Chanzo cha picha, Getty Images
Dakika 26 zilizopita
Televisheni ya taifa ya Iran iliripoti Jumamosi kwamba Iran imepata hati nyeti za nyuklia za Israel kupitia "uvamizi mkubwa wa kijasusi." Ripoti hiyo haikutoa maelezo ya kina juu ya jinsi Iran ilipata ufikiaji wa hati hizo.
Habari hiyo ilitangazwa kwa ufupi kwenye TV ya serikali kwamba "huduma za kijasusi za Iran zimepata taarifa na nyaraka za kimkakati na nyeti, ikiwa ni pamoja na maelfu ya nyaraka zinazohusiana na miradi na vifaa vyake vya nyuklia (Israeli)."
Israel bado haijatoa maoni yoyote kuhusu dai hili la Iran.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Tasnim, Waziri wa Ujasusi wa Iran Hojatoleslam Seyyed Esmail Khatib alisema kuwa "nyaraka za nyuklia za Israel zimehamishiwa Iran.
Amesema, Nyaraka tulizozipata kutoka kwa serikali ya Kizayuni zinahusiana na mpango wake wa nyuklia na pia zina taarifa nyingi kuhusu Marekani, Ulaya na nchi nyinginezo.
Habari hizi zinajiri wakati ambapo mpango wa nyuklia wa Iran unajadiliwa na Israel inayoona mpango huo kuwa tishio la kweli kwake. Marekani pia inaongeza shinikizo kwa Iran kusaini mkataba mpya wa nyuklia.
Mnamo Machi mwaka huu, kwa mujibu wa CBS News, mshirika wa BBC wa Marekani, Rais wa Marekani Donald Trump alisema katika mahojiano kwamba "ikiwa (mamlaka za Iran) hazitafanya makubaliano, basi kutakuwa na mashambulizi ya mabomu na mabomu ambayo hawajawahi kuonekana."
Akijibu, Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alionya kwamba ikiwa Marekani itaishambulia Iran, kwa kuzingatia tishio la Rais Donald Trump, kutakuwa na jibu kali.
Pia unaweza kusomaChanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Ayatollah Ali Khamenei amesema, "Marekani na Israel zimekuwa zikituchukia siku zote. Wanatutishia kwa mashambulizi ambayo hatufikirii yana uwezekano mkubwa, lakini ikiwa watafanya uovu wowote, bila shaka watapewa jibu kali."
Donald Trump aliambia Fox News kwamba amemwandikia barua Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei akimkaribisha kufanya mazungumzo.
Ingawa Iran inaendelea kufanyia kazi mpango wake wa nyuklia, wataalamu wanaichukulia Israel kuwa nchi pekee yenye nguvu za nyuklia katika Mashariki ya Kati.
Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, mshirika mkuu wa kimkakati wa Israel, zinaishutumu Iran kwa kumiliki silaha za nyuklia, lakini Iran imekanusha madai hayo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, Rafael Mariano Grossi, ameonya kwamba Iran "haiko mbali" na kutengeneza bomu la nyuklia.
Aidha amefafanua kuwa "Iran kwa sasa haina silaha za nyuklia, lakini ina malighafi zinazohitajika kwa ajili yake.
Katika mahojiano na gazeti la Financial Times la Uingereza amesema kuwa, Iran hivi sasa ina akiba kubwa na inayoongezeka ya urani iliyorutubishwa kwa asilimia 60. Pia amesema uwezo wa nyuklia wa Iran hauwezi kuangamizwa kwa shambulio moja.
Iran ilikataa msimamo wa mkuu wa IAEA, ikijibu kuwa "hakuna kikomo kwa kiwango cha kurutubisha."
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na Shirika la Nishati ya Atomiki zimetoa taarifa ya pamoja ikielezea masikitiko yake juu ya kuchapishwa ripoti hiyo ambayo wameiita "taarifa ya kisiasa" na kusisitiza kuwa Tehran imethibitisha mara kadhaa kutokuwepo maeneo au shughuli zozote za nyuklia ambazo hazijatangazwa.
