Mwananchi Communications Limited
TAARIFA kutoka Rwanda zinabainisha nahodha wa kikosi cha APR FC, Claude Niyomugabo anatakiwa na Azam FC kwa ajili ya msimu ujao.
Beki huyo wa kushoto mwenye umri wa miaka 26, alikuwa mchezaji muhimu wa APR katika msimu uliomalizika hivi karibuni wakati timu hiyo ikitwaa mataji mawili ambayo ni Ligi Kuu ya Rwanda na Kombe la Amani.
"Baada ya msimu wa soka Rwanda kumalizika, kumekuwa na taarifa kadhaa za usajili wakati huu ambao timu zinajiandaa kwa ajili ya msimu ujao.
"Katika maandalizi hayo, kuna wachezaji wanasajiliwa na wengine kutakiwa na timu zingine na miongoni mwa wanaotajwa kuondoka ni nahodha wa APR, Claude Niyomugabo ambaye anahusishwa na Yanga," alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza.
"Azam inaona kwa kuwa Niyomugabo alikuwa mchezaji muhimu katika mafanikio ya APR bila shaka atakuwa msaada kwao kwa msimu ujao wakati timu hiyo itakaposhiriki michuano ya kimataifa."
Beki huyo katika Ligi Kuu ya Rwanda msimu wa 2024-2025 uliomalizika hivi karibuni, alicheza mechi zote 30 na kuisaidia APR kuwapiku wapinzani wao Rayon Sports.
Mbali na APR, Niyomugabo ni mchezaji muhimu katika kikosi cha timu ya taifa ya Rwanda na alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshiriki michuano ya CHAN 2023.
Azam ambayo ina tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, eneo la beki wa kushoto amekuwa akicheza zaidi Pascal Msindo, hali inayoilazimu timu hiyo kuboresha eneo hili baada ya mapema mwaka huu Cheick Sidibe raia wa Senegal kutimkia HJK Helsinki ya Finland.