Mastar tisa Stars warudishwa kuiwahi dabi

8 hours ago 5

By  Charity James

Reporter

Mwananchi Communications Limited

WAKATI hatima ya Dabi ya Kariakoo kati ya wenyeji Yanga dhidi ya Simba ikiwa bado haifahamiki kama itachezwa au la, nyota tisa wa vigogo hivyo waliokuwa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ iliyocheza juzi usiku mechi ya kirafiki ya kimataifa na Bafana Bafana ya Afrika Kusini wamerudishwa Dar.

Nyota hao walikuwa sehemu ya kikosi hicho cha Stars kilichoenda Sauzi na juzi kutoka suluhu dhidi ya Wasauzi na fasta baada ya mechi hiyo waliruhusiwa kuondoka kurejea nchini ili kuwahi maandalizi ya Simba na Yanga kwa ajili ya dabi iliyopangwa kupigwa Juni 15, iliyokwama kuchezwa Machi 8.

Wachezaji hao waliorejea nchini jana na kulikosa pambano la michuano ya Kombe la Cosafa dhidi ya Madagascar lililopigwa jioni ya jana na ule wa Eswatini ni pamoja na Abdulrazak Hamza, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kibu Denis, Ally Salim, Yusuf Kagoma na Valentino Mashaka wote wa Simba.

Wengine ni mabeki wawili wa Yanga, Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ sambamba na kiungo chipukizi Shekhan Ibrahim.

Mapema asubuhi Mwanaspoti lilipenyezewa taarifa kwamba wachezaji wa Simba na Yanga wameruhusiwa kuondoka kambi ya Stars kurudi nyumbani, jambo lililothibitishwa na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo alipotafutwa na gazeti hili.

Ndimbo alisema ni kweli wachezaji hao wa Simba na Yanga wameruhusiwa kutoka sehemu ya kikosi cha Stars ili kuwahi maandalizi ya dabi.

“Ni kweli wameondoka leo (jana), hii ikiwa ni mara baada ya mechi dhidi ya Bafana Bafana. Hawatakuwa sehemu ya kikosi cha wachezaji 20 kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Cosafa, tukianza kucheza na Madagascar leo (jana) kisha kumalizia na eSwatini,” alisema Ndimbo.

Stars imepata nafasi ya kushiriki michuano ya Cosafa iliyoanza Juni 4 na kutarajiwa kumalizika  Juni 15 ikipangwa Kundi C baada ya Morocco waliokuwa wamealikwa kuchomoa dakika za jioni na kwa msimu huu michuano hiyo inashirikisha timu za taifa za nchi 14.

Nchi hizo ni wenyeji Afrika Kusini, Msumbiji, Mauritius  na Zimbabwe zilizopangwa Kundi A, huku Kundi B likiwa na Angola, Namibia, Malawi na Lesotho, wakati Kundi C lina Tanzania, Madagascar na Eswatini, ilihali Zambia, Comoros na Botswana zikipangwa Kundi D.

Read Entire Article