Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Mallory Moench and Flora Drury
- Nafasi, BBC News
Dakika 22 zilizopita
Ahmad amekuwa akijificha nchini Afghanistan kwa miaka kadhaa.
Mfanyakazi huyo wa zamani wa jeshi la Afghanistan anaishi kwa hofu ya kupatikana na Taliban, ambayo iliingia madarakani mwaka 2021 wakati vikosi vya Marekani vilipojiondoa katika taifa hilo la Asia ya Kati.
Kutokana na hilo, Ahmad hawezi kupata kazi wala huduma za matibabu na amekuwa akitegemea misaada kutoka kwa wahisani na marafiki walio nje ya nchi kujikimu kimaisha. Mwanawe wa kiume aliye na umri wa miaka 12, hawezi kuenda shule.
Wakinipata, Ahmad ''wataniangamiza'' anasema, akiashiria Taliban.
Matumaini yake yalikuwa mpango wa Marekani wa kuwapokea wakimbizi wanaokabiliwa na hali kama yake nchini Marekani, na alikuwa amesalia hatua ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kukamilisha mpango huo - kabla ya mchakato mzima wa uhamiaji kusitishwa na utawala wa Trump
Bado, alikuwa na matumaini. Lakini matumaini hayo yalididimia Alhamisi wiki iliyopita alipoamkia taarifa za Rais Marekani Donald kutoa agizo mpya ya kuwapiga marufuku watu walio na pasipoti za Afghanistan kuingia nchini humo, akitaja vitisho vya usalama wa taifa
"Mimi sio tishio kwa usalama wa Marekani," Ahmad aliiambia BBC.
BBC haitaji jina lake halisi ili kulinda usalama wake.
"Tulikuwa Marafiki wa Marekani," alisema.
Marufuku ya usafiri ya Trump iliyoanza kutekelezwa Jumatatu, inawazuia raia wa Afghanistan na mataifa mengine 11, zikiwemo saba kutoka barani Afrika kuingia Marekani. Nchi zingine saba pia zimewekewa vikwazo vya muda.
Kulingana na Marufuku hiyo, Afghanistan ilijumuishwa kwa sababu Taliban inachukuliwa na serikali ya Marekani na nchi hiyo haina "mamlaka kuu yenye uwezo au ushirikiano wa kutoa pasipoti au hati za kiraia", au "hatua zinazofaa za uchunguzi na ukaguzi". Pia inabainisha kiwango cha juu kiasi cha watu ambao wanaishi nchini humo licha ya muda wa viza zao kukamilika.
Utawala wa Trump, hata hivyo, hivi karibuni uliondoa hadhi ya muda ya ulinzi kwa zaidi ya Waafghani 9,000 wanaoishi Marekani, ikisema kuwa tathmini yake ilionyesha hali ya usalama na kiuchumi nchini Afghanistan imeimarika.
Lakini wale wanaoishi Afghanistan wanakabiliwa na msururu wa vikwazo vilivyowekwa na serikali ya Taliban kulingana na tafsiri yake kali ya Sharia ya dini ya Kiislamu..
Zile zinawaathiri wanawake - ni pamoja na kufinika nywele kwa lazima kuvaa hijab), vikwazo vya usafiri na masomo kwa wasichana walio na umri wa zaidi ya miaka 12 - hatua ambayo ni "ubaguzi wa kijinsia", kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Taliban inasema inaheshimu haki za wanawake kulingana na Sharia na utamaduni wa Afghanistan.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2023 iligundua kuwa kulikuwa na visa vya kuaminika kwamba mamia ya maafisa wa zamani wa serikali na wanajeshi wameuawa tangu kundi hilo liliporejea madarakani mwaka 2021, licha ya msamaha wa jumla. Taliban imesema hapo awali Waafghanistan wote wanaweza "kuishi nchini bila hofu yoyote" - na wale walio nje ya nchi wanapaswa kurejea kusaidia kujenga upya nchi.
"Kuna msamaha wa jumla," Mohammad Suhail Shaheen, balozi wa Taliban nchini Qatar, aliiambia BBC mapema mwaka huu. "Usalama wa umeimarishwa kote nchini Afghanistan. Kila raia na anaweza kufika sehmu yoyote ya nchi bila vikwazo vyovyote au matatizo yoyote."
Marufuku ya Trumpinatoa msamaha kwa kundi maalum la wahamiaji - ikiwa ni pamoja na Waafghanistan ambao walifanya kazi moja kwa moja na jeshi la Marekani kabla ya Taliban kurejea madarakani mwaka 2021.
Lakini Ahmad, ambaye maombi yake ya kupata makazi mapya yaliungwa mkono na mwanachama wa zamani wa huduma ya Marekani, hastahili kupata Viza Maalum ya Wahamiaji (SIV) kwa sababu hakufanya kazi moja kwa moja Marekani.
Na sio yeye pekee anayejipata katika hali hiyo.
Takriban raia 200,000 wa Afghanistan wamepatiwa makazi mapya tangu jeshi la Marekani lilipojiondoa nchini humo, lakini bado kuna maelfu zaidi wanaosubiri hatima yao kuamuliwa.
Baadhi yao wamekimbilia nchi jirani ya Pakistan ili kusubiri uamuzi kufanywa kuhusu maombi yao.
Samira, ambaye alizungumza na BBC Idhaa ya Afghanistan, kwa sasa yuko Pakistan- ambayo imekuwa ikiwafukuza maelfu ya raia wa Afghanistan katika miezi ya hivi karibuni.
"Kurejea Afghanistan sio chaguo kwetu - itakuwa changamoto kubwa," alisema. "Watoto wetu tayari wamepoteza miaka ya elimu, na hatuna matumaini ya kurudi salama."