Muktasari:
- Fountain Gate ambayo masikani yake ni Babati mkoani Manyara ilianza msimu huu ikiwa moto kabla ya pumzi kukata na kujikuta ikipambania kubaki kwenye ligi badala ya kumaliza nafasi za juu ambayo ndio yalikuwa malengo.
KOCHA Mkuu wa Fountain Gate, Mohamed Laizer amedai mechi mbili za Ligi Kuu Bara zilizosalia ni ngumu kutokana na mahitaji ya wapinzani wao, akizitaja dakika 180 kuwa ndizo zinazomnyima usingizi kwa sasa.
Fountain Gate ambayo masikani yake ni Babati mkoani Manyara ilianza msimu huu ikiwa moto kabla ya pumzi kukata na kujikuta ikipambania kubaki kwenye ligi badala ya kumaliza nafasi za juu ambayo ndio yalikuwa malengo.
Timu hiyo katika mechi 28 ilizocheza imekusanya alama 29 zilizoiweka kwenye msitari wa njano wa kucheza mtoano ili kubaki katika ligi ikiwa nafasi ya 14 ikiwa imeshinda mechi nane, sare tano na kupoteza 15, huku ikifunga mabao 30 na kufungwa 54, ambapo inahitaji kushinda mechi zilizosalia ugenini dhidi ya Coastal Union na Azam kujihakikishia kubaki.
Lakini, ili ikwepe kucheza mtoano inatakiwa Pamba Jiji, Namungo na Coastal zilizopo nafasi ya 12, 11 na 10 zifanye vibaya katika mechi zilizosalia na yenyewe ishinde.
Laizer ameliambia Mwanaspoti kuwa mechi hizo zinamuumiza kichwa ikizingatiwa watacheza na timu ambazo zinahitaji kuwa juu kwenye msimamo, Azam ikitaka kumaliza nafasi ya tatu huku Coastal ikitaka kusogea juu zaidi.
"Maandalizi ni mazuri. Kwa sasa ni kuwapiga tu msasa vijana kwa sababu wachezaji ni walewale ambao nilianza nao msimu na nimerudi nimewakuta, hivyo nitawandaa kisaikolojia," alisema Laizer aliyerejea akitokea TMA inayoshiriki Ligi ya Championship.
Aliongeza kuwa kikosi ni kizuri, lakini kuna sehemu ambazo ameziongezea nguvu ili kuziba upungufu ambao awali ulionekana. "Kukaa juu kwenye msimamo katika mpira kama ilivyokuwa mwanzo siyo kazi rahisi. Nadhani tuliteleza, lakini nitajitahidi kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa," alisisitiza.
Kocha huyo alisema kambi ya maandalizi ambayo wameweka jijini Arusha kwa wiki tatu imewasaidia kurudisha utimamu wa miili kwa wachezaji na kuwafanya kuwa imara zaidi ambapo itakuwa na faida kubwa kwenye mechi mbili zijazo.
Mmoja wa wachezaji wa timu hiyo, Abdallah Kulandana alisema maandalizi yanaendelea vyema na kwamba, "kikubwa tu mashabiki waendelee kutuunga mkono ili mechi zilizosalia tukawafurahishe na kumaliza katika nafasi nzuri kwenye msimamo."
Naye Amos Kadikilo alisema ujio wa kocha huyo na mkurugenzi wa benchi la ufundi, Melis Medo aliyewahi kufundisha Coastal Union, Dodoma Jiji, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar kutawasaidia kutokana na ubora walionao.
Kadikilo alisema ligi ni ngumu na kila timu imejipanga, lakini wameapa kushinda dhidi ya Coastal na Azam ili kukusanya alama sita ambazo zitawaweka pazuri zaidi kwenye msimamo wa ligi na kuepuka presha ya kucheza mtoano.