.

Chanzo cha picha, @modgovksa/X

Dakika 54 zilizopita

Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia ilichapisha kwenye mitandao ya kijamii baadhi ya picha zilizoonyesha helikopta ya kijeshi na mfumo wa ulinzi wa anga ukiwa umewekwa katika eneo karibu na Msikiti Mkuu katika mji mtakatifu wa Mecca.

Katika picha hizo zilizotolewa, Wizara ya Ulinzi ya Saudia iliandika, "Jeshi la Ulinzi la Anga...linawafuatilia kwa karibu, na dhamira yake ni kuwalinda wageni wa Mungu."

Mojawapo ya maeneo mawili kwenye picha hizo, katika mtandao wa 'X' wa Wizara ya Ulinzi ya Saudia, inaonyesha mifumo ya makombora ya kuzuia mashambulizi ya ndege iliyowekwa kuzunguka mji wa Mecca, huku Mnara wa Saa ya Saudi, muundo wa kitambo mbele ya Msikiti Mkuu, pia ukionekana kwa nyuma.

Picha nyingine inaonyesha helikopta ikipiga doria juu ya Msikiti huo Mtakatifu na mazingira yake.

Picha hizo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, na watumiaji wa mitandao walijiuliza kwa nini serikali ya Saudia iliweka mifumo ya ulinzi wa anga wakati wa Hija.

Kuna mjadala kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi wakidai kuwa Saudi Arabia iliweka mfumo huu ili kulinda dhidi ya mashambulizi yanayoweza kufanywa na wapiganaji wa Houthi wa Yemen.

Tangu kampeni inayoongozwa na Saudia dhidi ya Houthis kuanza, wapiganaji wa Houthi wamedai mara kwa mara kuwa wamerusha makombora katika miji ya Saudi.

Kwa upande mwingine, Saudi Arabia imewashutumu Wahouthi kwa kuushambulia hapo awali mji wa Makka.

Hata hivyo, Wahouthi wamekanusha tuhuma kwamba walishambulia mji mtakatifu wa Waislamu.

Je, ni kwanini Saudia ilichukua hatua hiyo?

Pia unaweza kusoma

.

Chanzo cha picha, X/@modgovksa

Saudi Arabia iliweka mifumo ya kuzuia makombora ya Marekani ya Patriot karibu na Mecca ili kuwalinda mahujaji, kulingana na vyombo vya habari vya Saudia.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudia, Wizara ya Mambo ya Ndani ilifanya mkutano na waandishi wa habari kabla ya Hajj kujadili usalama na mipango mizuri kwa mahujaji wakati wa Hija.

Kuhusiana na hili, maafisa wakuu wa usalama walitoa maelezo kuhusu hatua zilizochukuliwa ili kuhakikisha usalama wakati wa Hija.

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika na Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Ufalme wa Saudi Arabia, Meja Jenerali Mohamed Al-Bassami, ambaye alizungumza na vyombo vya habari, alisema kuwa Saudi Arabia imejitolea kuwapa mahujaji mazingira salama, ili kufanikisha ibada hiyo muhimu.

Hii ni pamoja na mipangilio ya usalama, amani na utulivu, usimamizi wa umati, trafiki na usimamizi wa dharura.

Lengo lao ni kutoa nyenzo bora zaidi kwa mahujaji wakati wa safari ya kwenda Makka na Madina.

.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Mahujaji Mekka

Ufahamu mfumo wa anga wa Patriot

.

Chanzo cha picha, AFP

Mfumo wa ulinzi wa makombora unaoonekana kwenye picha zilizotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Saudia ni Patriot MIM 104.

Huu ni mfumo wa ulinzi wa makombora na anga. Unatengenezwa na makampuni ya Kimarekani Raytheon na Lockheed Martin.

MIM Patriot 104 ni mfumo wa makombora wa masafa marefu ulioundwa ili kukabiliana na aina mbalimbali za vitisho vya angani ikiwa ni pamoja na meli, makombora ya kusafiri, na makombora ya balestiki.

Unajulikana kwa rada yake ya hali ya juu, ambayo inajumuisha uwezo wa kufuatilia na kuharibu malengo mengi kwa wakati mmoja. Mfumo huu wa makombora ni wa masafa mafupi na una uwezo wa kukatiza na kushambulia mifumo ya kielektroniki.

Mfumo huu wa makombora uliwavutia wataalam wa kijeshi kwa kufanya vyema katika vita vya Iraq na Kuwait mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Majarida mengi ya ulinzi ya kimataifa yamejumuisha makombora haya kati ya mifumo kumi ya kisasa ya ulinzi iliyopo.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla