Chanzo cha picha, SBU
- Author, Paul Adams
- Nafasi, BBC
Dakika 15 zilizopita
Siku chache zimepita, na Ukraine bado inatafakari madhara kamili ya Operesheni ya Spider's Web, iliyoshuhudia mashambulizi makubwa siku ya Jumapili dhidi ya ndege za kivita za Urusi.
Siku ya Jumatano, shirika la ulinzi la Ukraine (SBU), ambalo lilipanga shambulio hilo, lilitoa video za ziada, za mashambulizi hayo, pamoja na taswira ya kustaajabisha ya jinsi operesheni hiyo tata ilivyoendeshwa.
Picha za satelaiti ambazo zimeibuka tangu Jumapili, zinaonyesha ndege za kivita zilizoharibiwa kwenye kambi za anga za Olenya, Ivanovo, Dyagilevo na Belaya, na kuthibitisha mafanikio makubwa ya operesheni hiyo.
Kwa waangalizi wa Ukraine, operesheni nzima iliyoandaliwa kwa mwaka mmoja na nusu, inabaki kuwa ya kushangaza.
"Hii inaweza kuhesabiwa kuwa moja ya operesheni nzuri zaidi katika historia yetu," anasema Roman Pohorli, mwanzilishi wa DeepState, kundi la wachambuzi wa masuala ya kijeshi kutoka Ukraine.
"Tumeonyesha kuwa tunaweza kuwa na nguvu, tunaweza kuwa wabunifu na tunaweza kuwaangamiza maadui zetu bila kujali wapo mbali kiasi gani."
Pia unaweza kusomaMafanikio ya operesheni
Chanzo cha picha, Reuters
Ni muhimu kutambua kwamba karibu taarifa zote ambazo zimejitokeza juu ya shambulio hilo zimetolewa na SBU yenyewe. Huku Kremlin ikiwa haijakanusha chochote.
Akizungumza na vyombo vya habari siku ya Jumatano baada ya kukabidhi nishani kwa maafisa wa SBU walioshiriki katika operesheni hiyo, rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky alirudia madai kuwa ndege 41 zimeharibiwa.
"Nusu ya hizo haziwezi kukarabatiwa tena," alisema, "na zingine zitachukua miaka kuzikarabati, ikiwa kuna uwezekano huo wa kuzikarabati."
Iwapo kungekuwa na usitishaji mapigano, aliongeza, Operesheni ya Spider's Web isingetokea.
Video ya dakika nne iliyotolewa na SBU inatoka maelezo muhimu. Droni 117 zilihusika, kushambulia ndege za kivita, ndege za usafirishaji na ndege za rada (AWACS).
Moto unaonekana kwenye ndege kadhaa zilizoshambuliwa. Moto unaonekana kwenye mbawa za baadhi ya ndege, na kufichua kwamba tayari ndege hizo zilikuwa na makombora ya kushambulia, ambayo Urusi imeyatumia katika mashambulizi yake ya anga dhidi ya Ukraine.
Ndege zisizo na rubani, zinazorushwa na marubani, walioketi nchini Ukraine, zimeshambulia kwa uangalifu na kwa usahihi maeneo hatari, ikiwa ni pamoja na matangi ya mafuta yaliyo kwenye mabawa ya ndege.
Baadhi ya milipuko ya moto yanaashiria matangi hayo yalikuwa yamejaa mafuta, tayari kwa kupaa.
Sehemu moja muhimu ya video inaonyesha droni zikishambulia ndege mbili za Beriev A-50, ndege kubwa za rada zilizotengenezwa kwa mara ya kwanza wakati wa utawala wa Umoja wa Kisovieti.
Kati ya ndege zote zilizolengwa katika Operation Spider's Web, A-50 ndio muhimu zaidi, zina rada zenye uwezo wa kuona shabaha na vitisho umbali wa zaidi ya kilomita 600 (maili 372).
Ndege za rada
Chanzo cha picha, Getty Images
Kabla ya uvamizi wa Urusi mwaka 2022, inaaminika Urusi ilikuwa na ndege aina hiyo A-50s tisa. Kabla ya Jumapili iliyopita, takribani tatu kati ya ndege hizo zilidunguliwa au kuharibiwa katika mashambulizi ya nyuma ya droni.
Picha za hivi punde zaidi zinaashiria kwamba droni zimepiga ndege mbili za rada aina ya A-50 zilizoegeshwa kwenye uwanja wa ndege wa Ivanovo Severny, kaskazini-mashariki mwa Moscow. Hata hivyo, kwa kuwa video ilikatika wakati wa shambulio, hii ni vigumu kuthibitisha hilo.
Picha za setilaiti, zinaonyesha kwa uwazi mabaki ya ndege za kivita, lakini hazionyeshi ndege za A-50. Ikiwa madai ya Ukraine ni ya kweli, basi ndege hizi muhimu za rada za Urusi kwa sasa, huenda zimebaki nne.
"Kuanzisha upya uzalishaji wa A-50 kwa sasa ni vigumu, kutokana na vikwazo vya uagizwaji wa vifaa kutoka nje na uharibifu wa viwanda vya uzalishaji," anasema mchambuzi wa masuala ya ulinzi Serhii Kuzan.
"Kwa hivyo, kila uharibifu wa aina hii ya ndege ni tatizo kwa Urusi, kwani haiwezi kurekebisha uharibifu huo kwa haraka."
Kusafirisha droni
Chanzo cha picha, SBU
Mapema Jumatano, SBU ilitoa video nyingine ya mashambulizi ya Jumapili: matumizi ya kontena maalumu, zilizowekwa kwenye ya malori na kusafirisha ndege zisizo na rubani hadi maeneo yaliyo karibu na vituo vinne vya anga vya Urusi.
Video mbili zinaonyesha lori lililobeba kile kinachoonekana kuwa maboksi ya mbao yaliyoficha droni.
"Kwa mtazamo wa kijeshi, hii ni hatua ya mabadiliko katika vita," anasema mtaalamu wa usafiri wa anga Anatolii Khrapchynskyi.
"Kwa sababu tumetoa pigo kubwa kwa Urusi na uwezo wa Shirikisho la Urusi."
Zaidi ya miezi mitatu baada ya Donald Trump kumkashifu Volodymyr Zelensky, akimwambia "hana nguvu," Ukraine imetoa jibu kali.
"Ukraine imeonyesha dunia nzima kwamba Urusi kwa kweli ni dhaifu na haiwezi kujilinda ndani," anasema Khrapchynskyi.
Lakini hilo halimaanishi kwamba Urusi iko karibu kubadilika.
Baada ya mazungumzo yake ya hivi punde na Vladimir Putin, Donald Trump amesema wamejadili kuhusu mashambulizi ya Ukraine.
"Yalikuwa mazungumzo mazuri," Rais Trump alisema kupitia mtandao wa kijamii wa Truth Social, "lakini sio mazungumzo ambayo yatasababisha amani ya haraka."
"Rais Putin amesema, na kusisitiza sana, kwamba atalazimika kujibu mashambulizi ya hivi karibuni ya Ukraine kwenye viwanja vyake vya ndege."