Chanzo cha picha, AP
Dakika 35 zilizopita
Maafisa wa Marekani na Iran walifanya mazungumzo ya ana kwa ana mjini Muscat, mji mkuu wa Oman, kwa lengo la kuafikia makubaliano mapya kuhusu mpango tata wa nyuklia wa Iran.
Hapo awali, makubaliano ya nyuklia yalitiwa saini kati ya Iran na nchi zenye nguvu duniani, lakini mwaka wa 2018, Donald Trump alitangaza kwamba Marekani itajiondoa katika makubaliano hayo, na kwa kuweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran, alikasirisha rasmi Tehran.
Baada ya kuingia madarakani, Rais Trump alianza mazungumzo kuhusu makubaliano mapya ya nyuklia na Iran, na kuonya kwamba ikiwa mazungumzo haya hayataisha kwa mafanikio, huenda hatua za kijeshi zikachukuliwa dhidi ya taifa hilo.
Pia unaweza kusomaKwa nini Iran hairuhusiwi kuwa na silaha zake za nyuklia?
Iran inasisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa madhumuni ya amani.
Inasisitiza kuwa haitafuti kutengeneza silaha za nyuklia, lakini nchi nyingi na shirika la kimataifa la kudhibiti nyuklia, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), haziamini.
Mashaka kuhusu nia ya Iran yalizuka mwaka 2002 ilipogundulika kuwa nchi hiyo ina vifaa vya siri vya nyuklia.
Hii ina maana ya kukiuka kile kinachoitwa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia (NPT), uliotiwa saini na Iran na takriban nchi nyingine zote.
NPT inaruhusu nchi kutumia teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni yasiyo ya kijeshi kama vile dawa, kilimo na nishati, lakini hairuhusu uundaji wa silaha za nyuklia.
Je, mpango wa nyuklia wa Iran umepiga hatua kiasi gani?
Tangu Marekani ilipojiondoa katika mapatano ya nyuklia yaliyopo, yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA), mwaka 2018, Iran imekiuka majukumu yake ya msingi katika kukabiliana na kuwekewa upya vikwazo.
Iliweka maelfu ya centrifuge za kisasa (mashine za kusafisha) kurutubisha uranium iliyopigwa marufuku na JCPOA.
Uranium iliyorutubishwa hadi 90% inahitajika kwa silaha za nyuklia. Chini ya JCPOA, Iran inaruhusiwa tu kuhifadhi hadi kilo 300 za uranium iliyorutubishwa kufikia kiwango cha 3.67% - ambayo inatosha kwa nguvu za nyuklia za kiraia na madhumuni ya utafiti, lakini sio kwa mabomu ya nyuklia.
Hata hivyo, kufikia Machi 2025, IAEA ilitangaza kwamba Iran ina takriban kilo 275 za uranium na imerutubisha hadi 60%.
Iwapo Iran itarutubisha uranium zaidi, kinadharia itatosha kutengeneza silaha sita hadi saba.
Maafisa wa Marekani wamesema kuwa wanaamini kuwa Iran itaweza kubadilisha uranium hii kuwa nyenzo ya kutosha kwa bomu moja ndani ya wiki moja tu.
Sambamba na hayo wamesisitiza kuwa itachukua Iran mwezi mmoja hadi 18 kutengeneza silaha za nyuklia.
Wataalamu wengine wanasema kuwa bomu "rahisi" linaweza kufanywa kwa miezi sita au chini.
Kwa nini Trump alijiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia?
Tangu mwaka 2010, Umoja wa Mataifa, Marekani na Umoja wa Ulaya zimeiwekea Iran vikwazo vikubwa vya kiuchumi kutokana na tuhuma kwamba mpango wake wa nyuklia unatumiwa kutengeneza mabomu.
Vikwazo hivyo vimekatisha uuzaji wa mafuta ya Iran katika masoko ya kimataifa na kufungia mali ya nchi hiyo yenye thamani ya dola bilioni 100 za kigeni. Matokeo yake, uchumi wake umeporomoka, sarafu yake imeshuka hadi rekodi ya chini, na mfumuko wa bei umepanda.
Mwaka 2015, Iran na nchi sita - Marekani, China, Ufaransa, Urusi, Ujerumani na Uingereza - zilitia saini makubaliano ya JCPOA baada ya miaka mingi ya mazungumzo.
Mbali na kuzuia shughuli za Iran kuhusiana na mpango wake wa nyuklia, makubaliano haya yaliruhusu IAEA kuingia katika vituo vyote vya nyuklia vya Iran na kukagua maeneo yanayotiliwa shaka.
Kwa upande wake, nchi hizo zilikubali kuondoa vikwazo.
