Yanga, TFF hakijaeleweka

1 day ago 4

By  Daudi Elibahati

Reporter

Mwananchi Communications Limited

Muktasari:

  • Hivi karibuni kumekuwa na mzozo unaoendelea kuhusiana na taasisi hizo mbili kwa kile kilichoibuliwa na Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe kuweka wazi hawatocheza mechi ya fainali ya FA dhidi ya Singida Black Stars hadi watakapolipwa fedha zao za ubingwa za msimu uliopita.

SAKATA linaloendelea kati ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Yanga kuhusu madai ya fedha za ubingwa wa Kombe la Shirikisho (FA), limechukua sura mpya baada ya kutofikia kwa maelewano.

Hivi karibuni kumekuwa na mzozo unaoendelea kuhusiana na taasisi hizo mbili kwa kile kilichoibuliwa na Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe kuweka wazi hawatocheza mechi ya fainali ya FA dhidi ya Singida Black Stars hadi watakapolipwa fedha zao za ubingwa za msimu uliopita.

Katika taarifa kwa Umma iliyotolewa na Yanga jana Juni 10, 2025, ilieleza TFF imekuwa ikishikilia fedha zote za ubingwa wa michuano hiyo iliyotwaa timu hiyo kwa misimu mitatu, 2021-2022, 2022-2023 na 2023-2024, jambo ambalo ni kinyume na taratibu.

Baada ya hilo, TFF ilitoa taarifa kwa Umma ikiwataka wataalamu wa fedha wa Yanga leo Jumatano saa 4:00 asubuhi kufika makao makuu ya TFF, kujadiliana kwa kina juu ya sakata hilo ili kufikia uamuzi wa mwisho kwani Yanga haidai bali inadaiwa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine akizungumza na waandishi wa habari leo baada ya kutoka katika ofisi za TFF, amesema hawana chochote cha kujadiliana zaidi ya kutaka fedha zao za ubingwa wa FA.

"Wewe umeona wapi hela ya zawadi ikakatwa kwenye madeni? Sisi kwa upande wa Yanga hatutaki kujadiliana jambo lolote kwa sasa zaidi ya kudai haki yetu ya msingi ambayo ni fedha za ubingwa," amesema.

Kwa upande wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo, amesema Yanga hawakutaka kuzungumza chochote katika kikao walichoitiwa, zaidi ya kuleta barua kisha kuondoka.

"Baada ya Yanga kufika hawakutaka kuzungumza chochote zaidi ya kuleta barua ya kimaandishi kama waliyoitoa katika taarifa zao kwa Umma," amesema Ndimbo.

Ndimbo aliongeza kuwa, hata Mtine alipotakiwa kuzungumza na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao kuhusiana na sakata hilo hawakuwa tayari, zaidi ya kuwasilisha barua pekee.

"Kidao alitaka kuzungumza nao lakini baada ya kuingia waliweka barua yao na kuondoka, hawakutaka kuzungumza jambo lolote," amesema.

Akizungumzia bingwa wa Kombe la FA anachukua kiasi gani, Ndimbo amesema hakuna sehemu yoyote iliyotangazwa kiasi cha fedha kuongezeka kama Yanga inavyodai.

"Wakati CRDB wanaingia makubaliano na TFF, kila kitu kilikuwa wazi kwa sababu ilikuwa inajulikana fedha zile ni za uendeshaji na sisi ndio ambao tunapanga tuzitumie kwa namna gani, hivyo hakuna sehemu tuliyotangaza kama kiasi hicho kimeongezeka," amesema.

Kwa mujibu wa Yanga, katika misimu hiyo mitatu ilipaswa kupewa kiasi cha Sh300 milioni kwa mchanganuo wa 2021-2022 (Sh50 milioni), 2022-2023 (Sh50 milioni) na 2023-2024 (Sh200 milioni).

Read Entire Article