Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Rob Stevens
- Nafasi, BBC Michezo Afrika
14 Juni 2025, 15:14 EAT
Imeboreshwa Dakika 15 zilizopita
Hatua ya Shirikisho la Soka duniani(FIFA) kuongeza idadi ya timu zitakazoshiriki katika michuano ya Kombe la dunia la vilabu inatoa fursa kwa vilabu vinne vya Afrika kuelekea nchini Marekani kwa mashindano hayo ya kwanza yatakayojumuisha timu 32.
Ahly ya Misri, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Wydad Casablanca ya Morocco na Esperance ya Tunisia ndizo timu za Afrika ziitakazochuana na klabu kubwa za Ulaya na washindani wengine kutoka kote duniani.
Hakuna klabu yoyote ya Afrika ambayo imewahi kushinda Kombe la dunia la vilabu, na ni klabu mbili pekee zilizowahi kufika fainali ya michuano hiyo katika mashindao 20 yaliyopita.
Lakini sasa kuna faida ya kushiriki- zawadi kwa washindi na ushiriki zikipanda mpaka kufikia jumla ya dola $1bn huku dola $475m zikitengwa kwa ajili ya namna timu zitakavyoonyesha viwango vya ubora.
Hata ingawa mashandano hayo yanaongeza idaid ya mechi zaidi katika kalenda ya soka ambayo tayariri ina inalalamikiwa kuwa na mechi nyingi, kocha wa klabu ya Esperance Maher Kanzari anasema hii ni "fahari kubwa" kwa wachezaji watakaoshiriki.
Mauzo ya tiketi yameripotiwa kuwa chini huku michuano hiyo ikitarajiwa kung'oa nanga Jumapili hii Juni 15. Hata hivyo shabiki mmoja wa Sundowns anaunga mkono mfumo mpya ulioanzishwa na Gianni Infantimno, rais wa shirikisho la soka duniani, ambao utatoa nafasi kwa michuano hiyo kuandaliwa kila baada ya miaka minne.
"Huwezi kuishi maisha bila kutarajia mabadiliko," Thabo Mothabela aliambia BBC Michezo Afrika.
"Lazima ubadilike na kufanya mambo mapya. Hivyo ndivyo tunavyokua na kuimarika."
Kuiwakilisha Afrika kwa fahari
Chanzo cha picha, Getty Images
Kanzari ametoa wito kwa kikosi chake "kupambana vilivyo" watakapokutana na Flamengo, Chelsea na Los Angeles FC katika Kundi D.
"Kuiwakilisha Esperance, Tunisia na bara la Afrika ni wajibu mkubwa," aliiambia BBC.
"Tunajua mashabiki wetu watakuwa wanatufuatilia, na sisi tutafanya kila liwezekanalo kuonyesha kiwango ambacho kinastahiki cha soka la Afrika."
Mabingwa hao mara nne wa Afrika watashiriki kwa mara ya kwanza tangu 2019.
"Kushiriki mchuano wa kiwango cha Kombe la Dunia la Klabu ni ndoto ya kila mchezaji na kocha," Kanzari aliongeza.
Al Ahly, kwa upande wake, itamenyana na Inter Miami ya Lionel Messi katika mechi ya ufunguzi Jumapili kabla ya kukutana na Palmeiras ya Brazil na Porto.
Miamba hao wa Cairo walimteua Jose Riveiro muda mfupi baada ya kushinda taji lao la 45 la Misri, na wameimarika kwa kuwasajili washambuliaji wa Misri Trezeguet na Zizo.
Wydad, ambao hawatashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao baada ya kushika nafasi ya tatu kwenye ligi ya Morocco, watafungua kampeni yao ya Kundi G dhidi ya Manchester City kabla ya kumenyana na Juventus na klabu ya Al Ain ya Milki za Kiarabu UAE.
Utofauti mkubwa wa mgao wa fedha
Chanzo cha picha, Getty Images
Klabu zote nne za Afrika zinazoshiriki michuano hiyo zitapokea ada ya kushiriki ya $9.55m - sawa na wawakilishi kutoka Asia na Kaskazini na Amerika ya Kati na eneo la Caribbea.
Fedha hizo ni ni kama tone la maji ukilinganisha na zawadi ya dola milioni nne zilizokabidhiwa kwa washindi wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu Pyramids.
Hata hivyo, vilabu vya Afrika ni miongoni mwa vilabu vinavyopata mgao mdogo zaidi katika Kombe la Dunia la Vilabu. Wawakilishi sita kutoka Amerika Kusini watapokea kila mmoja dola milioni 15.21, huku vilabu 12 vya Ulaya vikilipwa kati ya dola milioni 12.81 hadi kiasi cha kushangaza cha dola milioni 38.19.
Ushindi wa hatua ya makundi una thamani ya $2m na sare $1m,na mabingwa wa watakaotawazwa East Rutherford tarehe 13 Julai wataweka mfukoni dola $40m.
