Chanzo cha picha, Getty Images
Dakika 26 zilizopita
Ayatollah Ali Khamenei ndiye kiongozi wa dini mbali na kuwa kiongozi mkuu wa utawala wa Iran. Yeye ndiye anayefanya uamuzi wa mwisho kuhusu masawala ya kisiasa nchini Iran.
Ayatollah Khamenei mara ka mara amepinga mataifa ya magharibi hususan Marekani.
Licha ya kuunga mkono kundi la wapatanishi wa taifa lake , Ayatollah Khamenei amekuwa akipinga matokeo kuhusu mazungumzo na mataifa yenye uwezo mkubwa duniani kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Ayatollah Khemenei alimrithi mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ayatollah Khomeini 1989.
Kabla ya kuchukua wadhfa huo alikua rais wa taifa hilo kwa mihula miwili kuanzia 1981 hadi 1989.
Alizaliwa kaskazini-mashariki mwa Mashhad mwaka wa 1939, mtoto wa mwanazuoni wa kidini, Ali Khamenei alisoma katika seminari za mji alikozaliwa kabla ya kuhamia mji mtakatifu wa Washia wa Qom.
Mnamo 1962, alijiunga na vuguvugu la upinzani la kidini la Ayatollah Khomeini dhidi ya Shah Mohammad Reza Pahlavi.
Akiwa kijana Ali Khamenei akawa mfuasi makini wa Khomeini. Kwa mujibu wa maelezo yake mwenyewe, kila kitu alichofanya na anachoamini leo kimetokana na maono ya Khomeini kuhusu Uislamu.
Ali Khamenei alishiriki kikamilifu katika maandamano dhidi ya shah na alifungwa jela mara kadhaa.
Baada ya Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, Ali Khamenei alihudumu katika Baraza la Mapinduzi, ambalo liliongoza kwa ushirikiano na serikali ya mpito. Baadaye akawa naibu waziri wa ulinzi na kusaidia kuandaa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ambalo liliibuka kwa moja ya taasisi zenye nguvu zaidi za Iran.
Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo Juni 1981, alijeruhiwa vibaya katika shambulio la bomu dhidi ya msikiti mmoja mjini Tehran ambalo lilidaiwa kufanywa na kundi cha waasi wa mrengo wa kushoto. Tukio hilo lilisababisha mkono wake wa kulia kupooza .
Miezi miwili baadaye, kundi hilohilo la waasi lilimuua Rais wa Iran, Mohammad-Ali Rajai. Ali Khamenei alichaguliwa kurithi nafasi ya Rajai na alishikilia nafasi hiyo kwa miaka minane, mara nyingi akigombana na waziri mkuu wa wakati huo, Mir Hossein Mousavi, ambaye alihisi anashinikiza mageuzi mengi ya mfumo wa Iran.
Baada ya kifo cha Khomeini mnamo Juni 1989, Baraza la Wataalamu (baraza la maulama) lilimchagua Ali Khamenei kuwa Kiongozi Mkuu mpya, ingawa hakuwa amefikia daraja inayohitajika miongoni mwa maulama wa Kishia ambayo katiba ilitamka - marja-e taqlid (chanzo cha kuigwa) au ayatollah mkuu.
Ili kurekebisha hali hiyo, katiba ilirekebishwa na kusema Kiongozi Mkuu alipaswa kuwa "mwanazuoni wa Kiislamu", na kumwezesha Ali Khamenei kuchaguliwa. Pia alipandishwa hadhi kutoka cheo cha ushekhe cha Hojjat al-Islam hadi Ayatollah.
Katiba ya Iran pia ilibadilishwa ili kufuta wadhifa wa Waziri Mkuu na kuweka mamlaka makubwa katika mamlaka ya urais.
Uwezo wake ulihojiwa
Marais wanne waliohudumu chini ya Ayatollah Khamenei tangu wakati walihoji mamlaka yake bila ya kuidhoofisha Jamhuri ya Kiislamu.
Mohammad Khatami, mwanamageuzi, alishinikiza kutokuwa na uhusiano na nchi za Magharibi na uhuru zaidi wa kijamii na kisiasa nchini Iran alipokuwa madarakani kati ya 1997 na 2005. Lakini kiongozi mkuu na washirika wake walizuia utekelezaji wa sehemu kubwa ya mageuzi yake.