Iran yadai ufikiaji wa hati nyeti
Chanzo cha picha, Tasneem
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran la Fars News, "huduma za kijasusi za Iran zimefaulu kuhamisha kiasi kikubwa cha taarifa za kimkakati na nyeti na nyaraka, ikiwa ni pamoja na miradi na suhula za nyuklia, kutoka katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu."
Shirika hilo limeitaja operesheni hiyo kuwa "shambulio kubwa zaidi la kijasusi" dhidi ya Israel katika historia.
Iran mara kwa mara hutangaza kukamatwa kwa watu binafsi kwa tuhuma za ujasusi na kuishutumu Israel kwa "mauaji yaliyolengwa au vitendo vya hujuma vinavyohusishwa na mpango wake wa nyuklia."
Kinyume chake, mnamo Mei 2025, Israeli ilikamata watu wawili wanaoshukiwa kufanya kazi za kukusanya kijasusi kwa niaba ya Iran.
Shirika la habari la Iran liliripoti, likinukuu vyanzo vya habari, kwamba "maelfu ya nyaraka zinazohusiana na miradi ya nyuklia ya Israel ni miongoni mwa vitu vilivyokamatwa."
Kwa mujibu wa habari, operesheni hii ilifanyika kitambo, lakini kutokana na wingi wa nyaraka na haja ya kusafirisha kwa usalama shehena yote hadi Iran, operesheni hiyo ilifanywa kuwa siri.
Vyanzo vya habari vilithibitisha kwamba hati nyingi zitawasilishwa katika maeneo "salama". Kulingana na wao, kuna hati nyingi sana ambazo itachukua muda mwingi kuzipitia na kutazama picha na klipu zilizomo kwenye hati hizi.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametishia mashambulizi ya kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran. Iran inasisitiza juu ya haki yake ya nishati ya nyuklia ya kiraia, haswa kwa uzalishaji wa umeme, chini ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia, ambayo imeutia saini.
Mvutano kati ya nchi hizo mbili ulifikia kilele chake mwaka jana wakati Iran iliposhambulia moja kwa moja ardhi ya Israeli mara mbili kwa mamia ya makombora au droni.
Iran ilidai kuwa mashambulio hayo yalikuwa jibu la kufaa kwa mashambulizi mabaya ya Israel dhidi ya ubalozi wake mdogo nchini Syria.
Tehran ilikuwa imetangaza kulipiza kisasi kwa mauaji katika ardhi yake ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh na mauaji ya aliyekuwa Katibu Mkuu na mshirika wa Hizbullah, Hassan Nasrallah.
Iran inailaumu Israel kwa mauaji ya viongozi wote wawili waliodai kumuua Hassan Nasrallah katika shambulio la anga.
Operesheni ya Mossad
Mnamo mwaka wa 2018, shirika la ujasusi la Israeli Mossad lilifanya operesheni ya siri ndani ya Iran, ikilenga ghala moja huko Tehran ambalo lilikuwa na kumbukumbu za mpango wa nyuklia wa Iran.
Kulingana na mkuu wa zamani wa Mossad Yossi Cohen, operesheni hiyo ilipangwa kwa miaka miwili na ilihusisha maajenti 20, wote wasio Waisraeli, ambao walifanikiwa kufungua 'sefa' 32 za chuma na kuwasilisha nusu tani ya hati kwa Israeli kwa usiku mmoja.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Ufaransa AFP, Mossad waliiba takriban nyaraka 100,000 na faili katika muda wa saa sita na nusu kabla ya walinzi kuwasili mapema asubuhi. Nyaraka zilizoibiwa zilijumuisha faili za kidijitali zilizorekodiwa kwenye CD.
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Israel Haaretz, operesheni hiyo ilifanywa baada ya ufuatiliaji wa karibu wa tovuti hiyo tangu Februari 2016, wakati Wairani walianza kuhamisha hati hizo.
Hati hizo zilifichua maelezo ya kina kuhusu mpango wa Imad, ukijumuisha maeneo ya siri (kama vile Varam na Turkestan), taarifa kuhusu miundo ya vichwa vya nyuklia na operesheni za siri, na ramani za vichuguu vinavyotumika kuficha shughuli za urutubishaji.
Pia unaweza kusomaImetafsiriwa na Seif Abdalla