Muktasari:
- Mechi hiyo iliyopigwa jioni ya leo Juni 17z, 2025 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ilikuwa ya pili kwa Twiga Stars kwenye mashindano hayo baada ya ya kwanza kuitandika Sudan Kusini mabao 4-0.
TWIGA Stars ambayo ni timu taifa ya Tanzania upande wa soka la wanawake, imeendelea kutoa vichapo kwenye michuano ya CECAFA Senior Women Championship baada ya kuitandika Burundi mabao 6-0.
Mechi hiyo iliyopigwa jioni ya leo Juni 17z, 2025 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ilikuwa ya pili kwa Twiga Stars kwenye mashindano hayo baada ya ya kwanza kuitandika Sudan Kusini mabao 4-0.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Twiga Stars ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 yalifungwa na nahodha wa timu hiyo, Opah Clement dakika ya tisa na 31 kabla ya Jamila Rajabu kuongeza la tatu dakika ya 65.
Dakika tano baadae, Clara Luvanga alifunga bao la nne kwa kifua, Diana Msewa akaongeza la tano dakika ya 73 na la sita likifungwa na mfungaji bora wa Ligi ya Wanawake msimu huu, Stumai Abdallah.
Dakika zote 90 mashabiki waliojaa kutazama mchezo huo walikuwa wanaliimba jina la Opah ambaye aliibuka nyota wa mchezo huo akikabidhiwa kiasi cha shilingi laki mbili na nusu (250,000).
Kwa kufunga mabao mawili leo, yanamfanya Opah kuwa kinara wa kufumania nyavu hadi sasa akiwa nayo manne akifuatiwa na Silvia Kabene wa Uganda mwenye matatu.
Kocha wa Burundi, Niyungeko Alain Olivier amesifu kiwango kilichooneshwa na Twiga Stars akiamini kama wataendeleza moto huo watafanya vizuri kwenye michuano ya WAFCON.
"Naipongeza Tanzania ni nzuri, tumezidiwa mechi yote sijui kama tumechoka kwa sababu hatukuweza kufanya mazoezi vizuri.
"Mechi ya mwisho nitakuwa na mapumziko kidogo kabla ya kucheza, angalau tunaenda kurekebisha, ukiangalia nchi zingine zina mazoezi ya kutosha.
"Nina siku kama tatu za mapumziko na nitatumia kuwapatia mazoezi ya kutosha wachezaji wangu ili niweze kuona angalau sasa nisifungwe na Sudan Kusini," alisema kocha huyo.
Kocha wa Tanzania, Bakari Shime, amesema ameridhishwa na kiwango cha wachezaji akiamini mchango wao kwenye mashindano hayo yanaweza kuwa na manufaa kuelekea WAFCON mwezi ujao.
"Sisi tuko kwenye maandalizi ya mashindano ya WAFCON, nimeridhika na kiwango cha wachezaji," amesema Shime na kuongeza.
"Leo tulijaribu kitu tofauti kuanza na viungo wawili, na washambuliaji watatu wenye asili ya kucheza kati, Clara anaisukuma timu na kuwapoteza wapinzani kiwanjani na anawanyima uhuru."