Mwananchi Communications Limited
Muktasari:
- SIKU moja baada ya Yanga kusema haitocheza mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Singida Black Stars msimu huu hadi itakapolipwa fedha za zawadi za msimu uliopita, Benki ya CRDB inayodhamini mashindano hayo imetoa ufafanuzi.
Yanga ilitwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho (FA) msimu wa 2023/2024 baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 6-5 dhidi ya Azam kwenye fainali iliyochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Juni 2, 2024.
SIKU moja baada ya Yanga kusema haitocheza mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Singida Black Stars msimu huu hadi itakapolipwa fedha za zawadi za msimu uliopita, Benki ya CRDB inayodhamini mashindano hayo imetoa ufafanuzi.
Benki hiyo imesema kuwa ilishafanya malipo ya fedha hizo kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
“Benki ya CRDB inapenda kutoa ufanunuzi wa madai yaliyotolewa na Msemaji wa Klabu ya Yanga katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika tarehe 09 Juni 2025 katika Makao Makuu ya klabu hiyo.
“Katika mkutano huo, Msemaji wa Klabu hiyo alinukuliwa akitoa taarifa kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kwetu kama Mdhamini Mkuu wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la Benki ya CRDB kuwa Klabu ya Yanga haitocheza fainali za mashindano hayo msimu huu kama hawatolipwa fedha za ubingwa wa msimu uliopita.
“Tungependa kufahamisha umma na wadau wote wa soka kuwa Benki ya CRDB ni taasisi yenye kuzingatia weledi, kanuni na taratibu na kwa msingi huo tayari Benki ilikwishatekeleza kikamilifu wajibu wake wa kifedha kwa TFF kama sehemu ya makubaliano ya udhamini wa mashindano haya. Malipo yote ya msimu uliopita yalifanyika kwa TFF kwa mujibu wa mkataba baina ya Benki ya CRDB na TFF.
“Benki ya CRDB inatambua kuwa mbali na mchezo wa soka kuunganisha jamii yetu na kutoa burudani, lakini pia mchezo huu ni ajira kwa vijana wengi, hivyo dhamira yetu ni kuendelea kushirikiana na TFF, vilabu na wadau wengine katika kukuza mchezo huu kwa maslahi mapana ya Taifa letu,” imefafanua taarifa hiyo ya CRBD.
Jana Jumatatu, Juni 9, 2025, Ałły Kamwe alisema kuwa Yanga inajiandaa kutocheza mechi ya fainali ya michuano hiyo kwa vile haijapewa fedha zake za zawadi ya ubingwa za msimu uliopita.
“Taarifa hii iwafikie ofisi ya Katibu Mkuu wa TFF na wadhamini wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la CRDB kuwa hatutacheza mchezo wa Fainali wa CRDB siku ya tarehe 28 mpaka tutakapolipwa hela yetu ya ubingwa kwa msimu uliopita. Tumevumilia dharau hizi kutoka kwa mamlaka za soka kwa muda mrefu sana. Sasa imefika mwisho. Hii ya Zanzibar pia hatutacheza,” alisema Kamwe.
Alipopigiwa kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma hizo za Yanga, Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo alisema yuko msibani.
“Sipo katika mazingira mazuri, nipo msibani,” amesema Ndimbo.