Makadirio ya bei kwa usiku mmoja kwenye hoteli ya hadhi ya nyota tatu huko Miami ni kati ya Dola 180 hadi 250, New York ni 200 hadi 300, Los Angeles (180 hadi 270) na Seattle ni 150 hadi 220.
Kwa upande wa zile hoteli za bei ya chini kule Miami huanzia Dola 70 hadi 120, New York 90 hadi 150, Los Angeles 80–140 na Seattle ni Dola 60 hadi 110.
Hata hivyo, bei hizo zinaweza kupanda zaidi wakati wa michuano husika.
TIKETI ZA NDEGE
Gharama ya tiketi ya ndege inategemea nchi unayotoka, muda uliokata na uwanja wa ndege unaotua nchini Marekani.
Hata hivyo, haya hapa ni makadirio ya nauli ambazo hutozwa kutoka maeneo mbalimbali mfano gharama ya kwenda na kurudi kutoka Cairo, Misri kwenda Miami au New York, Marekani nauli huwa kati ya Dola 850 hadi 1,200.
Nairobi (Kenya) hadi Los Angeles ni Dola 900 hadi 1,300, Sao Paulo (Brazil) hadi Houston ni Dola 600 hadi 950.
Kutoka London (Uingereza) hadi Miami ni Dola 500 hadi 800, pia Tokyo (Japan) hadi San Francisco ni Dola 900 hadi 1,400.
Mashabiki waliokata tiketi miezi miwili au mitatu iliyopita wanaweza kuwa wamepata kwa bei rahisi tofauti na wale watakaokata kipindi ambacho kina uhitaji mkubwa.
TIKETI ZA MECHI
Fifa imeweka tiketi kwa bei ya wastani ili kuwavutia mashabiki, lakini kwa mechi za hatua za mtoano na kuendelea bei inaonekana kuwa kubwa zaidi. Mechi za makundi, tiketi zinapatikana kuanzia Dola 30, ingawa idadi ya tiketi za bei hiyo ni ndogo. Bei nyingi za tiketi za mechi za makundi ziko kati ya Dola 60 hadi 300, kulingana na jukwaa husika.
Hatua ya 16 bora tiketi zinauzwa Dola 80, nusu fainali tiketi za bei ya chini zinauzwa Dola 140 na kwa upande wa fainali tiketi zinaanzia Dola 300, na zile za VIP ni 2,200.
USAFIRI WA NDANI
Mechi zitafanyika katika miji 12, hivyo mashabiki wengi watalazimika kusafiri kati ya miji mbalimbali ili kushuhudia timu zikicheza. Gharama za treni zinakadiriwa kuwa kati ya Dola 30 hadi 150 ikitegemea na umbali wakati ndege ni Dola 80 hadi 200 na magari ya kukodi kama Uber na Tax ni Dola 50 hadi 90.
CHAKULA
Mashabiki wengi huchagua vyakula vya haraka ili kuokoa muda na fedha hasa wale wanaotembelea viwanja tofauti.
Makadirio ya gharama ya kila siku kupitia chakula ni kwa wale watakaokula vyakula vya kawaida bei inatajwa kuwa kati ya Dola saba hadi 12 wakati vyakula vya bei ya juu vikiwa ni Dola 40 na kuendlea. Hivyo inapaswa maandalizi kwelikweli.