a

Chanzo cha picha, EPA

Dakika 3 zilizopita

Kufuatia mashambulizi ya Israel dhidi ya maeneo yake ya nyuklia na viongozi wa kijeshi, Iran imerusha mamia ya makombora ya balistiki kuelekea Israel, huku baadhi yakigonga maeneo lengwa ardhini. Ingawa Israel iliyatambua na kuyazuia mengi ya makombora hayo, kadhaa yalivuka mifumo yake ya ulinzi, na kusababisha uharibifu mkubwa na majeruhi, ikiwemo Tel Aviv ya kati na maeneo mengine.

Ukubwa halisi wa silaha za makombora haya ya balistiki za Iran haujulikani wazi, lakini kwa ujumla inachukuliwa kuwa moja ya silaha kubwa na za kisasa zaidi katika kanda.

Makombora haya yanatofautiana kwa masafa mafupi (SRBM), ya kati (MRBM/IRBM), na yale ya masafa marefu (LRBM), ambayo yanaweza kusafiri maelfu ya kilomita.

Katika mgogoro unaoendelea kati ya Israel na Iran, makombora haya, hasa yale ya masafa marefu, yamekuwa sehemu muhimu ya nguvu ya Iran.

Jinsi makombora ya Balistiki yanavyofanya kazi

a

Chanzo cha picha, European Photopress Agency

Iran imetengeneza aina mbalimbali za makombora ya balistiki katika miongo mitatu iliyopita, ikiwa na mojawapo ya silaha kubwa na za kisasa zaidi katika kanda.

Makombora ya balistiki hasa ya masafa marefu (LRBM), ni silaha za masafa marefu zilizobuniwa kutoa vichwa vya kawaida au vya nyuklia kwa kufuata mzingo wa balistiki. Kurushwa kwa makombora haya hufanywa kwa kutumia injini zenye nguvu za roketi, ambazo huyasukuma juu kuelekea juu angani, yakisafiri kwa kasi kubwa sana.

Mchakato huu wa kurusha hugawanywa katika hatua kadhaa: kwanza, injini huwaka na kutoa msukumo mkubwa wa kwanza; kisha, baadhi ya roketi huweza kujitenga (stage separation) ili kupunguza uzito na kuongeza kasi. Ni muhimu kutambua kwamba, tofauti na ndege, makombora ya balistiki hayategemei hewa kwa ajili ya msukumo wao. Yanabeba mafuta na vifaa wezeshi, vinavyoruhusu kusafiri hata nje ya angahewa.

Mara tu injini zao zinapozimwa na mafuta kwisha, kombora hufuata njia iliyopangwa kabla, likieleeka juu na baadaye kurudi chini kwa kasi kuelekea ilipoelekezwa kugonga shabaha yake. Fizikia inayoongoza mwendo wa makombora ya balistiki inafanana na ile inayoongoza utupaji wa mkuki, ambapo kombora hupata msukumo wake wa awali tu kutoka kwa nguvu za kurushwa, na kisha kuendelea kusafiri chini ya ushawishi wa mvutano (gravity), kasi yake (momentum), na msuguano wa hewa (air resistance).

Kasi, umbali, na muda wa kusafiri

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Kiwango na Umbali:

Makombora ya balistiki yanaweza kusafiri umbali mbalimbali, kuanzia mamia machache ya kilomita hadi zaidi ya kilomita 10,000 kuvuka mabara. Aina muhimu ni Makombora ya Balistiki ya Masafa Marefu (LRBM), ambayo yanaweza kusafiri kati ya kilomita 3,500 hadi 5,500 (maili 2,175-3,418), na hivyo kuwa tishio kubwa kwa maeneo lengwa yaliyoko mbali.

Kasi:

Makombora haya husafiri kwa kasi kubwa sana, hivyo kuyawezesha kusafiri maelfu ya kilomita ndani ya dakika chache tu. Kasi yao hupimwa kwa kipimo kinaxhoitwa (Mach) kinacholingana na kasi ya sauti (Mach 1 ni takriban kilomita 1,225/saa). Baadhi ya makombora ya masafa mafupi hufikia kasi ya juu ya sauti (zaidi ya Mach 1), huku yale ya masafa marefu, ikiwemo LRBM, yanaweza kusafiri kwa kasi ya hypersoniki, yaani zaidi ya Mach 5 (kilomita 6,125/saa).

Muda wa Kusafiri:

Umbali kati ya Iran na Israel ni takriban kilomita 1,300 hadi 1,500 (maili 800-930). Makombora ya balistiki kutoka Iran yanayosafiri kwa Mach 5 yanaweza kufika Israel kwa takriban dakika 12, ingawa muda kamili unategemea aina ya kombora na eneo la kurushia.

Kwa nini makombora ya Balistiki ni magumu Kuzuiwa?

s

Chanzo cha picha, Press Association

Maelezo ya picha, Kombora la cruise ambalo husafiri polepole kulinganisha na Balistiki

Kinachofanya makombora ya balistiki kuwa hatari sana ni mchanganyiko wa masafa yao marefu, kasi yao kubwa, na ugumu wa kuyazuia. Njia yao ya kuruka juu kwa kasi huipa mifumo ya ulinzi muda mfupi sana wa kuyakabili, na yanaporejea kutoka angani, yanashuka haraka hata zaidi, jambo linalofanya uzuiaji kuwa mgumu zaidi.

Kasi yao ya ajabu, hasa katika awamu ya mwisho inaporudi kutoka angani, inamaanisha kuna muda mfupi sana kwa mifumo ya rada kugundua, kufuatilia, na kurusha kombora la kuyazuia.

Zaidi ya hayo, baadhi ya makombora ya kisasa hutumia mbinu za kupunguza kuonekana na kugundulika (stealth technology), vifaa vya kudanganya (decoys) au hatua zingine za kukabiliana (countermeasures) ili kuficha ishara zao za rada na kudanganya mifumo ya ulinzi ya makombora, na hivyo kuyafanya kuwa magumu zaidi kuzuiwa kwa ufanisi.

Tofauti na makombora aina kama cruise ambayo huruka kwneye anga ya chini na polepole, na hivyo kuruhusu kuzuiwa, makombora ya balistiki husafiri kwa kasi kubwa sana na kwa mzingo unaotabirika, lakini kasi hiyo ndiyo inayoyafanya kuwa magumu kuyazuia. Ingawa makombora ya cruise yanaweza kuchukua takriban masaa mawili kufika Israel kutoka Iran, na droni hadi masaa tisa, makombora ya balistiki ni ya haraka zaidi na hatari zaidi kutokana na kasi na njia yao ya kuruka. Na ndiyo yamekuwa nguzo muhimu ya Iran katika vita yake ya sasa na Israel.