Tanzania yaifumua Sudan Kusini Cecafa

1 day ago 2

By  Nevumba Abubakar

Reporter

Mwananchi Communications Limited


BAADA ya Burundi kuichapa Uganda kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza wa mashindano ya Cecafa ya Wanawake, Tanzania ikawachapa Sudan Kusini mabao 4-0.

Tanzania na Burundi zimeanza kwa ushindi katika siku ya kwanza ya mashindano ya Cecafa 2025 yanayofanyika katika Uwanja wa Azam Complex Dar es Salaam.

Tanzania inayojipanga kwa ajili ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON), iliicharaza Sudan Kusini mabao 4-0 yaliyofungwa na Diana Lucas katika dakika ya tisa, Opah Clement aliyefunga mawili dakika ya 34 na 62 huku  Clara Luvanga akifunga moja. 

Kocha wa Tanzania, Bakari Shime amesema sio tu Clara aliyepoteza nafasi nyingi, lakini karibu timu nzima kwani walikuwa wanafika eneo la timu pinzani kwa ufasaha.

"Ni kweli tuliunda nafasi nyingi za kufunga sio kwa Clara pekee, lakini kwa wachezaji wengi. Pia tulicheza kwa kasi kubwa. Tutazidi kujiboresha kila mechi,” amesema.

"Haijalishi unacheza na timu gani kikubwa ni 'game plan' yako ikoje. Tumecheza vizuri, lakini tutaenda kufanyia kazi tatizo la kupoteza mipira."

Licha ya Uganda kutawala mechi kipindi cha kwanza na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga, Burundi iliibuka na ushindi baada ya Esperance Habonimana kufunga bao pekee dakika ya 75 kwa mpira wa adhabu ndogo na Kipa wa Uganda alikosea kuupangua mpira huo mrefu ulioingia wavuni.

Baada ya mechi hizo, Tanzania inaongoza kundi kwa pointi 3 na tofauti ya mabao manne, ikifuatiwa na Burundi yenye pointi 3 lakini kwa bao moja. Mashindano yataendelea kesho Jumapili ambapo Burundi itavaana na Kenya, huku Sudan Kusini ikikabiliana na Uganda.

Read Entire Article