Mwananchi Communications Limited
Muktasari:
- Coastal ambayo msimu huu imeshuka kiwango tofauti na uliopita, kwa sasa inashika nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa imecheza mechi 28, ikishinda saba, sare 10 na kupoteza 11 na kukusanya pointi 31.
KOCHA wa Coastal Union, Joseph Lazaro ameweka wazi maeneo makubwa mawili ya kiungo na ushambuliaji ambayo kikosi hicho kinatakiwa kuongezewa nguvu kwa ajili ya msimu ujao.
Coastal ambayo msimu huu imeshuka kiwango tofauti na uliopita, kwa sasa inashika nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa imecheza mechi 28, ikishinda saba, sare 10 na kupoteza 11 na kukusanya pointi 31.
Nafasi iliyopo Coastal, inaifanya timu hiyo kupiga hesabu kali kuhakikisha haiangukii kwenye mtego wa kucheza mechi za mtoano kuwania kubaki ligi kuu, hivyo italazimika kushinda mechi mbili za mwisho za nyumbani dhidi ya Fountain Gate na Tabora United.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lazaro alisema msimu huu kikosi hicho kimefunga idadi ndogo ya mabao jambo ambalo limewakwamisha kufanya vizuri tofauti na na msimu uliopita.
Alisema kwa kiwango hicho, klabu hiyo haiwezi kukwepa kufanya usajili wa nguvu ili msimu ujao kuondoa presha inayowakuta hivi sasa.
"Kwa msimu ujao huwezi kubadili timu nzima, lakini yapo maeneo makuu mawili hasa ya mbele ili kuwa na mwisho mzuri wenye matokeo bora.
"Eneo la viungo na washambuliaji linatakiwa kufanyiwa maboresho kwani ukiangalia uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa haupo sawa," alisema kocha huyo na kuongeza.
"Kama Lammeck Lawi ataondoka, itabidi tuongeze mmoja katika eneo la beki wa kati ili kuwa na kikosi kipana zaidi msimu mzima."
Kuhusu mechi mbili zilizobaki, Lazaro alisema: "Mechi zilizosalia tunacheza nyumbani na faida kubwa ni uwanja wa nyumbani, kwa hiyo tunaufahamu vyema, licha ya maandalizi mazuri ila hilo linatupa kujiamini zaidi."
Katika kikosi cha Coastal Union, wanaocheza eneo la kiungo kuna Abdul Hamis, Greyson Gwalala, Charles Semfuko na Lucas Kikoti, huku ushambuliaji wakiwepo Crispin Ngushi, Dennis Modzeka na Roland Junior.
Coastal Union msimu uliopita ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya nne huku ikionyesha kiwango kizuri baada ya kukusanya pointi 43, huku ikiwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Licha ya timu hiyo kufunga mabao 22 ambayo ni machache kulinganisha na ya msimu huu (24), lakini ilishinda mechi nyingi (11), huku ikipata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu na kuishia hatua ya awali.
MECHI ZILIZOSALIA
Juni 18: Coastal Union vs Fountain Gate
Juni 22: Coastal Union vs Tabora United