.

Maelezo ya picha, Mwanamke akifanya ibada ya maombi
  • Author, Abdalla Seif Dzungu
  • Nafasi, BBC Swahili
  • Twitter, @SeifDzungu
  • Akiripoti kutoka Nairobi Kenya
  • Dakika 14 zilizopita

Utafiti mpya wa kituo cha Utafiti cha Pew umebaini kwamba Afrika ya jangwa la Sahara imelipiku bara Ulaya kama sehemu ilio na Wakristo wengi duniani.

Kulingana na ripoti hiyo Pew inasema kwamba hali hiyo imesababishwa na kuzaliwa kwa wingi kwa wafuasi wa dini hiyo Afrika huku wafuasi wanaoishi Ulaya wakipungua kwasababu ya kujiondoa katika dini hiyo.

Hatahivyo ripoti hiyo kuhusu Jinsi Mandhari ya Kidini Ulimwenguni Ilivyobadilika Kuanzia 2010 hadi 2020 iliotolewa tarehe 9 mwezi Juni 2025, inasema kwamba Uislamu ndio kundi la kidini lililokuwa kwa kasi zaidi katika muongo huo.

Idadi ya Waislamu iliongezeka kwa wafuasi milioni 347 - zaidi ya dini nyingine zote kwa pamoja, ikipanda kutoka pointi 1.8, hadi 25.6%.

Kulingana na Pew, Idadi hiyo ya Waislamu inakadiriwa kuongezeka kwa angalau pointi 5 katika mataifa ya Kazakhstan, Benin na Lebanon, na kushuka kwa angalau pointi 5 nchini Tanzania na Oman.

Ripoti hiyo inasema kwamba licha ya Wakristo kusalia kuwa kundi kubwa zaidi la kidini ulimwenguni, wafuasi wa dini hiyo hawakuendana na kasi ya ongezeko la watu duniani kuanzia 2010 hadi 2020.

''Wakristo, wanaojumuika katika madhehebu mbalimbali, wanasalia kuwa kundi kubwa zaidi la kidini duniani - wengi wakiwa katika maeneo yote isipokuwa maeneo ya Asia-Pacific, Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini - lakini "wanapungua kama sehemu ya idadi ya watu duniani, kwasababu wanajiondoa katika dini ," Pew inasema.

Utafiti wa awali wa Pew ulikadiria kuwa Waislamu ndio kundi la kidini linalozaana sana likiwa na wastani wa watoto 3.1 kutoka 2010-2015, huku Wakristo wakifuata, na watoto 2.7.

Pia unaweza kusoma

.

Maelezo ya picha, Wafuasi wa dini ya Kikristo wakiwa kanisani

'Wakristo wanaihama dini yao'

Katika utafiti mpya, Pew imesema kwamba ingawa "Wakristo wana kiwango cha juu cha uzazi ... wamekuwa wakipoteza wafuasi wakati wanapoacha Ukristo na kuwa wasio na dini."

Imeongezea kuwa Budha ndio kundi kubwa la kidini pekee ambalo lilikuwa na wafuasi wachache mwaka 2020 ikilinganishwa na muongo mmoja uliopita.

Idadi ya wafuasi wa Budha ulimwenguni ilipungua kwa milioni 19, na kufikia milioni 324, ikushuka kwa pointi 0.8, hadi 4.1%.

Kwa upande mwingine, Wahindu walikua karibu sawa na idadi ya watu ulimwenguni.

Idadi ya Wahindu iliongezeka kwa milioni 126, na kufikia bilioni 1.2.

Vilevile Idadi ya Wayahudi ulimwenguni iliongezeka kwa karibu milioni 1, na kufikia milioni 14.8.

Kwa mujibu wa asilimia, Wayahudi walikuwa kikundi kidogo zaidi katika utafiti, wakiwakilisha karibu 0.2% ya idadi ya watu duniani.

