Mwananchi Communications Limited
Baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutoka hadharani na kuijibu Yanga kuhusu madeni inayowadai, klabu hiyo imeibuka tena.
Katika taarifa kwa umma iliyowekwa kwenye kurasa rasmi za mitandao ya kijamii ya Klabu ya Yanga, imeeleza hivi: “Tumeona taarifa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuwa inaidai Klabu ya Young Africans bila kutoa ufafanuzi wa deni lenyewe.
“Tunapenda kuujulisha umma kuwa Klabu ya Young Africans haijawahi kulipwa fedha yoyote ya ubingwa wa Kombe la Shirikisho kwa misimu mitatu mfululizo (2021/2022, 2022/2023 na 2023/24).
“TFF wamekuwa wakishikilia fedha hizi za ubingwa kwenye akaunti zao kila msimu unapomalizika huku wakifahamu ni makosa na ni kinyume cha utaratibu.
“Hakuna uthibitisho wowote wa kimaandishi kuonyesha kama TFF wamewahi kulipa fedha hizi za ubingwa kwa Klabu ya Yanga.
“Ni aibu na fedheha na kumtia dosari mdhamini kuendesha mashindano bila kumlipa Bingwa kwa misimu mitatu mfululizo.
“Tunaelekeza, dawa ya deni ni kulipa kwa wakati ikiwa ni haki ya mshindi na inampa heshima mdhamini wa mashindano.
“leleweke, ada za malipo ya wachezaji wa kigeni walizozisema kwenye taarifa yao hulipwa mwanzo wa msimu mpya na hela hizi za Ubingwa hutolewa Mwisho wa msimu.
“Klabu ya Young Africans haijawahi kupokea taarifa yoyote rasmi kutoka TFF kuhusu Klabu yetu kuwa na deni kwao.
“Uongozi wa Klabu ya Young Africans unaendelea kusisitiza kulipwa pesa yake ya Ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB, kwa msimu wa 2023/24 ili tuweze kucheza mchezo wa Fainali siku ya tarehe 28 Juni, 2025.”