Muktasari:
Mashindano hayo yameanza leo yanatarajia kutamatika kesho, Jumapili lengo likiwa ni kukuza na kuendeleza vipaji vya waogeleaji.
WAOGELEAJI 295 wamejitokeza kushiriki mashindano ya kuogelea ya ubingwa wa Taifa kwa vijana wadogo chini ya miaka 12 kutoka Bara na Zanzibar.
Mashindano hayo yameanza leo yanatarajia kutamatika kesho, Jumapili lengo likiwa ni kukuza na kuendeleza vipaji vya waogeleaji.
Akizungumzia mashindano hayo, Mwenyekiti wa Chama Cha Kuogelea Tanzania (TSA), David Mwasyoge amesema ushiriki huo unaonyesha ukuaji wa mchezo huo hapa nchini.
Amesema lengo la mashindano hayo ni kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana hao kwa ajili ya manufaa ya timu za Taifa za mchezo huo kwa miaka ya baadaye.
“Mashindano haya ni mwisho wa kumaliza msimu ambao kwetu unaisha Julai, na tunaanza msimu na huwa tufanya kila mwaka na hii historia ya ushiriki wa namba kubwa haijawahi kutokea katika historia ya kuogelea," amesema Mwasyoge na kuongeza:
"Ukiona idadi kubwa ya watoto inakua na wanachipukia na wanashindana wenyewee hii inawajengea na kujipima uwezo wao wa kile walichofundishwa na kuja kukionyesha."
Amesema mashindano hayo yamekuwa na mchango mkubwa kwa vijana kutambua vipaji vyao na yanawajenga kiakili, kifikra na yanawapa uzoefu wa kushindana na yanaleta maendeleo.