Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC, Nairobi
- Akiripoti kutoka Nairobi
Dakika 30 zilizopita
Katika dunia ya karne ya sasa, wanaume wamejitosa kwenye urembo ingawa pengine tunaweza kusema idadi yao sio sawa na wanawake lakini inaendelea kuongezeka kila uchao.
Miaka ya sasa hivi, wanaume wamejitokeza kuwa wenye kujali muonekano wao na wengi kutoka kila pembe ya dunia wamekuwa wakitafuta huduma ya upasuaji kuimarisha muonekano wao wa sehemu tofauti za mwili.
Tuangazie wanaume 5 baadhi ya watu mashuhuri waliofanyiwa upasuaji kubadili muonekano wao.
1. Michael Jackson
Chanzo cha picha, Getty Images
Michael Jackson ni mmoja wa waimbaji maarufu duniani. Hakika katika tasnia hii alikuwa gwiji.
Pengine huenda alibadilisha muonekano wa sehemu zaidi ya moja lakini miongoni mwa vilivyovutia nadhari ilikuwa namna alivyobadilisha uso na pua yake.
Inasemekana kwamba alifanya upasuaji mara kadhaa ili uso wake uwe na usawa zaidi na uonekane kama wa kijana mdogo.
Katikati ya miaka ya 1990, Michael Jackson alikuwa tayari maarufu. Alijulikana kwa kuwa "mtu wa nyuso nyingi" na mara nyingi alivaa mabarakoa ili kuepuka wapiga picha wa kujitegemea.
Mnamo mwaka wa 1993, Michael Jackson alifanyiwa upasuaji wa pua pande zote mbili kwa siku moja, dhamira ikiwa kupunguza pua zake na kuzifanya zionekane zaidi.
Baadhi ya vyanzo viliripoti kuwa mnamo mwezi Januari 3, 2009, Jackson alilazwa katika kliniki ya kibinafsi kufanyiwa upasuaji wa kuboresha muonekano wake.
Utaratibu huo ulifanywa na Dk. Steven Hoefflin, ambaye hapo awali alikuwa ameshamfanyia Jackson upasuaji kadhaa wa uso.
Katika mahojiano na "Daily Mirror", Jackson alikiri kwamba amefanya upasuaji kadhaa na anapanga kufanyiwa tena ikiwa pua yake haitaboreka.
"Nimefanya upasuaji wa pua lakini nafkiri pua yangu inaonekana vizuri sasa," alisema. "Ila ikiwa inazidi kuwa mbaya katika siku zijazo basi pengine huenda nikafanyiwa tena."
Hatimaye, upasuaji huo ulimdhuru.
Duru zinasema pua yake ikawa ndogo sana kwa sababu alifanyiwa upasuaji mara nyingi.
Katika kipindi cha Oprah Winfrey, mamake Michael Jackson alikiri kuwa mtoto wake alipenda sana upasuaji wa kubadilisha umbo.
Katherine alisema katika mahojiano na Oprah Winfrey: "Hakutaka kuanza 'kuonekana kama muonekano wa ng'ombe', alisema (akimaanisha mabaka mabaka). Sijui alifanya nini lakini alibadilisha" muonekano wake.
Michael Jackson alifariki Juni 25 mwaka 2009 akiwa na umri wa miaka 50, kutokana na kuzidisha kipimo cha dawa ya usingizi na zingine za maumivu zilizopatikana kwenye mfumo wake.
Pia unaweza kusoma:2. Dwayne "Rock" Johnson
Chanzo cha picha, Getty Images
Dwayne "Rock" Johnson anajulikana kama mmoja wa wanaume wenye nguvu na misuli inayovutia.
Kabla ya upasuaji, alijitahidi kupata muonekano wa mwili anaotaka kwa kufanya mazoezi kwa muda mrefu.
Mwaka 2005, alifanywa upasuaji wa 'gynecomastia', utaratibu unaondoa mafuta mengi na tishu za tezi kutoka kwa kifua cha mwanamume.
Kwa sababu alitumia wakati mwingi bila kuvaa nguo ya kuziba kifua, iwe kwenye mieleka au kwenye skrini kuna uwezekano alihisi atajiamini zaidi baada ya kufanyiwa upasuaji huo.
