Chanzo cha picha, PA Media
Dakika 7 zilizopita
Mwanamume Uingereza ambaye ndiye mtu pekee aliyenusurika katika ajali ya ndege ya Air India Alhamisi anasema alifanikiwa kutoka kwenye mabaki hayo kupitia sehemu iliyokuwa wazi kwenye ndege hiyo.
"Nilifanikiwa kujifungua mkanda, nikatumia mguu wangu kusukuma kupitia eneo la wazi, na kutambaa nje," Vishwashkumar Ramesh aliviambia vyombo vya habari vya serikali ya India, DD News.
Bw Ramesh, mwenye umri wa miaka 40, alikuwa katika kiti nambari 11A kwenye ndege ya Boeing 787 iliyokuwa ikielekea London ilipoanguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege wa Ahmedabad, magharibi mwa India siku ya Alhamisi.
Air India ilisema abiria wengine wote na pamoja na wafanyikazi walifariki - ikiwa ni pamoja na raia 169 wa India na raia 52 wa Uingereza. Zaidi ya miili 200 imepatikana kufikia sasa, ingawa haijulikani ni abiria wangapi waliokuwa ardhini.
Akizungumza kutoka hospitalini, Bw Ramesh alisema taa ndani ya ndege "zilianza kuwaka" muda mfupi baada ya kupaa.
Ndani ya sekunde tano hadi 10, walihisi kama ndege "ilikuwa imekwama angani", alisema.
"Taa zilianza kubadilika rangi ya kijani na nyeupe ... ghafla ndege iligonga jengo na kulipuka."
Ndege hiyo aina ya Boeing 787-8 Dreamliner ilianguka kwenye jengo lililotumika kama malazi ya madaktari katika Chuo cha Matibabu cha Byramjee Jeejeebhoy na Hospitali ya Kiraia.
Lakini Bw Ramesh, ambaye anatoka Leicester nchini Uingereza anasema sehemu aliyokuwa amekaa ilitua karibu na ardhi na haikugonga jengo hilo.
"Mlango ulipovunjika na nikaona kuna nafasi, nilijaribu kutoka hapo na nikafanya hivyo.
"Hakuna mtu angeweza kutoka upande wa pili, ambao ulikuwa kwenye ukuta, kwasababu ilianguka hapo."
Video iliyoshirikishwa kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha Bw Ramesh akitembea kuelekea kweney gari la wagonjwa na moshi ukifuka nyuma.
Chanzo cha picha, Hindustan Times
Alimwambia mtangazaji wa India kwamba haamini alitoka vipi kwenye mabaki hayo ya ndege akiwa hai.
"Niliona watu wakifa mbele ya macho yangu - wahudumu wa ndege, na watu wawili waliokuwa karibu nami," alisema.
"Kwa muda, nilihisi kama nitakufa pia, lakini nilipofungua macho yangu na kutazama pande zote, niligundua kuwa nilikuwa hai.
"Bado siamini jinsi nilivyonusurika. Nilitoka kwenye kifusi."
Dk Dhaval Gameti, ambaye alimtibu Bw Ramesh, alisema alikuwa "amechanganyikiwa, na majeraha mengi mwili mzima", lakini hayuko "hatarini".
Siku ya Ijumaa asubuhi, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alitembelea eneo la ajali kabla ya kuelekea hospitalini kukutana na watu waliojeruhiwa akiwemo Bw Ramesh, na familia za waathiriwa.
Ndugu ya Bw Ramesh, Ajay, pia alikuwa ndani ya ndege hiyo.
Ndugu yao mwingine, Nayan Kumar Ramesh, aliiambia BBC News Alhamisi kutoka nje ya nyumba ya familia yao huko Leicester: "Alipotupigia simu [Vishwashkumar], alikuwa na wasiwasi zaidi juu ya [Ajay]... Hilo ndilo analojali kwa sasa."
Bwana Ramesh, ambaye ni mfanyabiashara ambaye alizaliwa India lakini ameishi Uingereza tangu 2003, ana mke na mtoto wa miaka minne.
Pia unaweza kusoma:Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi