Savio yashindwa kuonyesha makali

2 days ago 5

WAKATI Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) ikizidi kushika kasi, mambo bado hayajakaa vizuri kwa timu kongwe ya Savio baada ya kuchemsha katika mechi zake kadha za ligi hiyo.

Savio iliyowahi kuwa bingwa mwaka 2016, 2017, 2018 na 2021, msimu huu imeshindwa kuonyesha makali kama ilivyozoeleka kwani ilianza kwa kufungwa na DB Oratory kwa pointi 75-66, Stein Warriors pointi 93-74, Vijana City Bulls pointi 70-50, Dar City pointi 92-73 kabla ya kushinda dhidi ya Polisi kwa pointi 93-59.

Savio iliyozoeleka kucheza vizuri katika mzunguko wa pili, katika ligi ya msimu huu inayochezwa mzunguko mmoja, imeonyesha itakuwa na wakati mgumu kufanya vizuri.

Ligi ya mwaka huu imeonyesha kila timu inapambana kutafuta nafasi ya kucheza hatua ya robo fainali na huku zikionyesha ushindani.

Ushindani huo umezifanya timu kongwe zicheze kwa tahadhari kubwa kuhofia zisifungwe kirahisi.

Moja ya timu kongwe iliyowahi kuchezea kichapo ni timu ya JKT iliyofungwa na Pazi kwa pointi 63-50 na mchezo mwingine ikafungwa na UDSM Outsiders kwa pointi 60-56.

Kutokana na ushindani huo unavyoendelea UDSM nayo ikafungwa na KIUT kwa pointi  64-53.

Ligi inatarajiwa kuendelea leo kati DB Troncatti na City Queens, UDSM Queens na Jeshi Stars, na upande wanaume itakuwa ni kati ya Dar City vs Mgulani JKT, Vijana 'City Bulls' vs Kurasini Heat. 

Read Entire Article