.

Chanzo cha picha, Reuters

Dakika 7 zilizopita

Kwa sasa mapigano kati ya Israel na Iran yanaonekana kuwa ya mataifa hayo mawili pekee. Katika Umoja wa Mataifa na kwingineko kumekuwa na wito mkubwa mataifa hayo kujizuia kuendeleza mashambulizi.

Lakini hali itakuwaje ikiwa watashindwa kujizuia? Na je, hali itakuwaje ikiwa mapigano yataongezeka na kutanuka?

Fahamu matukio machache mabaya zaidi yanayoweza kutokea.

Marekani kuingizwa katika vita hivi

Licha ya yote ambayo Marekani imekanusha, Iran inaamini kabisa kwamba majeshi ya Marekani yaliidhinisha na pia kuunga mkono mashambulizi ya Israel kimyakimya.

Iran inaweza kushambulia maeneo ya Marekani kote Mashariki ya Kati - kama vile kambi za vikosi maalum vya kijeshi nchini Iraq, kambi za kijeshi katika eneo la Ghuba, na misheni zake za kidiplomasia katika eneo hilo.

Vikosi vya washirika wa Iran - Hamas na Hezbollah - vinaweza kuwa vimepunguzwa makali yake sana lakini wanamgambo wake wanaounga mkono Iran nchini Iraq wamesalia na silaha na bado ni imara.

Marekani ilihofia mashambulizi kama hayo yangeweza kutokea na kuwaondoa baadhi ya wafanyakazi wake. Katika ujumbe iliyotoa hadharani, Marekani imeionya Iran kuhusu matokeo ya shambulio lolote dhidi ya maeneo yake muhimu.

Soma zaidi:

Nini kinaweza kutokea ikiwa raia wa Marekani atauawa, tuseme, huko Tel Aviv au mahali pengine?

Donald Trump anaweza kujikuta akilazimika kuchukua hatua. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekuwa akishutumiwa kwa muda mrefu kwa kutaka kuiburuza Marekani imsaidie ili kuishinda Iran.

Wachambuzi wa masuala ya kijeshi wanasema ni Marekani pekee iliyo na mabomu ya kufyatua mabomu ambayo yanaweza kupenya ndani kabisa ya vituo vya nyuklia vya Iran, hasa kile cha Fordow.

Trump aliahidi eneo bunge lake la MAGA hataanzisha vita vyovyote vinavyoitwa "vita vya milele" katika Mashariki ya Kati. Lakini vile vile Warepublican wengi wanaunga mkono serikali ya Israel na mtazamo wakee kwamba sasa ni wakati wa kutafuta mabadiliko ya utawala mjini Tehran.

Lakini Marekani ikiingizwa kwenye vita hivyo, vitakuwa vimetanuka vibaya mno huku vikiwa na uwezekano wa kuendelea kwa muda mrefu na kuwa na athari mbaya zaidi.

Mataifa ya Ghuba kuburuzwa katika mzozo huo

Iwapo Iran itashindwa kuharibu jeshi la Israel linalolindwa vizuri na shabaha nyinginezo, basi inaweza kuelekeza makombora yake kwenye maeneo muhimu ya Israel katika ukanda wa Ghuba, hasa nchi ambazo Iran inaamini zilisaidia maadui zake kwa miaka mingi.

Kuna maeneo lengwa mengi ya nishati na miundombinu katika kanda hiyo. Kumbuka Iran ilishutumiwa kwa kushambulia maeneo ya mafuta ya Saudi Arabia mnamo mwaka 2019 na washirika wake wa Houthi walifikia shabaha zake huko UAE mnamo 2022.

Tangu wakati huo kumekuwa na maridhiano ya aina fulani kati ya Iran na baadhi ya nchi za eneo hilo.

Lakini nchi hizi ni mwenyeji wa kambi za ndege za Marekani. Baadhi pia - kwa busara - walisaidia kuilinda Israel dhidi ya shambulio la kombora la Iran mwaka jana.

Iwapo eneo la Ghuba lingeshambuliwa, basi nayo inaweza kudai ndege za kivita za Marekani zije kuilinda pamoja na Israel.

.

