Chanzo cha picha, NASA/Johns Hopkins
Dakika 13 zilizopita
Mgogoro unaoendelea kuhusu muswada wa bajeti kati ya Donald Trump na Elon Musk umeongeza sintofahamu kuhusu hatima ya bajeti ya Shirika la Anga za Juu la Marekani (NASA). NASA tayari inakabiliwa na kupunguzwa kwa kiasi kikubwa cha bajeti.
Shirika hilo, lililowasilisha mapendekezo yake ya bajeti kwa Bunge la Marekani, pia lilipendekeza kupunguza ufadhili wa miradi ya kisayansi kwa karibu nusu. Miradi mikubwa 40 ya sayansi ya anga za juu, iwe bado inatengenezwa au tayari iko njiani, inakabiliwa na hatari ya kusitishwa.
Rais wa Marekani Trump ametishia kujiondoa katika mikataba inayohusisha kampuni ya Elon Musk, SpaceX. NASA inategemea roketi ya Falcon 9 ya SpaceX kutuma wafanyakazi na vifaa kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (International Space Station).
NASA inatarajia kutuma wanaanga mwezini na sayari ya Mars kwa kutumia roketi ya Starship, lakini roketi hiyo bado iko katika awamu za awali.
Chanzo cha picha, Reuters
Kuathiri hatma ya baadaye ya NASA
Dkt. Simeon Barber, mwanasayansi wa anga za juu kutoka Open University, alisema sintofahamu hiyo itakuwa na "athari ya kukatisha tamaa" kwenye mpango wa kupeleka binadamu angani.
"Mabadiliko ya kushangaza, maamuzi ya ghafla, na migongano tuliyoishuhudia wiki iliyopita inafifisha misingi ya malengo yetu. Sayansi ya anga na utafiti hutegemea mipango ya muda mrefu, na ushirikiano kati ya serikali, makampuni, na taasisi za elimu," alisema.
Mbali na mgogoro kati ya Rais Trump na Musk, kuna pia wasiwasi juu ya ombi la NASA la kupunguza bajeti kwa kiasi kikubwa. Akiba inatarajiwa katika idara zote isipokuwa mpango wa kutuma wanaanga kwenye sayari ya Mars, ambao utaokoa dola milioni 100.
Casey Dreyer, mkuu wa sera za anga kutoka taasisi ya Planetary Society yenye makao yake makuu Pasadena, alisema upunguzaji huo ni mfano wa mpango wa anga wa Marekani unaokabiliwa na mgogoro usio na kifani.
Chanzo cha picha, NASA
Misheni 40 Kusitishwa
"Elon Musk na Jeff Bezos mmiliki wa kampuni ya anga ya Blue Origin, wanatoa fedha kwa ajili ya maendeleo ya njia mbadala za mfumo wa Anga unaoitwa Space Launch System (SLS), roketi mpya iliyoundwa kwa ajili ya wanaanga wa Marekani wanaokwenda Mwezini.
Ikiwa kampuni hizo zitapoteza ile hamu na nia ya kuendelea na shughuli, na SpaceX au Blue Origin wakisema wanahitaji uwekezaji zaidi kukuza mifumo yao, Bunge linapaswa kuwapa ufadhili," Dkt. Adam Baker, mchambuzi wa anga kutoka Chuo Kikuu cha Cranfield anaamini hivyo.
"Zaidi ya hayo, kuna hatari ya uharibifu kwa misheni 40 za kuchunguza sayari nyingine na kufuatilia athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani kutoka angani. Nyingi zinahusisha mashirika ya kimataifa." Dkt. Barber alilalamika, "Inasikitisha sana kuona kitu kilichojengwa kwa bidii kiasi hicho kisha kubomolewa ghafla bila mipango yoyote ya kukijenga upya."
Kati ya miradi inayokabiliwa na kupunguzwa, "Tayari tumetumia gharama za kuendeleza na kuzindua misheni nyingi. Tukizisitisha sasa, kutakuwa na akiba ndogo tu katika gharama za uendeshaji. Na hakutakuwa na faida kubwa."
Chanzo cha picha, Getty Images
Mzozo kugusa mikataba ya Ulaya?
Pia kuna wasiwasi kuhusu mikataba miwili na European Space Agency. Mmoja ni mpango kabambe wa kurudisha duniani uchafu kutoka sayari ya Mars uliokusanywa na rover ya Perseverance ya NASA, na mwingine ni misheni ya kutuma rover ya Rosalind Franklin ya Ulaya kwenye sayari hiyo kutafuta dalili za uhai.
Wakati mabadiliko hayapendezi, ni "fursa ya kufikiria jinsi Ulaya inaweza kufanya vizuri zaidi katika shughuli zake za anga," alisema Profesa Sir Martin Sweeting, mkuu wa shirika la anga la Uingereza Surrey Satellite Technology Limited na mwandishi mwenza wa ripoti ya Royal Society kuhusu mustakabali wa anga.
Lakini alionya kwamba Ulaya inaweza kuteseka sana kwa muda mfupi. ESA ilisema katika makala iliyochapishwa hivi karibuni, "Tutajitahidi kuendelea kuwa mshirika imara na anayetegemewa na mashirika ya anga duniani kote, ili kuendeleza uwezo wetu huru katika anga."
Maoni haya yanakusudiwa kudokeza kuwa watafanikisha hilo wakiwa na NASA au bila NASA.
Chanzo cha picha, Getty Images
Dkt. Baker alisema pia kuna upunguzaji wa ufadhili kwa programu zinazoendelea na zilizopendekezwa za utafiti wa dunia. "Programu hizi za ufuatiliaji wa ardhini hutoa onyo la mapema kuhusu hatari za mazingira zijazo," aliiambia BBC News. Kuzisitisha kunamaanisha... "Uwezo wetu wa kutabiri na kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa utapunguzwa sana. Itakuwa jambo baya sana kufunga mfumo huu wa tahadhari ya mapema," alisema.
Mapendekezo ya bajeti bado hayajaidhinishwa na Bunge. Warepublican wengi wamewaambia waelekezi kwa siri kwamba wako tayari kupiga kura dhidi ya kupunguzwa, Cassie Dreyer wa Planetary Society aliiambia BBC News.
Dreyer alieleza wasiwasi kwamba bajeti yoyote inaweza isipitishwe kutokana na mkwamo wa kisiasa. Kupunguzwa kwa bajeti ya Ikulu ya White House kuna uwezekano wa kuwa hatua ya muda ambayo inaweza kuwa ngumu kubadilisha baadaye, kwa sababu mara tu misheni za anga zikisimamishwa, ni ngumu kuzianzisha tena.
Pia unaweza kusoma:Imetafsiriwa na Yusuph Mazimu na kuhaririwa na Ambia Hirsi