Kwa pamoja, 75.8% ya watu duniani walitambuliwa na dini kufikia 2020. Asilimia 24.2 iliyobaki hawakujihusisha na dini yoyote, na kufanya watu wasio na dini kuwa kundi la tatu kwa ukubwa katika utafiti huu, baada ya Wakristo na Waislamu.

  • Wakristo ndio kundi kubwa zaidi la kidini ulimwenguni
  • Waislamu ndilo kundi la kidini lililokuwa kwa kasi zaidi kati ya 2010 na 2020
  • Karibu robo ya idadi ya watu ulimwenguni hawana uhusiano wa kidini
  • Afrika ya Jangwa la Sahara imeipiku Ulaya na kuwa eneo ambalo Wakristo wengi wanaishi
  • Idadi ya watu wasio na uhusiano wa kidini iliongezeka katika nchi 35
  • Uchina ina watu wasio na uhusiano wa kidini mara 7 zaidi ya Marekani na Japan zikijumuishwa
  • Uholanzi, New Zealand na Uruguay sasa zina watu wengi wasio na uhusiano wa kidini
  • Watu 3 wazima wameacha dini kwa kila mtu mzima aliyejiunga
  • Nchi zilizoendelea kiuchumi huwa na sehemu ndogo za watu wanaohusishwa na dini
  • Wakristo ndio kundi la kidini lililosambaa kwa usawa zaidi ulimwenguni
  • Idadi kubwa ya Waislamu duniani ni chini ya miaka 50
  • Asilimia 84 ya Wakristo wanaishi katika maeneo ambayo Ukristo ni dini ya wengi

.

Chanzo cha picha, Sohail Khan

Maelezo ya picha, Waislamu wakifanya maombi

'Kubadili' kidini

Licha ya kwamba watu wengi ulimwenguni bado wanajihusisha na dini ambayo walilelewa, mabadiliko ya kidini yameenea sana.

Kwa ujumla, kumekuwa na vuguvugu la watu kubadilika na kuwa jamii isiyohusishwa na dini yoyote.

Utafiti huu wa Pew Research Center ni wa kwanza kuripoti juu ya mifumo ya kuhama na kutoka kwa vikundi vya kidini katika ngazi ya kimataifa.

Katika nchi nyingi, mabadiliko haya yamefuata mtindo wa kizazi: Kila kizazi kipya cha vijana kina sehemu kubwa ya watu ambao hawana uhusiano wa kidini, ama kwa sababu hawakulelewa katika dini yoyote au kwa sababu wameacha dini ambayo wamelelewa.

Kwa kutumia tafiti kutoka nchi na maeneo 117, Pew ilichanganua data kutoka kwa watu wazima waliojibu na kulinganisha dini ambayo wanasema walilelewa (wakiwa watoto) na utambulisho wao wa sasa wa kidini (wakiwa watu wazima).

Kituo hicho kilitumia data kutoka kwa watu wazima wenye umri wa miaka 18 hadi 54 na kugundua kwamba kwa kila mtu mzima katika rika hilo ambaye anasema alijiunga na dini baada ya kulelewa bila dini, 3.2 waliacha dini kabisa baada ya kulelewa katika moja.

Kulingana na utafiti huo, Wakristo ndio waliopata hasara kubwa zaidi kutokana na kubadili (3.1 wameondoka kwa kila 1.0 aliyejiunga). Wakristo wengi waliojitenga na dini hiyo hawajihusishi tena na dini yoyote licha ya wengine kujiunga na dini tofauti.

Utafiti huo pia unasema kwamba Wabudha pia wamekuwa wakiytoka katika dini hiyo kuliko kujiunga nayo(1.8 kutoka, 1.0 kujiunga).

Vileivle Pew inasema kwamba Wahindu wamekuwa na wafuasi wengi wanaoondoka kuliko kujiunga, huku kinyume chake kikifanyika kwa dini ya Kiislamu