Mrithi wa kihafidhina wa Bw Khatami, Mahmoud Ahmadinejad, alionekana na baadhi ya watu kama mfuasi wa Ayatollah Khamenei. Lakini alikabiliwa na ukosoaji mkubwa juu ya usimamizi wa uchumi na maamuzi ya sera za kigeni serikali yake hadi akagombana na kiongozi mkuu baada ya kuripotiwa kujaribu kuongeza mamlaka yake.
Kuchaguliwa tena kwa Bw Ahmadinejad mwaka 2009 pia kulisababisha maandamano makubwa zaidi tangu mapinduzi hayo. Kiongozi huyo mkuu alisisitiza kuwa matokeo hayo yalikuwa halali na kuamuru msako mkali dhidi ya wapinzani ambao ulisababisha makumi ya wafuasi wa upinzani kuuawa na maelfu ya wengine kuzuiliwa.
Chanzo cha picha, Getty Images
Hassan Rouhani, mwenye msimamo wa wastani ambaye alichukua madaraka mwaka 2013, alisaidia kufikiwa kwa mkataba wa kihistoria wa nyuklia na mataifa yenye nguvu duniani kwa ridhaa ya Ayatollah Khamenei. Lakini kiongozi mkuu alipinga juhudi za rais za kupanua uhuru wa raia na kufanyi amarekebisho sera za kiuchumi.
Kushindwa kwa Bw Rouhani kukabiliana na changamoto za kiuchumi zilizowakabili raia wa Wairan, ambayo yalizidi kuwa mabaya zaidi baada ya Marekani kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia mwaka wa 2018 na kurejesha vikwazo dhidi ya Iran, yalizua maandamano makubwa mnamo Novemba 2019. Katika maandamano hayo, watu walisikika wakiimba "kifo kwa dikteta" - wakimuashiria kiongozi mkuu.
Machafuko hayo yalisababisha msako mkali wa umwagaji damu uliyofanywa na vikosi vya usalama. Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilisema zaidi ya watu 304 waliuawa, huku ripoti ya shirika la habari la Reuters ikikadiria idadi ya waliofariki kuwa 1,500. Mamlaka ya Iran ilipuuzilia mbali takwimu zote mbili.
Afisa mmoja pia alikanusha ripoti kwamba Ayatollah Khamenei aliamuru vikosi vya usalama na serikali "kufanya kila wawezalo kuwazuia wapinzani", kutoka nje ya nchi.
Chanzo cha picha, Getty Images
Ayatollah Khamenei amedaiwa kupoteza umaarufu mkubwa kama mtangulizi wake. Khomeini alikuwa kiongozi wa dini wa hadhi ya juu aliyefaa kuigwa.
Wakati Ayatollah Khamenei alipochukua uongozi , katiba ililazimika kufanyiwa ukarabati ili kuruhusu wadhfa huo kuchukuliwa na kiongozi yeyote wa dini bila kutilia shime wadhfa wake.
Aliimarisha uongozi wake kama kiongozi mkuu wa dini nchini humo kwa kujenga uhusiano wake na taasisi mbalimbali nchini humo pamoja na vikosi vya usalama, hususan jeshi lenye uwezo mkubwa la Islamic Revolution Guards Corps (IRGC).
Mwaka 1997 , alikosana na Ayatollah Hossein Montazeri , kiongozi wa dini aliyeheshimika na msomi.
Ayatollah Montazeri , mkosoaji wake mkubwa aliyefariki 2009, alihoji uwezo wa kiongozi huyo wa dini.
Hatua hiyo ilisababisha kufungwa kwa shule yake ya kidini , shambulio katika afisi yake ya Qom na kuhukumiwa kifungo cha nyumbani kwa muda.
Chanzo cha picha, OTHER
Uamuzi wa Ayatollah Khamenei pia ulikosolewa
Wakati alipomuunga mkono rais wa zamani wa Iran Mahmoud Ahmadinejad, kufuatia ushindi wake katika uchaguzi uliokumbwa na utata 2009 , raia wengi wa Iran walifanya maandamano wakipinga matokeo hayo.
