Mbu

Chanzo cha picha, SPL

  • Author, Ambia Hirsi
  • Nafasi, BBC Swahili
  • Akiripoti kutoka Nairobi
  • Dakika 27 zilizopita

''Ilianza na baba yangu mzazi wiki tatu zilizopita... Nilikuwa nimetoka kwa shughuli zangu za siku kama kawaida mara nikapigiwa simu kutoka nyumbani kuambiwa unajua baba hajatoka kitandani mpaka sasa? Nilipouliza kwa nini nikaambiwa anasema hawezi kuamka. Nilipokimbilia nyumbani nilimpata akiwa na maumivu makali hawezi kuinua hata mkono na analia kama mtoto mdogo'', ananiambia Mercy mkaazi wa Bamburi Mombasa, Kenya.

''Nilisthtuka sana manake mzee ana umri wa miaka 86 na kumuona akiwa katika hali hiyo bila shaka ni wazi amelemewa na ugonjwa. Hapo ndipo tulimkimbiza hospitali ambapo alifanyiwa vipimo na kupatikana na virusi vya chikungunya.''

Mercy anasema tangu baba yake alipopatikana na ugonjwa huo watu wengine wannne wa familia yake pia wamebainishwa kuugua chikungunya akiwemo yeye binafsi.

Unajua hii chikungunya dalili zake zinatofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine? aliniambia Mercy katika mahojiano yangu na yeye kwa njia ya simu.

''Yangu ilianza na maumivu ya kuumwa na kichwa nikadhani nina msongo wa mawazo nikasema wacha nitumie dawa za kutuliza maumivu pengine zitanisaidia ...lakini wapi? kesho yake nilizidiwa na maumivu hadi nikaenda hospitali kutafuta huduma za matibabu.

Sio Mercy na familia yake pekee inayokabiliwa na hali kama hii.

Wiki iliyopita Kaunti ya Mombasa Pwani ya Kenya ilithibitisha mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa Chikungunya ambao maafisa wake afya wameripoti kuwa umeenea katika maeneo mengine sita ya jimbo hilo.

Mkuu wa afya ya umma katika Kaunti ya Mombasa Fatma Ali, aliiambia BBC kuwa sampuli za damu zilizokusanywa na kupelekwa katika maabara ya kitaifa ya KEMRI na kufanyiwa vipimo vya DNA- RNA kuthibitisha uwepo wa ugonjwa huo.

Lakini je, unaufahamu ugonjwa wa Chikungunya ni nini na dalili zake ni zipi?

Chikungunya ni nini?

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO chikungunya ni ugonjwa unaonezwa na mbu jike aina ya Aedes aliyebeba virusi vya chikungunya.

WHO inasema kuna spishi mbili za Aedes zinasambaza ugonjwa huo ambazo ni Aedes aegypti na Aedes albopictus.

Spishi hizi mbili zinaweza pia kusambaza magonjwa mengine yanayoenezwa na mbu kama vile dengue. Mbu hawa hung'ata nyakati za mchana, ingawa wanaweza pia kung'ata asubuhi na alasiri.

Utajuaje unaugua chikungunya?

Kulingana na WHO dalili kuu za chikungunya ni homa ya ghafla ikiambatana na maumivu ya viungo.

Dalili nyingine za kawaida ni maumivu ya misuli, kuumwa na kichwa, kihisi kichefuchefu na kutapika, kuhisi uchovu na kutokwaa vipele. Maumivu ya viungo yanachosha kwani hudumu kwa siku moja hadi wiki kadhaa.

Dalili za chikungunya huonekana kati ya siku 4 na 7 baada ya mgonjwa kung'atwa na mbu aliyebeba vimelea vya chikungunya. Kwa ujumla dalili nyingi hudumu kwa siku 2 hadi 3 na ni nadra sana mtu kufa kwa chikungunya.

Baadhi ya wagonjwa hupona baada ya siku chache lakini wakati mwingine maumivu ya viungo yanaweza kudumu kwa wiki, miezi au hata zaidi

Nani yuko hatarini kupata chikungunya?

Mbu

Chanzo cha picha, Getty Images

Msafiri anakabiliwa na tishio la kupata kupata virusi vya chikungunya ikiwa utazuru nchi au ameneo ambayo yana mlipuko wa ugonjwa huo.

