Chanzo cha picha, Getty Images
Dakika 17 zilizopita
Neno la Kiswahili 'pamoja' likiwa na maana ya pamoja, limekuwa likitumika kuzitaja Kenya, Tanzania na Uganda kuwa wenyeji wa michuano ya Mataifa ya Afrika (CHAN), lakini majirani hao hawako sawa linapokuja suala la maandalizi ya fainali hizo mwezi Agosti.
Inatarajiwa kuwa mara ya kwanza kwa mashindano ya bara kuandaliwa kwa pamoja na nchi tatu, lakini mashindano ya wachezaji wa nyumbani tayari yameahirishwa mara moja kwa sababu kazi za miundombinu na vifaa hazijakamilika.
Afisa mmoja mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) anasema Kenya iko tayari "asilimia 90", lakini ameonya kwamba hatua lazima zipigwe na kwamba masuala ya usalama ya uwanjani yanahitaji kushughulikiwa.
"Uganda tunaweza kucheza jana, Tanzania tunaweza kucheza kesho, Kenya tunaweza kucheza kesho," Katibu Mkuu wa Caf Veron Mosengo-Omba aliambia BBC Sport Africa alipokuwa ziarani Nairobi Jumatano.
"Nchini Kenya nimeona viwanja vya mazoezi vikiwa tayari, vyumba vya kubadilishia nguo vimewekwa tayari.
"Lazima waongeze kasi.
"Ikiwa watapunguza kasi, hatutaruhusu CHAN kuandaliwa hapa."
Pia unaweza kusomaUsalama wa viwanja
Chanzo cha picha, Getty Images
Udhibiti wa umati wakati wa mechi kubwa nchini Kenya umekuwa eneo la wasiwasi katika miezi ya hivi karibuni.
Mnamo Machi, mashabiki walilazimika kuingia Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo wakati wa mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026 dhidi ya Gabon kwa kuvunja lango.
Tukio hilo lilijiri wakati wa mchezo wa kwanza wa Harambee Stars katika ardhi ya nyumbani baada ya takriban miaka miwili.
Mosenga-Omba anakiri kwamba ingawa tatizo hilo la kutokuwepo kwa muda mrefu katika kuandaa kandanda ya kimataifa "inaeleweka", "haikubaliki".
Huku michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 ikitarajiwa kuandaliwa kwa pamoja na Kenya, Tanzania na Uganda, Caf tayari inachukua hatua kuhakikisha viwango vya usalama vinafikiwa kwa CHAN.
"Tumezindua kozi za kutoa mafunzo kwa polisi, kwa sababu jinsi unavyosimamia usalama katika umati wa watu uwanjani na nje ya uwanja ni tofauti," Mosengo-Omba aliongeza.
"Kwa hiyo tunawafundisha polisi jinsi ya kulinda usalama uwanjani na pia tunatoa mafunzo kwa wanachama wa shirikisho ili kuimarisha ulinzi.
"Tutaendelea hadi mwisho wa CHAN na Afcon."
Je, miundo mbinu ikoje?
Chanzo cha picha, Peter Njoroge/BBC
Kenya itatumia viwanja viwili jijini Nairobi kwa mashindano ya CHAN; Uwanja wa Kasarani wenye uwezo wa kubeba watu 60,000 na Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo unaochukua watu 22,000.
Kulingana na afisa mkuu mtendaji wa kamati ya andalizi nchini humo Mike Rabar, ni masuala kama hayo ambayo yameitia wasiwasi Caf.
"Tatizo kubwa kufikia sasa ni vitu kama ukuta wa uwanja wa Nyayo, ambao unapaswa kuwa tayari kufikia mwishoni mwa mwezi huu," Rabar aliiambia BBC Sport Africa.
"Ndio maana hadi kufikia sasa Caf haijaturuhusu kuandaa michunao hiyo kwa asilimia 100, kuna mambo madogo madogo.
"Viingilio vinavyozunguka uwanja lazima vidhibitiwe na miundombinu thabiti ili kuhakikisha raia pia wanadhibitiwa kwa njia iliyopangwa.
"Haya ni mambo ambayo Caf inasisitiza kuhusu - usalama wa mashabiki."
Kuhusu mchezo wa Kenya na Gabon mwezi Machi, ambapo tiketi za mtandaoni zilitumika na mauzo kumalizika siku moja kabla ya mchezo huo, Rabar alisema waandaaji "walifanya vyema" katika baadhi ya vipengele.
"Kwa kweli, kulikuwa na ukiukwaji kutoka kwa miundombinu dhaifu karibu na uwanja," aliongeza. "Hayo ndio masuala ambayo tunapaswa kuzingatia."
Rais wa Caf Patrice Motsepe, ambaye alizuru Afrika Mashariki kuangalia maendeleo ya maandalizi ya CHAN mwezi Disemba, anatarajiwa kuzuru eneo hilo tena hivi karibuni.
Safari hiyo itatumika kama makataa muhimu kwa mataifa matatu mwenyeji.
Kwa upande wake, kamati andalizi nchini Kenya ina hamu ya kuwa tayari mwishoni mwa mwezi Juni.
"Kinachosubiriwa ni mambo madogo kama vile kuunganisho [kompyuta], masuala ya nguvu za umeme na mawasiliano," Rabar alisema.
"Caf imeweka viwango vya juu sana kwa hivyo tunajaribu kuona jinsi ya kuviafikia ili inapofika wiki ya kwanza ya Julai tunaweza kuandaa mchezo kwa raha."
Wakati huo huo, mawaziri wa michezo kutoka mataifa matatu wenyeji wamethibitisha kujitolea kwao kuandaa mashindano yenye mafanikio kwa bajeti ya $39m.
Majadiliano ya 'Pamoja visa' kuwezesha kuingia na harakati yanaendelea, na nchi hizo tatu pia zinashughulikia kutoa misamaha ya kodi kwa vifaa vinavyoletwa katika maeneo yao.
Pia unaweza kusomaImetafsiriwa na Seif Abdalla