Mustafa apishana na Manula Azam FC

1 day ago 3

By  Charity James

Reporter

Mwananchi Communications Limited

BAADA ya Azam FC kumalizana na aliyekuwa kipa wa Simba, Aishi Manula mabosi wa klabu hiyo kwa sasa wapo hatua za mwisho kuvunja mkataba wa mwaka mmoja na Mohamed Mustafa.

Mustafa raia wa Sudan, alisajiliwa na Azam kutoka El Merrikh ya Sudan baada ya mkataba wa awali wa mkopo kumalizika ikimsajili kwa mkataba wa miaka miwili hadi mwaka 2026.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Azam, kimeliambia Mwanaspoti kuwa tayari wamefikia makubaliano ya kuvunja mkataba na kipa huyo ili kumpisha Manula ambaye tayari amerejea kikosini kwa mara nyingine na kilichobaki ni kutambulishwa tu.

“Mazungumzo yamefikia hatua nzuri, Mustafa hatakuwa sehemu ya kikosi chetu kwa msimu ujao hilo limefanyika kwa kuzingatia matakwa ya benchi la ufundi kuhusiana na mkataba kila kitu kitaenda sawa,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;

“Ujio wa Manula kikosini ni sehemu ya kuimarisha safu yetu ya ulinzi ambayo kwa namna moja ama nyingine ndio iliyotuangusha msimu huu tukishindwa kufikia malengo tuliyokuwa tumejipangia mwanzo mwa msimu.”

Chanzo hicho kilisema mbali na maboresho yaliyofanywa eneo hilo bado wana mkakati wa kuendelea kufanya usajili maeneo mengine ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusaka mataji msimu ujao.

Mustafa msimu huu amecheza mechi 17, dakika 1530 karuhusu mabao 10 ana clean sheet 10 akisaidiwa na Zuberi Foba, lakini uongozi wa timu hiyo umeona kuna haja ya kusaka kipa mwingine namba moja kikosini.

Read Entire Article