- Author, Esther Namuhisa
- Nafasi,
- Twitter, @enamuhisa
- Akiripoti kutoka BBC News, Dar es Salaam
Dakika 6 zilizopita
Khdija Mwanamboka, alianza na ndoto ya kipekee ya kutaka kuwa tofauti. Tangu akiwa mtoto, alijua hakutaka kuvaa nguo alizonunuliwa dukani, alitaka kubuni mavazi yake mwenyewe. Kila alipoandamana na mama yake kwenda dukani kununuliwa nguo alikataa ,kununuliwa kwa sababu akilini mwake alijiona kuwa mbunifu, si mteja wa mitindo.
Safari ya ubunifu kwake haikuanzia na ndoto ya biashara kubwa, bali na shauku binafsi. Mwaka 1996, akiwa msichana mdogo, alisimama kwenye jukwaa la Diamond Jubilee jijini Dar es salaam kwa mara ya kwanza. katika kipindi cha muda wa mapumziko baada ya kumaliza kidato cha nne, alipata muda wa kufanya majaribio kwa kuaandaa onyesho la mitindo kwa kuwakusanya rafiki zake ili kuonesha ubunifu wake.
Kwake, halikuwa onyesho la kawaida lilikuwa ni tangazo la ndoto yake.
Alitumia muda mwingi kusoma majarida ya mitindo, kuchora, na kujaribu kubadilisha maana ya mavazi ya asili kama khanga, batiki na vitenge kuwa mavazi ambayo yamekuwa yakihusishwa na shughuli za nyumbani, misiba, au ibada. Kwake khanga aliweza kutengeneza vazi la jioni la heshima..,Batiki ingeweza kuwa suti rasmi ya kuhudhuria sherehe za ubalozi. Anaamini alianza harakati zake kama muhamasishaji wa mavazi ya asili, akiamini kuwa mtindo unaweza kuwa sauti ya utaifa.
Chanzo cha picha, Khadija
Kujiamini kupitia mafanikio: Miss Tanzania na mlango mpya wa ujasiri
Chanzo cha picha, Khadija IG
Mwaka 1998, alitengeneza mavazi ya Basila Mwanukuzi katika mashindano ya Miss Tanzania ambapo Basila alishinda. Ushindi huo ulimtia nguvu isiyoelezeka: "Usiku huo ndipo nilijua naweza, Niliona kuwa ubunifu wangu unaweza kushindana kimataifa, na pia unaweza kubadilisha fikra za watu kuhusu mavazi ya asili."Na hiyo ilimpa mwanya wa kuendelea kubuni mavazi kwa walimbwende wengi wa Tanzania.
Kazi zake zikawa si tu mavazi, bali ujumbe wa utaifa. Alielewa kuwa mitindo ina sura mbili: biashara na harakati za kijamii. Ingawa hakuona faida ya kuuza zaidi ya wengine, alijiona kama mwanaharakati wa utaifa kupitia mitindo, akihamasisha watu kujivunia utamaduni wao kwa mavazi.
Kwa miaka mingi ameshona mavazi ya wanaume, wanawake na watoto. Akiwa na kipaji cha ubunifu wa hali ya juu, alijifunza pia kusimamia hisia zake. "Nikiwa sina furaha, siwezi kubuni. Lazima nijipe motisha kwa kufanya vitu vingine." Kwa mfano, licha ya kutopenda kupika, alipata msisimko mkubwa kwenye "packaging"akaamua kuweka nembo kwenye vyakula na kuuza mtandaoni kwa nembo ya Vitu vya Khadija.
Anakiri kuwa kwake, ubunifu ni sehemu ya maisha yake iwe ni mavazi, chakula, au tamasha.
Chanzo cha picha, Khadija
Chanzo cha picha, IG
Nguo mpya, Fikra mpya: Mitindo inavyobadili Maisha
Chanzo cha picha, IG-Khdija Mwanamboka
Kwa Khadija, nguo si tu kifaa cha kuvaa bali ni dawa ya kujiamini, faraja ya hisia, na chombo cha kubadilisha mtazamo wa mtu kuhusu maisha. "Hakuna kitu kinachobadilisha hali ya mwanamke kama kuvaa nguo mpya.,kama ulimwona jana akiwa na huzuni, msongo wa mawazo au hasira, lakini leo akivaa nguo mpya huyo ni mwanamke tofauti kabisa," anasema Khadija. Nguo mpya au kupendeza, kwake, ni tiba ya kihisia na anaamini ni kichocheo cha kujiamini kwa mwanamke yeyote. Inaweza kumfanya awe na furaha, kuchangamka kazini, au hata kuboresha mahusiano yake.
