Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Amir Azimi
- Nafasi, Mhariri wa BBC Persian
Dakika 14 zilizopita
Israel inaamini kuwa kuna tishio kubwa kutoka kwa nguvu za nyuklia za Iran. Inasema lengo kuu la mashambulizi iliyofanya Ijumaa ilikuwa ni kuharibu tishio hilo.
Lakini Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ana lengo kubwa zaidi, kusababisha mabadiliko ya serikali nchini Iran.
Netanyahu anaweza kuamini kwamba kwa kufanya mashambulizi makubwa kuliko hapo awali, anaweza kusababisha mlolongo wa athari zitakazopelekea ghasia, ambazo hatimaye zitasababisha kuanguka kwa Jamhuri ya Kiislamu.
Ijumaa jioni, alisema: "Ni wakati wa Wairani kuungana chini ya bendera yenu na urithi wake wa kihistoria, kwa kusimama kwa ajili ya ukombozi kutoka kwa utawala mbaya na wa ukandamizaji."
Wairani wengi wamechukizwa na hali ya kiuchumi ya nchi hiyo, ukosefu wa uhuru wa kujieleza, na ukiukaji wa haki za wanawake na wachache. Mashambulizi ya Israel yanaonekana kuwa tishio kubwa kwa uongozi wa Iran.
Katika mashambulizi haya, kamanda wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC), mkuu wa majeshi, na viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa IRGC waliuawa. Na mashambulizi ya Israel bado hayajaisha.
Chanzo cha picha, EPA-EFE/Shutterstock
Ijumaa alasiri, Iran ilijibu kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi.
"Maeneo kadhaa, vituo vya kijeshi, na vituo vya anga vilishambuliwa," IRGC ilisema.
Hali ilizidi kuwa mbaya zaidi, na baada ya mashambulizi ya makombora ya kulipiza kisasi ya Iran, Netanyahu alisema, "mashambulizi zaidi yanakuja."
Viongozi wengine wengi wa Iran wanaweza kulengwa.
Israel inaweza kuhesabu kwamba mashambulizi haya na mauaji yatasababisha machafuko ndani ya serikali na kupelekea uasi wa wananchi.
Angalau, Netanyahu anatumaini hivyo.
Lakini huu ni mchezo mkubwa wa kubahatisha.
Kwanza, hakuna ushahidi wowote hadi sasa kwamba mlolongo wa athari kama wanavyotarajia utatokea. Hata kama utaanza, haijulikani wazi ni wapi mchakato huo utaishia.
Nguvu kubwa nchini Iran iko mikononi mwa wale wanaodhibiti jeshi na uchumi. Sehemu kubwa ya udhibiti huo iko mikononi mwa watu wenye misimamo mikali ndani ya Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) na baadhi ya taasisi zisizochaguliwa na wananchi.
Kwa kuwa tayari wako madarakani, hawana sababu ya kupindua serikali. Lakini kuna uwezekano mkubwa watapeleka Iran kwenye njia ya migogoro zaidi.
Kwa upande mwingine, kuna uwezekano kwamba serikali itaanguka na kisha Iran itatumbukia katika machafuko.
Matukio yanayotokea katika nchi hiyo yenye idadi ya watu takriban milioni 90 yataathiri sana Mashariki ya kati nzima.
Israel inaweza kutamani kuona uasi ukitokea Iran, na hatimaye, washirika wa Israel wakichukua madaraka nchini humo.
Lakini swali muhimu ni nani atakuwa mbadala.
Katika miaka ya hivi karibuni, vikosi vya upinzani vya Iran vimegawanyika. Kwa hiyo, kwa sasa hakuna mbadala wazi.
Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka 2022, baada ya harakati ya "Mwanamke Maisha Uhuru" ("Woman Life Freedom") iliyotingisha sehemu kubwa ya Iran, baadhi ya vyama vya upinzani vilijaribu kuunda muungano wa makundi na wanaharakati mbalimbali wanaopinga Jamhuri ya Kiislamu.
Muungano huo haukudumu kwa muda mrefu kutokana na kutofautiana kwa maoni juu ya nani anapaswa kuongoza baada ya kupinduliwa kwa serikali, na ni aina gani ya serikali mpya inapaswa kuwa.
Viongozi wa Israel wanaweza kuona baadhi ya makundi haya au watu binafsi kama chaguo mbadala wanazozipendelea.