JCPOA ilipaswa kuwa halali kwa miaka 15, na baada ya hapo vikwazo vingeondolewa.
Chanzo cha picha, Getty Images
Trump aliuita "mpango mbaya" kwa sababu haukuwa wa kudumu na haukuangazia mpango wa makombora wa balistiki wa Iran, miongoni mwa masuala mengine.
Trump amerejesha vikwazo vya Marekani kama sehemu ya sera ya "shinikizo la juu" kuilazimisha Iran kufanya mazungumzo ya makubaliano mapya na yaliyopanuliwa.
Uamuzi wa Trump uliathiriwa na washirika wa Marekani katika eneo hilo, haswa Israeli.
Israel inadai kuwa Iran bado inaendeleza mpango wa siri wa nyuklia na imeonya kuwa Iran inaweza kutumia mabilioni ya dola katika msamaha wa vikwazo ili kuimarisha uwezo wake wa kijeshi.
Marekani na Israel wanataka nini sasa?
Kauli ya Trump kuhusu mazungumzo na Iran iliishangaza Israel. Ingawa kwa muda mrefu amekuwa akisema kwamba atafanya mapatano "bora" kuliko JCPOA, Iran hadi sasa imekataa kuyafanyia marekebisho mapatano hayo.
Trump hapo awali alionya kwamba Iran "itapigwa bomu" ikiwa haitaki kutia saini mkataba mpya.
Mshauri wake wa usalama wa taifa, Mike Waltz, alisema Trump anataka "uharibifu kamili" wa mpango wa nyuklia wa Iran, na "unaojumuisha urutubishaji, silaha, na mpango wake wa kimkakati wa makombora."
Iran inatarajia makubaliano ya kuweka kikomo, lakini sio kuondoa kabisa, mpango wake wa nyuklia badala ya kulegeza vikwazo.
"Lengo letu ni kufikia makubaliano ya haki na usawa kwa usawa," Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi alisema.
Ingawa Trump alisema kutakuwa na "mazungumzo ya moja kwa moja," Arakchi alisema mazungumzo ya Oman hayakuwa ya moja kwa moja, na mazungumzo mafupi tu kati yake na Balozi wa Marekani Steve Whitkoff yalifanyika walipokuwa wakiondoka.
Araqchi alisema kuwa Iran iko tayari kwa mazungumzo na Marekani, lakini Trump lazima kwanza akubali kwamba hakutakuwa na "njia ya kijeshi".
Chanzo cha picha, Reuters/Getty Images
Baada ya kauli hiyo ya Trump, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisisitiza kuwa makubaliano pekee yanayokubalika yatatiwa saini pale Iran itakapokubali kuharibu kabisa mpango wake wa nyuklia.
Aliieleza hivi: "Tutaingia na kulipua vifaa na kusambaratisha vifaa vyote chini ya usimamizi na udhibiti wa Marekani."
Wasiwasi mkubwa wa Israel ni kwamba Trump anaweza kukubaliana na maafikiano ambayo hayatasalimisha kabisa Iran, lakini yanaweza kuwasilishwa kama ushindi wa kidiplomasia.
Israel ambayo haijatia saini Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia, inaaminika kuwa na silaha za nyuklia, lakini haithibitishi wala kukanusha.
Anaamini kuwa kumiliki silaha za nyuklia na Iran ambayo haitambui haki ya Israel kuwepo duniani ni tishio kubwa.
Je, Marekani na Israel zinaweza kushambulia Iran?
Marekani na Israel zote zina uwezo wa kijeshi kulipua miundombinu ya nyuklia ya Iran, lakini operesheni kama hiyo itakuwa ngumu na ya hatari, na matokeo yake huenda yakawa na athari kubwa.
Vituo vikuu vya nyuklia vimezikwa chini ya ardhi, na ni mabomu yenye nguvu zaidi ya kulipua chini ya ardhi yanaweza kuvifikia. Ingawa Marekani ina mabomu kama hayo, haijulikani ikiwa Israeli inayo.
Iran italazimika kujilinda yenyewe, kushambulia malengo ya Marekani katika eneo hilo, na kurusha makombora kwa Israeli.
Kwa operesheni kama hiyo, Marekani labda itahitaji kutumia kambi zake za kijeshi katika Ghuba ya Uajemi, pamoja na meli zinazobeba ndege za kivita .
Hata hivyo, nchi kama vile Qatar, ambako ndiko kambi kubwa zaidi ya anga ya Marekani, huenda zisikubali kuisaidia Marekani kuishambulia Iran , kwa kuhofia kulipizwa kisasi.
Pia unaweza kusomaImetafsiriwa na Seif Abdalla