Chanzo cha picha, Getty Images
Dakika 13 zilizopita
Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusitisha mara moja vitendo vya kutoweka kwa wapinzani wa kisiasa, watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari.
"Kuminya uhuru wa vyombo vya habari na kutisha waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu, ni jambo lisilokubalika.
''Tunasikitishwa na ripoti za ukandamizaji kuelekea uchaguzi mkuu wa Tanzania mwezi Oktoba," wataalamu hao walisema.
Ripoti hiyo inafuatia kutekwa kwa watetezi wawili wa haki za binadamu na waandishi wa habari, Boniface Mwangi kutoka Kenya na Agather Atuhaire kutoka Uganda, jijini Dar es Salaam tarehe 19 Mei 2025.
Wakati waangalizi wengine wakikataliwa kuingia, Mwangi na Atuhaire walikuja Tanzania kufuatilia kesi ya kiongozi wa upinzani wa kisiasa Tindu Lissu, ambaye alishtakiwa kwa uhaini na kuchapisha habari za uongo.
Walikamatwa na maafisa wa polisi na hatima yao na taarifa kuhusu waliko kufichwa.
"Zaidi ya kesi 200 za kutoweka zimerekodiwa nchini Tanzania tangu 2019," . "Kukamatwa kiholela, kuteswa na kutoweka kwa Mwangi na Atuhaire hivi karibuni kunaonekana kuwa mbinu ya wazi ya kukandamiza upinzani na kukwepa sheria zinazofaa."
"Tunaziomba mamlaka za Tanzania kuacha mara moja kuficha taarifa za waliokamatwa, kwani hii ni sawa na kutoweka. Lazima pia zichunguze na kuwawajibisha wahalifu," wataalamu hao walisema.
"Serikali lazima itoe haki na fidia kwa waathiriwa. Hii ni pamoja na kupata huduma za matibabu, kisaikolojia na kisheria zinazozingatia jinsia kwa waathirika wa mateso na unyanyasaji wa kijinsia."
'Kama waliteswa waje washtaki' Polisi Tanzania wawaambia wanaharakati
Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam Jumanne Muliro aliiambia BBC kuwa wanaharakati kutoka Kenya na Uganda Boniface Mwangi na Agatha Atuhaire kama waliteswa basi waende kushtaki katika mamlaka husika.
Muliro aliongeza pia madai yao ni ya kiuanaharakati na ni maoni yao.
"Kama wangekuwa hapa, ningewashirikisha, ningewauliza wanasema nini, wanamaanisha nini... Katika sheria, mambo hayo yanaitwa ushahidi wa tetesi au tetesi," Jumanne Muliro aliiambia BBC. Alisema wanapaswa kutoa taarifa kwa mamlaka kwa ajili ya uchunguzi.
"Tusiwe shamba la bibi"
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alitoa onyo kali kwa wanaharakati kutoka nchi jirani kuacha kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania, akisisitiza kuwa taifa hilo haliwezi kuwa "shamba la bibi" ambapo kila mtu anaingia na kufanya apendavyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa toleo jipya la Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (Toleo la 2024), Rais Samia alisema kuna mwenendo unaoibuka wa baadhi ya wanaharakati kuvuka mipaka na kuingilia masuala ya ndani ya nchi, hali ambayo haiwezi kuvumiliwa.
"Tusuiwe shamba la bibi kwamba kila mtu anaweza kuja na kusema anachokitaka… Tumeanza kuona mtitiriko au mwenendo wa wanaharakati ndani ya region (kanda) yetu hii, kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku," alisema Rais Samia.
Kauli hiyo aliitoa siku moja baada ya wakili mashuhuri wa Kenya na aliyewahi kuwa Waziri wa Sheria, Martha Karua, pamoja na Jaji Mkuu wa zamani Willy Mutunga na wanaharakati wengine wawili, kuzuiwa kuingia nchini Tanzania.
Walikuwa wamewasili kushuhudia kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa upinzani Tanzania, Tundu Lissu, ambayo imeendelea leo katika Mahakama ya Kisutu.
Kauli ya Rais Samia imeonekana kutoa mwelekeo wa msimamo wa serikali juu ya suala hilo.
"Sasa kama kwao wameshadhibitiwa wasije kutuharibia huku. Tusitoe nafasi, walishaharibu kwao, walishavuruga kwao, nchi iliyobaki haijaharibika watu wako na usalama na amani na utulivu ni hapa kwetu, aliongeza Rais Samia.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wasimamizi wa sera za nje, wanapaswa kuhakikisha kuwa hakuna "watovu wa adabu" kutoka mataifa mengine wanaovuka mipaka ya Tanzania na kuingilia masuala ya kitaifa.
"Niombe sana vyombo vya ulinzi na usalama na ninyi wasimamizi wa sera zetu za nje, msitoe nafasi kwa watovu wa adabu wa nchi nyingine kuja kuvuka hapa kwetu," alisisitiza.
Kesi ya Tundu Lissu inaendelea huku mashinikizo kutoka ndani na nje ya nchi yakiongezeka, yakihusisha madai ya ukandamizaji wa haki za kiraia na kisiasa, jambo ambalo Serikali ya Tanzania inakanusha.