Swali linaloibuka hapa ni iwapo fedha hizi nyingi zitakazotolewa zitaathiri mashindano ya vilabu barani Afrika - hasa ikizingatiwa kwamba vilabu vya Al Ahly, Esperance, Wydad na Sundowns vimeshinda mataji ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kati ya mwaka 2016 na 2024.
Fifa, hata hivyo inasema kwamba mapato yote yatakayotokana na Kombe la Dunia la Vilabu yatagawanywa kwa vilabu kote duniani, na ina lengo la kufikia $250m katika mpango wake wa uwekezaji wa kuimarisha mshikamano.
"Ni jukwaa ambalo tunahitaji kuonyesha uwezo wetu kama vilabu vya soka vya Afrika," Hersi Said, mwenyekiti wa Umoja wa Vilabu vya Afrika, aliiambia BBC.
"Tunahitaji kushinikiza kupata idadi zaidi ya washiriki katika mashindano yanayofuata."
Je, ni wakati wa Afrika kung'aa?
Chanzo cha picha, Getty Images
Baadhi ya watu wanamatumaini kuwa timu za Kiafrika zinazocheza Kombe la Dunia la Vilabu zinaweza kurudisha umakini kwenye mashindano ya vilabu ya bara hili, hata kama Ligi ya Mabingwa Afrika haina umaarufu na mapato makubwa ikilinganishwa na michuano kama hiyo barani Ulaya.
Ligi ya Klabu bingwa Afrika ilizinduliwa kwa kishindo na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) mwaka 2023 nchini Tanzania.
Klabu ya Sundowns yenye makao yake njini Pretoria, inayomilikiwa na bilionea na rais wa Caf, Patrice Motsepe, imejiimarisha kama klabu kubwa nchini Afrika Kusini, ikinyakua mataji manane ya ligi.
Hata hivyo shabiki mmoja wa timu pinzani anafikiri kuwa uwepo wa Sundowns katika Kundi F, ambapo watamenyana na Ulsan HD, Borussia Dortmund na Fluminense, kunaweza kusaidia kukuza na kulitangaza soka la Afrika.
"Katika jukwaa la kimataifa, sidhani Sundowns inajulikana kama vilabu vingine," shabiki wa Kaizer Chiefs Wayne Magwaza alisema.
"Katika klabu zote za Afrika zinazoshiki, ni Ahly ambayo ni maarufu zaidi.
"Endapo Sundowns itafanya vyema basi itabadili mtazamo wa soka la Afrika Kusini na pengine kuleta umakini kwa ligi ya nchi yetu (PSL.)"
Wasiwasi wa uchovu
Ratiba ya michuano ya kombe la dunia la vilabu tayari ishavuruga kalenda ya soka duniani huku michuano ya kombe la soka la mataifa ya bara la Afrika ikilazimika kuahirishwa kutoka mwezi Juni -Julai hadi Disemba.
Muungano wa wanasoka wa kulipwa duniani wa Fifpro na uongozi wa ligi kuu za ulaya waliwasilisha malalamishi ya kisheria mwaka jana kuhusu kile wanachodai FIFA inatumia mamlaka vibaya lakini mashindano hayo yataendelea bila kujali lolote.
AC Milan ya Italia anayoicheza Samuel Chukwueze haitashiriki michuano hiyo ila, winga huyo wa Nigeria anadhani kuwa mechi hizo ni nyingi mno kwa wachezaji.
'Huo ndio muda pekee wa wachezaji kupumzika na ndio wakati ambao wameiratibu michuano hiyo'Alisema mchezaji huyo mwenye miaka 26.
'Ni ngumu sana kucheza mechi nyingi.Unachoka na kudhoofika miguu na akili na mwishoe unakosa hamu ya kucheza'
'Lakini ni mashindano na kwa hiyo haina budi, lazima ucheze'
Kwa mashabiki ,fursa ya mapambano ya kuwania taji inasisimuwa kama kawaida
'Kushiriki michuano ya kombe la dunia la klabu si jambo rahisi lakini tuna matumaini makubwa 'shabiki wa Sundowns anasema
Jinsi wanavyocheza , wanatupa ujasiri. Tunaamini watafika hatua ya nusu fainali
Uwezekano wa timu ya Afrika kunyakuwa kombe hili ni finyu sana, lakini FIFA inalenga mashindano hayo kuanzisha zama mpya za soka la kimataifa.
Ingawaje, haijabainika wazi iwapo mabilioni ya fedha na zawadi za kifahari zitakazotolewa Marekani zitaipa faida pia timu za Afrika, uwepo wa michuano ni nafasi nyingine ya Afrika kuonyesha uwezo kung'ara, na kushangaza dunia.
Maelezo ya ziada yamechanngiwa na Morad Dakhil na Eshlin Vedan.