Chanzo cha picha, iStock
- Author, Michelle Spear
- Nafasi, the conversation
Dakika 2 zilizopita
Machozi kwa kawaida huonekana kama ishara ya huzuni au maumivu, lakini pia watu hulia wakati wa furaha maishani: harusi, siku ya kuzaliwa, kuungana na uliyempoteza, ushindi katika michezo, au hata tendo la fadhili usilolitarajia.
Machozi ya furaha? Hii misamiati inaonekana kukinzana, lakini yanaeleza jinsi ubongo wa mwanadamu unavyoshughulikia hisia kali.
Kulia ni jibu la kibayolojia pindi hisia ziwapo kubwa - na haibagui kati ya hisia nzuri na mbaya. Iwe hisia imechochewa na huzuni au furaha, machozi ni matokeo ya ubongo kujaribu kuchakata zaidi ya kile unachoweza kudhibiti kwa wakati huo.
Hisia chanya na hasi, huamsha mfumo wa limbic, sehemu ya ubongo inayohusika katika kuchakata hisia na kumbukumbu. Ndani ya mfumo huu, nyuroni hufanya kazi ya kuwa kengele ya hisia, inapotambua msisimko na kuufanya mwili ujibu.
Mfumo wa amygdala unapopokea hisia kali, huamsha maeneo mengine ya ubongo ikiwa ni pamoja na eneo la hypothalamus, eneo linalodhibiti utendaji kazi wa mwili, kama vile mapigo ya moyo, kupumua na kutoa machozi.
Mfumo mwingine muhimu ni anterior cingulate cortex, ambao una jukumu la kuendesha hisia, maamuzi na huruma. Husaidia kuratibu mwitikio wa ubongo panapotokea mgongano wa kihisia, kama vile kupata furaha na huzuni kwa wakati mmoja. Mwingiliano huu unaeleza kwa nini furaha ya ghafla inaweza kutoa majibu ambayo kwa kawaida huhusishwa na dhiki (machozi).
Wanasayansi wanaamini kilio cha furaha ni njia ya kuturudisha kwenye usawa wa kihisia baada ya kupata hisia kubwa za furaha. Kulia huamsha mfumo wa neva ambao hupunguza kasi ya moyo kupiga na kuufanya mwili kutulia, baada ya kuongezeka kwa hisia kali. Kwa maneno mengine, machozi hutusaidia kutulia.
Mwili kutulia haitokei unapokuwa na furaha pekee. Pia kulia wakati wa msongo wa mawazo au kiwewe husaidia kuutuliza mwili. Kinachoshangaza kuhusu kilio cha furaha ni jinsi mwili unavyounda uwiano pale hisia zinapokinzana: kitulizo baada ya hofu, shukrani baada ya shida, furaha baada ya mapambano.
Pia unaweza kusomaMachozi ya furaha
Kinachojulikana kama machozi ya "furaha" ni zaidi ya machozi. Mara nyingi huibuka kutokana na mchanganyiko wa hisia. Kwa mfano, mzazi akimtazama mtoto wake akihitimu anaweza kuwa na furaha, na huzuni kidogo kwa wakati mmoja.
Kukutana tena baada ya muda mrefu kunaweza kuchochea furaha ya kuonana na huzuni ya kutokuwa mmeonana kwa muda mrefu. Wanasaikolojia wanataja hali hii kuwa ni kihisia inayokusanya hisia zote chanya na hasi.
Hisia huhusisha mifumo ya kumbukumbu pia, ambayo huchakata na kurejesha historia ya maisha binafsi ya mtu. Ndio maana wakati wa furaha unaweza kutokwa na machozi bila kutarajia – baada ya kumbukumbu za kupoteana na changamoto kurudi.
Wanadamu ndio wanyama pekee wanaojulikana kutoa machozi ya hisia. Ingawa mamalia wengi hutoa machozi lakini ni ya kulainisha jicho tu, wanadamu ndio pekee ambao hulia kama jibu la hisia.
Kilio cha furaha kinaweza kuimarisha mahusiano ya kijamii, kama kukaribisha huruma. Utafiti umeonyesha kwamba kuna uwezekano mkubwa wa watu kutoa msaada kwa mtu anayelia, bila kujali kama machozi yake ni ya huzuni au ya furaha.
Kwa hivyo kwa nini tunalia tukiwa na furaha? Kwa sababu furaha si hisia rahisi. Mara nyingi huibua kumbukumbu, utulivu, hofu na uzito wa mambo.
Machozi ni njia ya ubongo kushughulikia utata huu, na kuashiria wakati ambao ni muhimu, au wakati ni wa furaha.