Fedha za Kenya

Chanzo cha picha, AFP

  • Author, Na Peter Mwangangi & Ambia Hirsi
  • Nafasi, BBC Swahili
  • Akiripoti kutoka Nairobi
  • Dakika 43 zilizopita

Bajeti ya kitaifa nchini Kenya ya mwaka ujao wa kifedha (2025/2026) inatarajiwa kusomwa bungeni na Waziri wa fedha John Mbadi alhamisi Juni 12.

Lakini kabla wabunge hawajapata fursa ya kusikiliza na baadaye kujadili kuhusu makadirio yatakayokuwepo, Wakenya wanaendelea kutoa maoni yao kuhusu vipengee ambavyo wanahisi hawakubaliani navyo, hasa katika mswada wa fedha ambao huorodhesha kodi zitakazotozwa ili kufadhili bajeti inayopendekezwa ya Kes 4.356 trilioni ($33.6bn).

Taarifa za kuwafahamisha Wakenya kuhusu yanayopendekezwa katika mswada huo wa fedha zimeanza kuchapishwa katika mitandao ya kijamii huku wengi wakitumia X kueleza kero lao na mapendekezo, lakini pia kumekuwa na majukwaa rasmi ya umma yaliyoandaliwa na serikali ili kutoa maoni kwa mujibu wa sheria.

Tuanze kwa kuangalia masuala matano yenye utata.

1. KRA kufikia data binafsi

Kuna pendekezo la kuipa mamlaka ya ukusanyaji ushuru KRA uwezo wa kupata taarifa muhimu za kibinafsi hasa katika shughuli za kibiashara, yaani data za kibinafsi zilizokusanywa kwa niaba ya wateja au zilizokusanywa wakati wa biashara. Kwa mfano kutoka kwa kampuni za teksi za kidijitali kama vile Uber na Bolt.

Pendekezo ni kwamba KRA itapata idhini ya kupata taarifa hizo muhimu bila kuhitaji amri ya mahakama, na kuna hofu kuhusu usalama wa taarifa za watu, baadhi wakisema hii inaweza kutumiwa kwa sababu nyingine zaidi ya kodi.

Shirika la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International limepinga hili, likisema kwamba "amri isiyokuwa na ukomo wowote wa kutaka ujumuishaji wa data zote bila kuzingatia ulinzi au usalama wake inaweza kugeuza ukusanyaji wa ushuru na kuufanya kuwa njia ya kufuatilia maisha ya watu wengi."

2. Bidhaa ambazo zilikuwa hazitozwi kodi

Kwa jumla, serikali haijasema moja kwa moja kwamba inaongeza kodi mpya katika mswada huu. Badala yake, imebadilisha baadhi ya bidhaa ambazo zilikuwa hazitozwi kodi, na kuziorodhesha miongoni mwa zile zitakazotozwa kodi ya nyongeza ya thamani (VAT).

Bidhaa hizi ni kama vile chakula cha mifugo, simu, magari, betri za sola na malighafi ya kutengeneza bidhaa za matibabu

"Mapendekezo ya kuongeza ushuru yamefichwa kijanja kwa kufanyia marekebisho vifungu vya sheria nyingine," anasema Mbunge Gathoni Wamuchomba ambaye amejitolea kuwahamasisha Wakenya mitandaoni kuhusu yaliyomo kwenye mswada huo.

3.Muundo wa sera ya kodi ya mapato

Mswada huo pia unapendekeza marekebisho madogo lakini muhimu kwa Sheria ya Kodi ya Mapato itakayoathiri wafanyakazi na waajiri wao, kwani waajiri watabadilisha jinsi wanavyotoa makato, na misamaha ya kodi katika mishahara, maarufu kwa kimombo kama pay-as-you-earn tax au PAYE.

Baadhi serikalini wanaona kama hili ni jambo zuri wakisema itaongezea wafanyakazi kipato katika mishahara yao, lakini baadhi wataalamu wa kodi wanatahadharisha kwamba hili linaweza kusababisha mapato ya mishahara kupungua.

Taasisi ya masuala ya kiuchumi (IEA) inasema kwamba kuna haja ya serikali kufafanua zaidi ili suala hili liwe wazi na kueleweka vyema na kila mtu.

Lakini sio kila kitu kibaya katika mswada huu. Kuna mapendekezo mazuri pia.

4. Malipo ya 'Per Diem'

Kwa mfano, wafanyakazi wanaopokea fedha wanaposafiri kwa kazi nje ya mji wao, yaani PER DIEM, kiwango cha chini kabisa kutozwa kodi kitakuwa Kes 10,000 ($77) kwa siku. Awali, ilikuwa Kes 2,000 ($15) pekee.

Kodi ya miamala ya kidijitali

Pili, mswada unapendekeza kupunguza kodi ya miamala ya kidijitali kutoka 3.0% to 1.5%. Hii itakuwa ahueni kwa wengi ambao hufanya malipo ya kidijitali, kwani hii ni sekta inayoendelea kukua.

5. Riba kwa wanaopanga kujenga nyumba

Na tatu, kwa wale wanaonuia kujenga nyumba, hawatatozwa riba ya hadi Kes 360,000 ($2,780) iwapo watachukua mkopo kutoka kwa taasisi za kifedha zilizoorodheshwa.

Maoni kuhusu mswada huo bado yanaendelea kutolewa, na huenda mapendekezo mengine yakaongezwa na mengine kuondolewa hadi kufikia siku ya kuwasilisha mswada ulioboreshwa rasmi bungeni.