2. Simon Cowell
Chanzo cha picha, Getty Images
Simon Cowell, wengi wanamtambua kama jaji kwenye kipindi cha America got talent, aliwahi kusema kuwa amefanyiwa upasuaji wa kuondoa makunyazi.
"Nimatumaini yangu nitakuwa na muonekano bora sasa - labda nilikuwa na makunyanzi kidogo sana miaka michache iliyopita, kwa sababu kila mtu kwenye Runinga anayo."
Simon amekuwa na uso unaoonekana mwororo kama wa kijana mwenye umri mdogo.
Lakini kando na kufanyiwa upasuaji huo, pia alibadilisha menyu yake.
Amekugeukia ulaji wa nyama nyeupe badala ya nyekundu na mbogamboga kwa wingi.
Na kutokana na mabadiliko hayo, amepunguza uzito sana.
4. Kanye West
Chanzo cha picha, Reuters
Mwanamuziki maarufu Kanye West alikubali kufanyiwa upasuaji wa kuondoa mafuta kwenye mwili wake maarufu kama 'liposuction' mnamo 2016 wakati wa maonyesho ya TMZ Live.
Nyota huyo aliogopa watu wangemdhihaki jinsi walivyofanya kwa Rob Kardashian, ambaye hakuhudhuria harusi ya dada yake Kim Kardashian kwa sababu ya mwili wake mkubwa.
"Nilifanyiwa upasuaji wa urembo kwa sababu nilikuwa najaribu kuonekana mzuri kwenu nyote. Nilifanyiwa 'liposuction', sikutaka muniite mnene kama vile ulivyomwita Rob kwenye harusi na akaamua kurudi nyumbani kabla yangu...," alisema kabla ya kurudia, "Sikutaka nyinyi nyote muniite mimi mnene, kwa hivyo nilifanyiwa liposuction."
Na baada ya kufanyiwa upasuaji huo, akawa mraibu wa dawa za kutuliza maumivu.
"Walinipa dawa za opioid na nikaanza kuzinywa mbili…", West alielezea, akisema upasuaji huo ulifanyika mnamo mwaka 2016 kabla ya kupata matatizo ya afya ya akili.
5. Jean-Claude Van Damme
Chanzo cha picha, Getty Images
Jean-Claude Van Damme alikuwa tayari maarufu nyumbani kwa mafanikio yake ya michezo, akiwa na umri wa miaka 16 na kuwa bingwa wa Karate wa Ulaya katika timu ya taifa ya Ubelgiji.
Lakini muda si muda, aligundua kuwa aina ya filamu za vita ilikuwa inazidi kuwa maarufu nchini Marekani, kwa hivyo, alifanya uamuzi mzuri wa kujitosa Hollywood.
Watayarishaji waligundua kuwa kijana huyo wa Ubelgiji sio tu alikuwa stadi katika mbinu zake za kupigana: wengi walipenda muonekano wake wa haiba ya juu na tabasamu la kipee ambalo hakusita kuonyesha pindi alipopata fursa ya kufanya hivyo.
Muigizaji huyo alirejelea mara kwa mara kuwa hayuko tayari kuzeeka na akiwa anaingia katika ujana, aliamua kufanyiwa upasuaji wa kuondoa makunyazi na kuwa na muonekanao wa kuvutia.
Ni mchakato unaofanya uso kuwa na muonekano wa kujaa jaa vizuri.
Alifanywa upasuaji wa kuinua uso na kope.
Kwa sasa hivi, umaarufu wa filamu za vita umepungua duniani, sio kama ilivyokuwa miaka ya 1990, kwa kuwa Van Damme ni mwigizaji, anarejea kwenye tasnia ya filamu muda wowote anapotaka kufanya hivyo.
Wanaume hawa mashuhuri ni mfano tu ya mamilioni ya wengi ambao siku hizi huchagua kufanyiwa upasuaji wa kuboresha muonekano, tofauti na zama za kale wakati ilidhaniwa ni wanawake tu ndio wenye kujitosa katika upasuaji wa kujibadilisha maumbile.