Mitindo, kwake, ni zaidi ya urembo, ni njia ya kumuinua mwanamke.
Na si wanawake au wanaume wakubwa tu. Ni imani hii ndio iliyomsukuma kuanza kufanya kazi na watoto wenye umri mdogo kuanzia miaka mitatu. Anaamini kuwa ubunifu unapaswa kuanza mapema, kama walivyo wachezaji wa mpira wanaofundishwa tangu utotoni. " miaka mitano sasa, Khadija amekuwa akifanya kazi na watoto, akiwahusisha kwenye maonyesho ya mitindo na kuwafundisha mbinu za ubunifu. Anaamini kuwa kipaji kinapaswa kulelewa mapema. "Kama wenzetu wanavyoanzisha watoto kwenye soka wakiwa wadogo, sisi pia tunaweza kuwapa nafasi kwenye mitindo."Sio lazima umlazimishe mtoto apende unachopenda, ila unaweza kumvutia, akajifunza na kuchagua mwenyewe." Akiwa na maono ya mbele, anaona kuwa kuwekeza kwa watoto ni kuwekeza kwenye mustakabali wa mitindo ya taifa.
Chanzo cha picha, IG
Vazi la Taifa na Dira ya Uzalendo
Chanzo cha picha, IG
Safari yake haikusimama kwenye majukwaa ya mitindo tu. Aliteuliwa kuwa mmoja wa wajumbe wa kuandaa vazi la taifa la Tanzania, jukumu alilolichukua kwa uzito mkubwa. Vazi hilo, ambalo litazinduliwa rasmi, limezingatia bendera, utambulisho wa kitaifa, na vivutio vya kiutamaduni vya nchi. "Ni heshima kubwa sana kwa mbunifu kushiriki kuandika historia ya taifa lake kupitia vazi., kwangu mimi ni faraja kubwa,"Khadija anaeleza.
Kwa mtazamo wake, anasema ili Watanzania wavutiwe kuvaa mavazi ya ndani, ni muhimu kuwekeza kwenye viwanda. "Fundisho moja kubwa ni kuwa si kila mtu anaweza kushonewa nguo na fundi mmoja, inachukua muda na gharama ni kubwa. Kama tukijenga viwanda vya kutengeneza mavazi kwa wingi na kwa bei nafuu, watu hawatakuwa na sababu ya kuvaa mitumba." Anaamini kuwa kazi ya mbunifu si tu kushona, bali pia kutafuta suluhisho la kiuchumi na kijamii katika tasnia ya mitindo.
Mbali na kazi zake za ubunifu, ameendelea kushiriki katika kazi za kijamii kama vile kushirikiana na wanawake wanaopambana na saratani, kuchangisha fedha za mahitaji muhimu, na kuwa balozi wa mitindo yenye maana. Hadi sasa, ameshinda tuzo tano za ubunifu, lakini kwake, mafanikio si mwisho. "Sio vyema kushiba mafanikio haraka. Unatakiwa kujifunza kila siku. Mimi nasoma fashion magazine kila mara. Dunia inabadilika, lazima na wewe ubadilike nayo."
.
Zaidi ya Mitindo: Mwanamke mbunifu ni mbadilishaji Jamii
Chanzo cha picha, Khadija Mwanamboka
Kwenye kila kipande cha khanga, kila mshono wa batiki, na kila suti yenye rangi za taifa kuna sauti ya mwanamke anayeamini katika ubunifu wenye maana. Sauti ya mwanamke ambaye alikataa kununua tu nguo, akachagua kubuni. Mwanamke ambaye ametumia mitindo kama jukwaa la kuhamasisha utaifa, kutoa furaha, na kubadili maisha ya wanawake na watoto kupitia ujasiri na maono.
Katika dunia inayobadilika kila siku, yeye ameendelea kuwa mwanga wa mabadiliko, mwanamke ambaye hatakumbukwa tu kwa mitindo aliyobuni, bali kwa moyo alioweka ndani ya kila mshono