Maisha yameenda kasi sana kwa Yao

1 day ago 2

By  Charles Abel

Mwananchi Communications Limited

YAO Kouassi Attohoula alipokuja kujiunga na kuanza kuitumikia Yanga, mambo yalimwendea vizuri sana hadi akateka hisia za mashabiki wa timu hiyo na wadau wengi wa soka.

Uwezo wake mzuri wa kujilinda lakini kusaidia kupeleka mbele mashambulizi ulifanya karibia wote hapa kijiweni tukubaliane jamaa ni beki wa pembeni wa kisasa kutokana na anavyofanya vizuri katika maboksi mawili muhimu pindi timu yake inapocheza.

Haikushangaza kuona msimu uliopita akiingia katika kikosi bora kwani alitoa mchango mkubwa katika kuilinda timu yake, pia kusaidia mashambulizi.

Hata hivyo, kijiwe kimepata habari ya kushtukiza kuhusu mchezaji huyo ambayo ni kutakiwa kufanyiwa upasuaji wa goti ambalo limekuwa likimsumbua kwa muda mrefu hadi kusababisha asitumike sana msimu huu.

Wasiwasi wa Kijiwe ni matibabu hayo yanaweza kumweka nje ya uwanja, Yao ambayo yanaweza kuishawishi timu yake kutomjumuisha katika usajili wake msimu ujao ili kumpa fursa beki huyo kupona vyema na kurudi uwanjani akiwa fiti kabisa.

Tayari tumeanza kusikia tetesi kuna beki kutoka TP Mazembe, Ibrahima Keita ambaye Yanga inamuwinda kwa ajili ya kuziba nafasi ya nyota huyo kutoka Ivory Coast kwa msimu ujao.

Ni ngumu kuwalaumu Yanga ikiwa itamuacha Yao kwa vile ikimsajili itajikuta inatumia gharama kubwa kuwa naye huku akiwa hatumiki wakati huo nafasi yake kama mchezaji wa kigeni ikiwa haiwasaidii.

Kijiwe kinawashauri wachezaji wetu wazawa kupata somo kupitia Yao Attohoula na kulifanyia kazi ili likija kuwatokea wasiwe kwenye majuto.

Soka ni kazi ya muda mfupi na isiyotabirika. Pale wanapokuwa katika ubora, watumie vizuri nafasi kujijenga kimaisha.

Read Entire Article