Chanzo cha picha, Reuters

Israel inashindwa kuharibu uwezo wa nyuklia wa Iran

Je itakuwaje shambulio la Israel likishindwa? Vipi ikiwa maeneo ya nyuklia ya Iran yako kina cha chini sana na yanalindwa vizuri? Je, hali itakuwaje ikiwa kilo 400 za madini ya urani iliyorutubishwa kwa 60% - fueli ya nyuklia ambayo imesalia kidogo tu kuwa silaha kamili, inayotosha kwa mabomu kumi au zaidi - hayataharibiwa?

Inadhaniwa kuwa yanaweza kufichwa ndani ya migodi ya siri.

Israel inaweza kuwa imeua baadhi ya wanasayansi wa nyuklia lakini hakuna mabomu yanayoweza kuharibu ujuzi na utaalamu wa Iran.

Je, itakuwaje ikiwa shambulio la Israel litashawishi uongozi wa Iran kwamba njia pekee ya kuzuia mashambulizi zaidi ni kuhakikisha imekuwa na nyuklia haraka iwezekanavyo?

Je, itakuwaje ikiwa viongozi wapya wa kijeshi walio kwenye meza ya mazungumzo ni wakaidi na hawajali sana kama ilivyokuwa kwa watangulizi wao waliokufa?

Hii inaweza kulazimisha Israel kufanya mashambulizi zaidi na uwezekano wa kuliweka eneo hilo katika mfululizo wa matukio ya vita na kujilinda.

Msukosuko wa kiuchumi duniani

Bei ya mafuta tayari imepanda.

Je, hali itakuwaje iwapo Iran itajaribu kuufunga Mlango-Bahari wa Hormuz, ikizuia zaidi usafirishaji wa mafuta?

Hali itakuwaje katika upande mwingine wa Rasi ya Arabia – ikiwa Wahouthi huko Yemen wataongeza mashambulizi yao dhidi ya meli katika Bahari ya Shamu? Wao ndio washirika wa mwisho waliosalia wa Iran wanaojulikana kwa kutotabirika.

Nchi nyingi ulimwenguni tayari zinakabiliwa na tatizo la gharama ya juu ya maisha. Kupanda kwa bei ya mafuta kutaongeza mfumuko wa bei kwenye mfumo wa uchumi wa kimataifa ambao tayari umeshuka kutokana na vita vya ushuru mkubwa vilivyoanzishwa na Trump.

Na tusisahau, mtu mmoja anayefaidika na kupanda kwa bei ya mafuta ni Rais Putin wa Urusi ambaye ghafla atakuwa na mabilioni ya dola akifidia hasara inayotokana na vita vyake dhidi ya Ukraine.

Kuanguka kwa tawala wa Iran kutasababisha ombwe

Je, itakuwaje ikiwa Israel itafaulu katika lengo lake la muda mrefu la kuangusha utawala wa nchi ya Kiislamu ya Iran?

Netanyahu anadai lengo lake kuu ni kuharibu uwezo wa nyuklia wa Iran. Lakini aliweka wazi katika taarifa yake kwamba lengo lake kubwa ni kuchochea mabadiliko ya utawala.

Aliwaambia "watu wa Iran" kwamba mashambulizi yake yalikuwa "yanawasafishia njia ya kufikia uhuru wenu" kutokana na kile alichokiita "utawala mbovu na wenye udhalimu".

Kuiangusha serikali ya Iran kunaweza kuwavutia baadhi ya watu katika eneo hilo, hasa baadhi ya Waisrael. Lakini inaweza kuacha ombwe gani? Je, athari zake zitakuwa gani? Mzozo wa wenyewe kwa wenyewe nchini Iran utakuwa wa namna gani?

Wengi wanaweza kukumbuka kilichotokea kwa Iraq na Libya wakati serikali kuu ilipokuwa imeondolewa.

Hata hivyo, mengi yanategemea sana jinsi mzozo huu utakavyoendelea katika siku zijazo.

Iran italipizaje na kwa nguvu kiasi gani? Na kujizuia kwa kiasi gani - kama kutakuwepo - Marekani inaweza kushawishi Israel kuwa nayo?

Jibu la maswali hayo mawili litaamua mengi yanayoibuka.