Chanzo cha picha, Getty Images
Dakika 6 zilizopita
Kabla ya mapinduzi ya kiislamu ya Iran ya mwaka 1979, Israel na Iran zilikuwa na uhusiano mzuri na wa kimkakati. Iran chini ya Mohammad Reza Pahlavi, ilikuwa mshirika muhimu wa Marekani na Israel katika kudumisha utulivu Mashariki ya Kati.
Hata hivyo, mapinduzi ya kiislamu yaliyomleta Ayatollah Ruhollah Khomeini madarakani yalibadilisha kabisa sera ya nje ya Iran.
Serikali mpya ilipitisha itikadi ya kupinga Uzayuni na kuitambua Israel kama "taifa haramu la Kizayuni" lililochipua katika ardhi ya Kiislamu. Kuanzia hapo, Israel ilianza kuonekana kama adui namba moja, na mzozo wa Palestina ukawa kiini cha sera ya kigeni ya Iran.
Mashambulizi ya Israel kwenda Irani wiki hii imeongeza mvutano kati ya mataifa hayo, ukifikia kilele chake, huku msingi mkuu wa uhasama huu ukiwa ni mpango wa nyuklia wa Iran. Irani inasema "Israel itajuta ilichokifanya".
Licha ya Iran kusisitiza kuwa mpango wake ni kwa malengo ya amani na nishati, Israel inauona kama tishio la moja kwa moja na la kimaisha, ikichukua hatua kali kuhakikisha Tehran haimiliki silaha za nyuklia.
Swali la msingi linabaki: Ni kwanini Israel ina msimamo mkali kiasi hiki dhidi ya uwezekano wa Iran kuwa na uwezo wa nyuklia wa kijeshi?
1. Hatari kwa uhai wa Israel
Chanzo cha picha, Getty Images
Iran ina mpango wake wa nyuklia inaosema kwamba ni kwa madhumuni ya amani. Irani inasisitiza kuwa haitafuti kutengeneza silaha za nyuklia, lakini nchi nyingi na shirika la kimataifa la kudhibiti nyuklia, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), haziamini. Hata Israel pia haiamini kuhusu mpango huo.
Israel inauona mpango wa nyuklia wa Iran kama tishio la moja kwa moja kwa uhai wake. Kauli za viongozi wa Iran, hasa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979, zimekuwa zikiihimiza kuharibiwa kwa Israel.
Licha ya kauli hizi mara nyingi kutafsiriwa kwa njia tofauti, huko Israel zinachukuliwa kwa uzito mkubwa, hasa kutokana na historia ya Wayahudi ya mauaji ya halaiki.
Hofu ni kwamba, ikiwa Iran itamiliki silaha za nyuklia, itakuwa na uwezo wa kutekeleza vitisho hivyo, na hivyo kuhatarisha kuwepo kwa taifa la Israel. Kwa Israel, suala hili si la kisiasa tu, bali ni la kimaisha.
2. Uhasama wa kidini na kiitikadi
Tofauti za kiitikadi na kidini zinachochea uhasama huu. Serikali ya Iran, inayofuata Uislamu wa Kishia, imepita kauli za mara kwa mara zenye uhasama mkubwa dhidi ya Israel, ikiiita "taifa la Kizayuni haramu."
Viongozi wa Iran mara nyingi wameahidi kuifuta Israel kutoka ramani ya dunia. Ingawa baadhi wanachukulia hizi kama kauli za kisiasa tu, huko Israel, kauli hizi zinachukuliwa kama jambo linalodhihirisha nia halisi ya kuangamiza.
Jambo hili linajenga mazingira ya kutokuaminiana kabisa na kuimarisha imani ya Israel kwamba mpango wa nyuklia wa Iran una lengo la kijeshi dhidi yake.
3. Ushawishi wa kikanda
Chanzo cha picha, Getty Images
Iran imejenga mtandao mpana wa vikundi shirikishi katika Mashariki ya Kati, vikiwemo Hezbollah nchini Lebanon, Hamas na Islamic Jihad huko Gaza, na Houthis nchini Yemen.
Vikundi hivi, vinavyopokea msaada wa kijeshi na kifedha kutoka Iran, vinapingana vikali na Israel na vimehusika katika mashambulizi mbalimbali dhidi yake.
Israel inaona vikundi hivi kama mikono ya Iran inayotumika kuhatarisha usalama wake kutoka pande mbalimbali.
Israel inapinga vikali ushawishi huu, ikiona vikundi hivi kama vitisho vya moja kwa moja kwenye mipaka yake. Hali hii imesababisha Israel kufanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya maeneo yanayohusishwa na Iran na Hezbollah nchini Syria na Lebanon.
Uwezekano wa Iran kuwa na silaha za nyuklia, wakati ikiendelea kuunga mkono vikundi hivi, unazidisha hofu ya Israel ya kutokea kwa mzozo mpana zaidi na hatari zaidi.
4. Hofu ya kuenea kwa silaha za nyuklia
Israel ina wasiwasi mkubwa kwamba, ikiwa Iran itamiliki silaha za nyuklia, itasababisha mataifa mengine katika eneo hilo, kama vile Saudi Arabia na Misri, pia kujaribu kutengeneza silaha zao za nyuklia ili kusawazisha nguvu.
Hali hii inaweza kupelekea mbio za silaha za nyuklia katika eneo lenye utulivu mdogo, na kuongeza hatari ya kutokea kwa vita vya nyuklia.
Israel inafuata sera isiyo rasmi ya "ukweli wa nyuklia," ambapo haithibitishi wala kukanusha kuwepo kwa silaha zake za nyuklia, lakini inasisitiza kuwa haitakubali taifa lingine lolote katika eneo hilo kumiliki silaha hizo.
5. Ukosefu wa imani na ukaguzi wa mpango wa Nyuklia
Chanzo cha picha, Getty Images
Licha ya makubaliano ya nyuklia ya 2015 (JCPOA) ambayo yalilenga kupunguza mpango wa nyuklia wa Iran kwa kubadilishana na kulegeza vikwazo, Israel iliendelea kutoamini nia halisi ya Iran.
Kujiondoa kwa Marekani kutoka makubaliano hayo kulichochea Iran kuanzisha tena shughuli zake za kurutubisha urani, na kurudisha kiwango cha hofu.
Ripoti za Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) zimeonesha changamoto katika ukaguzi wa maeneo fulani ya nyuklia ya Iran, na hivyo kuongeza shaka ya Israel kuhusu uwazi wa mpango huo. Kwa Israel, udhibiti kamili na ukaguzi usiokuwa na vikwazo ni muhimu.
Kwa ujumla, msingi wa msimamo wa Israel dhidi ya Iran kuwa na silaha za nyuklia unatokana na hofu ya kuwepo, uhasama wa kiitikadi na kauli za vitisho, ushawishi wa Iran kupitia vikundi shirikishi, hofu ya kuenea kwa silaha za nyuklia katika eneo tete, na ukosefu wa imani katika nia halisi za mpango wa nyuklia wa Iran.
Kwa Israel, hili si suala la kawaida la usalama, bali ni la kuwepo kwake kama taifa. Ndio maana Israel imekuwa ikitumia kila njia, kuanzia diplomasia hadi operesheni za kijasusi na mashambulizi ya kijeshi, kuzuia kile inachokiona kama tishio kubwa zaidi la karne hii.