NI rasmi kwamba Tausi FC maarufu kama Ukerewe Queens imekuwa bingwa wa Ligi Daraja la kwanza (WFDL) kwa wanawake baada ya kuichapa Bilo Queens kwa mabao 3-0 kwenye fainali iliyopigwa katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.
Mashindano hayo yalianza kupigwa Juni 8 hadi June 16, mwaka huu ambapo katika Uwanja wa Nyamagana yalishirikisha timu 16 zilizochuana hadi kupata mshindi.
Tausi inakuwa mabingwa na kufanikiwa kupanda Ligi Kuu Bara ikiungana na Bilo, Ruangwa Queens na Geita Queens ikichukua nafasi ya timu mbili zilizoshuka ambazo ni Mlandizi Queens na Get Program.
Msimu huu katika Ligi Kuu ya Wanawake timu zimeongezeka na kufikia 12 badala ya 10.
Katika mashindano hayo, Tausi imeandika rekodi ya kuchukua ubingwa bila kupoteza mchezo kwenye mechi tano, ikianza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Maendeleo Queens, ikaichapa mabao 8-0 Tanzania Prisons, ikaichapa Bunda Girls 2-0 na nusu fainali ikaitoa Geita Queens kwa mabao 2-0 na kutinga fainali, huku mshambuliaji wake, Adama Congo akiibuka mfungaji bora baada ya kutupia kambani mabao 14 kwenye mechi tano ikiwa ni wastani wa kufunga mabao matatu kila mchezo.
Katika mechi nyingine iliyopigwa uwanjani hapo ya mshindi wa tatu, Geita Queens iliichapa Ruangwa Queens kwa mabao 2-1.
Timu hiyo kabla ya ratiba ya ligi ilianza maandalizi mapema miezi mitano kabla ikiingia kambini Februari, mwaka huu jambo ambalo limeilipa kwa kiasi kikubwa hadi kubeba ubingwa.