Chanzo cha picha, Getty Images
Dakika 10 zilizopita
Alhamisi ya Juni 12, mjadala mkubwa wa kisiasa na kiuchumi katika nchi za Afrika Mashariki ulimetawaliwa na matukio muhimu ya bajeti.
Mawaziri wa Fedha kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, na Rwanda wamewasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya nchi zao yaliyopangwa kwa mwaka ujao wa fedha, wakiangazia vipaumbele vya kipekee vya kila taifa katika harakati zao za kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Huku kila nchi ikijaribu kuweka sawa matarajio ya maendeleo na uhalisia wa changamoto za kifedha, bajeti hizi zinatoa taswira halisi ya mikakati yao ya kujitegemea na ukuaji.
Tanzania: Elimu, Usalama vyapewa kipaumbele
Chanzo cha picha, Bunge
Kwa upande wa Tanzania, serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya Shilingi Trilioni 56.49 (takriban Dola Bilioni 21.73) katika mwaka wa fedha 2025/26. Bajeti hii imepangwa kufadhiliwa na mapato ya ndani ya Shilingi Trilioni 40.47 (takriban Dola Bilioni 15.56), huku kodi zikichangia Shilingi Trilioni 32.31 (takriban Dola Bilioni 12.43), mapato yasiyo ya kodi yakitarajiwa kuwa Shilingi Trilioni 6.48 (takriban Dola Bilioni 2.49), na mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yakiwa Shilingi Trilioni 1.68 (takriban Dola Bilioni 0.65).
Sekta tatu zilizopewa kipaumbele zaidi kama picha juu inavyoonyesha:
Elimu: Imetengewa Shilingi Bilioni 7,394 (takriban Dola Bilioni 2.84), ongezeko kutoka Shilingi Bilioni 6,369 (takriban Dola Bilioni 2.45) za mwaka wa fedha uliopita, ikisisitiza umuhimu wa sekta hii katika maendeleo ya nchi.
Ujenzi, Usafirishaji na Mawasiliano: Imepata Shilingi Bilioni 5,524.2 (takriban Dola Bilioni 2.12).
Ulinzi, Utawala wa Sheria na Usalama: Imepangiwa Shilingi Bilioni 5,493.2 (takriban Dola Bilioni 2.11), ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 6,398.1 (takriban Dola Bilioni 2.46) za mwaka uliopita.
Kipekee, matumizi ya maendeleo yametengewa asilimia 7.2 ya bajeti yote, ikiwa ni Shilingi Trilioni 17.49 (takriban Dola Bilioni 6.73), ambapo fedha za ndani zitachangia Shilingi Trilioni 12.12 (takriban Dola Bilioni 4.66). Kiasi hiki ni ongezeko kutoka Shilingi Bilioni 15,354 (takriban Dola Milioni 5.90) za mwaka uliopita.
Ikumbukwe kuwa matumizi ya maendeleo yalikuwa asilimia 7.8% mwaka 2020/2021, 9.2% mwaka 2021/2022, 7.8% mwaka 2022/2023, na 7.4% mwaka 2023/2024, ikionesha mwenendo unaotofautiana.Kuhusu ugawaji wa bajeti kwa deni la taifa, kiasi cha Shilingi Bilioni 14,209 (takriban Dola Bilioni 5.46) kimetengwa kwa ajili ya kuhudumia deni hilo. Mihimili ya Utawala, Usimamizi wa Mapato na Matumizi, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imetengewa jumla ya Shilingi Bilioni 10,308.3 (takriban Dola Bilioni 3.96), kutoka Shilingi Bilioni 7,981.7 (takriban Dola Bilioni 3.07) mwaka uliopita.
Kenya: Bajeti Kubwa na Mwelekeo Kwenye Ulinzi
Chanzo cha picha, star
Nchini Kenya, Waziri wa Fedha, John Mbadi, ameweka wazi bajeti kubwa zaidi katika ukanda huu, inayofikia takriban Shilingi Trilioni 4.29 za Kenya (Dola Bilioni 33.03). Bajeti hii imejikita pakubwa katika kuongeza mapato ya serikali. Jambo lililowashangaza wengi ni hatua ya Bunge la Kenya kupanga upya bajeti hiyo, ambapo sekta ya kijeshi imeibuka mshindi mkubwa, ikipokea nyongeza ya Dola Milioni 100.1. Hata hivyo, uamuzi huu umekuja na gharama, kwani sekta muhimu kama usimamizi wa fedha za umma, elimu, na michezo zimekumbana na kupunguzwa pakubwa kwa bajeti zao, ikionesha mwelekeo mpya wa vipaumbele vya Nairobi.
Uganda: Mafuta na Gesi Zapewa Kipaumbele Kikuu Kukwamua Uchumi
Nchini Uganda, Waziri wa Fedha Matia Kasaija amewasilisha bajeti yenye matumizi ya takriban Shilingi Trilioni 72.3 za Uganda (Dola Bilioni 20), ikilenga kukuza Pato la Taifa (GDP) kwa Shilingi Trilioni 27.3 za Uganda (Dola Bilioni 7.55). Mwelekeo mkuu wa bajeti hii ni kwenye shughuli za mafuta na gesi, pamoja na miradi mikubwa ya miundombinu kama vile matengenezo na ujenzi wa barabara, madaraja, na reli. Huku uchumi wa Uganda ukipona kutokana na mishtuko ya kimataifa na ya ndani, serikali inaamini kuwa uwekezaji huu utachochea ukuaji wa kasi, ikionesha uhakika wa Kampala katika sekta ya nishati na miundombinu kama vichocheo vikuu vya maendeleo.
Rwanda: Kukuza Uchumi Kupitia Miundombinu Mipya
Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa upande wa Rwanda, Waziri wa Fedha, Yusuf Murangwa, amewasilisha bajeti yenye lengo la kuongeza matumizi kwa asilimia 21, kufikia Faranga Trilioni 7 za Rwanda (Dola Bilioni 4.9). Kipaumbele kikuu cha Kigali kinabaki kuwa ujenzi wa miundombinu mikubwa, hususan uwanja mpya wa ndege huko Bugesera. Sambamba na hilo, sekta za kilimo, elimu, huduma za afya, makazi, na kuboresha upatikanaji wa umeme zimepewa kipaumbele, zikisisitiza dhamira ya Rwanda ya kuendelea kukuza uchumi wake kupitia uwekezaji wa kimkakati na wa muda mrefu.
Bajeti hizi za Afrika Mashariki, ingawa zimetofautiana kwa ukubwa na vipaumbele, zote zinaakisi azma ya pamoja ya mataifa haya kuelekea ukuaji wa kiuchumi na maendeleo ya kijamii, zikijaribu kutembea kwenye "kamba nyembamba ya kifedha" katika mazingira ya kiuchumi yenye changamoto.