Kwa mfano, Reza Pahlavi, mwana wa Shah wa zamani aliyepinduliwa mwaka 1979 na Mapinduzi ya Kiislamu, ambaye alikuwa mkuu wa zamani wa taji wa Iran.
Anaishi nje ya nchi na anafanya jitihada kubwa kutafuta uungwaji mkono wa kigeni kwa malengo yake.
Alisafiri kwenda Israel katika miaka ya hivi karibuni.
Ingawa ana umaarufu fulani miongoni mwa baadhi ya Wairani, haijulikani wazi kama hii itamfanya kuwa nguvu ya mabadiliko ya serikali haraka.
Kuna pia kundi la upinzani la Mujahedin-e Khalq (MEK), ambalo linafanya kazi nje ya nchi. Kundi hili linataka kuondoa Jamhuri ya Kiislamu lakini linapinga kurudi kwa utawala wa kifalme.
Kundi hilo, lililoanzishwa kama kundi la Kiislamu la mrengo wa kushoto, lilimpinga vikali Shah hapo awali.
Baada ya mapinduzi, Mujahedin-e Khalq (MEK) walikwenda Iraq. Katika miaka ya mapema ya 1980, walijiunga na Saddam Hussein katika vita vyake dhidi ya Iran. Hii ilipunguza ushawishi wao miongoni mwa Wairani wengi.
Mujahedin-e Khalq bado inafanya kazi kikamilifu. Wana marafiki nchini Marekani, na baadhi yao wako karibu na timu ya Donald Trump.
Hata hivyo, tofauti na ilivyokuwa wakati wa muhula wa kwanza wa Trump, inaonekana kwamba kundi hili la upinzani halina ushawishi mkubwa katika Ikulu ya White House.
Wakati huo, viongozi wakuu wa Marekani kama vile Mike Pompeo, John Bolton, na Rudy Giuliani walihudhuria mikutano ya Mujahedin-e Khalq (MEK) na kutoa hotuba za kuunga mkono.
Kuna nguvu zingine za kisiasa pia, kuanzia wale wanaotaka kuunda demokrasia ya kidunia hadi wale wanaotaka ufalme katika mfumo wa bunge.
Bado ni mapema sana kutabiri matokeo kamili ya mashambulizi ya Ijumaa. Lakini wakati wa mapigano kati ya Iran na Israel mwaka jana, hapakuwa na dalili zozote thabiti kwamba Wairani waliona hali hiyo kama fursa ya kuipindua serikali.
Hata hivyo, matukio ya wakati huo hayakufanana na uharibifu wa shambulio la Ijumaa.
Chanzo cha picha, Getty Images
Ni nini lengo la mwisho la Iran?
Sasa tunapaswa kujiuliza, ni nini lengo la mwisho la Iran? Licha ya kulenga malengo kadhaa nchini Israel, Iran haionekani kuwa na njia nyingi nzuri.
Baadhi wanaweza kuona kuendelea kujihusisha na mazungumzo na Marekani na kupunguza mvutano kama njia salama zaidi kwa Iran.
Lakini kurudi kwenye mazungumzo, kama ilivyodaiwa na Trump, itakuwa chaguo gumu kwa viongozi wa Iran. Kufanya hivyo kunaweza kumaanisha wamekubali kushindwa.
Njia nyingine ni kuendelea na mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel.
Hii inaonekana kuwa njia wanayoipendelea zaidi.
Hivi ndivyo viongozi wa Iran walivyowaahidi wafuasi wao. Lakini mashambulizi yakiendelea, yatapelekea mashambulizi zaidi kutoka Israel.
Katika siku za nyuma, Iran imetishia kulenga vituo vya Marekani, balozi, na maeneo katika kanda.
Lakini hii si rahisi kufanikiwa. Kushambulia Marekani kunaweza kusababisha Marekani kujiingiza moja kwa moja kwenye mzozo huu, jambo ambalo Iran halipendi sana.
Njia hizi si rahisi kwa pande zote mbili. Na matokeo yake ni magumu kutabiri.
Kwa sasa, hali bado haijabainika. Tunapaswa kusubiri na kuona athari halisi za matukio haya zitakapoanza kuonekana.
Imetafsiriwa na Yusuph Mazimu na kuhaririwa na Ambia Hirsi