MSHAMBULIAJI wa Wydad Casablanca ya Morocco, Mtanzania Seleman Mwalimu 'Gomez' ameanza kufanya vizuri baada ya kuhusika kwenye mabao manne kati ya saba ya timu hiyo kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya CS Saint-Laurent kutoka Montreal, Canada.
Katika mechi hiyo iliyopigwa juzi nchini Marekani, Gomez alifunga bao moja na kuasisti mara tatu wakati kikosi hicho kiliposhinda kwa mabao 7-0 ikiwa ni maandalizi ya timu hiyo kushiriki michuano ya Kombe la Dunia la Klabu inayoanza leo nchini Marekani hadi Julai 13, 2025.
Nyota huyo aliyejiunga na Wydad katika dirisha dogo la Januari, mwaka huu akitokea Fountain Gate aliyokuwa anaichezea kwa mkopo kutoka Singida Black Stars, alishirikiana kwenye mabao na aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz KI.
Mabao ya Wydad yalifungwa na Gomez aliyepokea pasi ya Aziz KI, kisha bao la Stephane akapewa asisti na Gomez, huku mengine yakifungwa na Samuel Obeng aliyefunga hat-trick wakati Mohamed Rayhi na Zouhair El Moutaraji wakifunga mojamoja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gomez alisema ni jambo nzuri kwake kufunga bao la kwanza akiwa na kikosi hicho, ingawa bado ana kazi kubwa ya kufanya ili kuendelea kuaminiwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kutokana na ushindani uliopo.
"Ni hatua nzuri kwangu kufunga bao la kwanza nikiwa Wydad tangu nimefika hapa. Haijalishi ni mechi ya kirafiki isipokuwa ninachojivunia ni kufanya vizuri. Nitaendelea pia kupambana kadri ambavyo nitaendelea kupewa nafasi," alisema.
Mchezaji huyo alisema kujumuishwa katika kikosi cha wachezaji watakaoshiriki michuano ya Kombe la Dunia la Klabu, ni heshima kwake kwani inamuongezea ari ya kuamini kwamba hakuna kinachoshindikana ikiwa utapigania malengo yake.
Wydad iko kundi G la michuano hiyo na itafungua pazia Juni 18 kwa kucheza na Manchester City ya England, huku Juni 22 ikipambana na Juventus ya Italia kisha kuhitimisha Juni 26 kwa kupambana na Al Ain FC ya Falme za Kiarabu.
Gomez ndiye wa kwanza kujiunga na Wydad baada ya kuonyesha kiwango bora akiwa na Fountain Gate ambapo hadi anaondoka nchini alikuwa ameifungia mabao sita katika Ligi Kuu Bara.
Kwa upande wa Aziz KI, amejiunga na timu hiyo baada ya kuichezea Yanga misimu mitatu tangu alipojiunga nayo Julai 15, 2022 akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast ambapo ametwaa mataji mbalimbali ikiwemo mawili ya Ligi Kuu Bara.