Kabla ya kusafiri, unashauriwa kuwasiliana na mtoa huduma wako wa afya au kufuatilia taarifa za mashirika ya afya kama vile Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kubaini kama sehemu unayozuru inakabiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa chikungunya.

Mama mjamzito aliye na virusi anaweza kumuambukiza mtoto aliye tumboni. Hata hivyo hakuna ushahidi unaoonyesha kwamba virusi vinaweza kueneakwa mtoto mchanga kupitia maziwa ya mama.

Lakini, wanawake ambao ni wajawazito wanaokaribia kujifungua wanashauriwa kusafiri kwenda maeneo yaliyo na mlipuko wa virusi vya chikungunya kwani zinaweza kupita kwa mtoto wao wakati wa kujifungua.

Athari za chikungunya ni zipi?

Baadhi ya wagonjwa hupona kikamilifu, lakini wakati mwingine maumivu ya viungo yanaweza kudumu kwa miezi kadhaa au hata miaka.

Matukio ya mara kwa mara ya matatizo ya jicho, mfumo wa mishipa ya fahamu na moyo yameripotiwa, pamoja na malalamiko ya utumbo.

Matatizo makubwa si ya kawaida, lakini ugonjwa huo unaweza kuchangia sababu ya kifo kwa wazee.

Mara nyingi dalili za watu walioambukizwa huwa hafifu na huenda maambukizi yasitambuliwe au kutambuliwa kimakosa katika maeneo ambayo homa ya dengue pia hutokea.

Chikungunya ina tiba?

Hakuna tiba mahususi dhidi ya virusi vya chikungunya na hakuna chanjo maalum ya kumkinga mtu dhidi ya chikungunya. Hata hivyo chanjo kadhaa zinatengenezwa kwa sasa.

Wataalamu wa afya wanasema kile ambacho mtu anapata iwapo amepatikana na chikungunya ni matibabu ya kudhibiti dalili zaidi na kupunguza maumivu.

Maumivu kwa kiasi kikubwa yanadhibitiwa kwa kutumia dawa za kushusha homa na kupunguza maumivu na zile za kupunguza maji mwilini.

Anayeugia chikungunya pia anashauriwa kunywa maji kwa wingi na kupata wasaa wa kupumzika.

Aspirini na dawa zingine za kupunguza maumivu na uvimbe hazipaswi kutumiwa hadi pale itakapothibitishwa kuwa mgonjwa hana dengue, kwani akipatiwa bila taarifa mahsusi mgonjwa anaweza kupata tatizo la kutokwa na damu.

Unawezaje kudhibiti maambukizi?

Moja ya njia ya kupambana na chikungunya ni kuangamiza mazalia ya mbu kwa kupuliza dawa

Chanzo cha picha, Getty Images

Kinga na udhibiti hutegemea sana kuondoa mazalia ya mbu anasema . Na wakati wa milipuko ya ugonjwa dawa za kuua wadudu zinaweza kunyunyiziwa kuua mbu wanaoruka, halikadhalika kuwekwa kwenye maeneo ya mazalia ya mbu kwenye makazi ya watu ili pia kuua viluilui vya mbu.

Unashauriwa kuvaa mavazi ya kufunika mwili kupunguza uwezo wa mbu kukung'ata, na pia unaweza kutumia dawa za kupaka kwenye ngozi.

Kwa wale wanaolala wakati wa mchana, hasa watoto wadogo, wagonjwa au wazee, vyandarua vilivyotiwa dawa vina uwezo wa kuwalinda dihdi ya mbu wanaoeneza virusi vya chikungunya.

Dawa za mbu za kuchoma na mashine za kutoa unyevunyevu wenye dawa nazo zinaweza kutumiwa ndani ili kuua mbu.

Pia unashauri kufika katika

Pia unaweza kupata maelezo zaidi kuhusiana na ugonjwa huo katika mahojiano hapo chini ambapo mwandishi wa BBC Jamhuri Mwavyombo amezungumza na Fatma Ali Mkuu wa afya ya umma katika Kaunti ya Mombasa.

Maelezo ya sauti, Unaufahamu ugonjwa wa Chikungunya?