Wagombea walioshindwa Mirhossein Mousavi na Mehdi Karroubi walipinga uchaguzi huo .
Wote waliwekwa katika kifungo cha nyumbani mnamo mwezi Februari 2011 , pamoja na mke wa bwana Mousavi Zahra Rahnavard, baada ya kuitisha maandamano wakiunga mkono mapinduzi ya raia yaliokuwa yakiendelea nchini Misri na Tunisia.
Udhibiti wa kihafidhina
Kama kiongozi wa kidini, Ayatollah Khamenei ana uwezo wa kuwachagua moja kwa moja wanachama wa baraza la walezi . Baraza hilo linasimamia uchaguzi mbali na ukaguzi wa wagombea.
Katika uchaguzi wa Mwaka 2004, baraza hilo liliwaondoa katika kinyang'anyiro maelfu ya wagombea wa ubunge ikiwemo wenye misimamo ya wastani, wanaopigania mageuzi na wanachama wa serikali iliopita.
Wahafidhina walishinda kwa asilimia 70 ya kura zilizopigwa.
Mwaka 2013, baraza hilo lilimzuia Akbar Hashemi -Rafsanjani , rais wa zamani na kiongozi wa baraza lenye ushawishi mkubwa nchini Iran kutowania urais kutokana na madai ya kuwa mzee.
Bwana Rafsanjani alikuwa ameunga mkono waandamanaji baada ya uchaguzi wa 2009.
Ayatollah Khamenei amekuwa akiunga mkono usimamizi wa baraza hilo la walezi , licha ya ukosoaji mkubwa kwamba kuwandoa wagombea katika kinyang'anyiro cha uchaguzi kunaharibu demokrasia.
Uhusiano wa kigeni
Katika hotuba yake kama rais 1981 , Ayatollah Khamanei aliahidi kukabiliana na upotofu, ukombozi na wasomi wanaounga mkono sera za Marekani.
Mwaka 2009 wakati rais Barrack Obama alipoipatia Iran 'mwanzo mpya wa mazungumzo ya kidiplomasia' jibu la Ayatollah Khamenei lilifutiliwa mbali.
Alisema kwamba hajawahi kuona mabadiliko katika sera ya Marekani akisisitiza kuhusu Marekani kuisaidia Israel na kuiwekea vikazo Iran.
Lakini alisema kua iwapo rais Obama angebadili sera hiyo ya Marekani basi alikua tayari kushirikiana nae.
Mwaka 2013, kabla ya kufanyika kwa mazungumzo ya kinyuklia ya Iran pamoja na mataifa yenye uwezo mkubwa duniani , Ayatollah alisema kuwa hapendi diplomasia.
Katika lugha ambayo ahusishwi nayo , Ayatollah Khamenei alizungumza kuhusu diplomasia kuwa chanzo cha kutabasamu katika mazungumzo.
Mnamo mwezi Novemba 2013, Iran na mataifa yenye uwezo mkubwa duniani waliafikia makubaliano ya kwanza ya kinyuklia na Iran, ambapo taifa hilo la Kiislamu lilikubali kusitisha mpango wake wa kinyuklia ili kuondolewa vikwazo.
Lakini tarehe 7 mwezi Julai 2014, ikiwa ni wiki mbili kabla ya makubaliano ya mpango huo kuafikiwa , Ayatollah Khamenei alitoa hotuba yenye maelezo mengi ya kiufundi , akisisitiza kuwa Iran inahitaji sana kuongeza uzalishaji wa madini ya Uranium.
Siku ya miwsho ya mwezi Julai ilipita na pande hizo mbili zikakubaliana na kuongeza muda wa mazungumzo hadi mwezi Novemba 2014.
Wakati na baada ya vita vya Marekani dhidi ya Iraq , Khamenei aliikosoa sera ya Marekani. ''Uvamizi wa Iraq sio kitu ambacho Marekani inaweza kumeza'', alisema.
Mnamo mwezi Juni 2014, baada ya wapiganaji wa Kijihadi wa Islamic State kuteka maeneo ya kaskazini mwa Iraq , Ayatollah kwa mara nyengine alipinga hatua ya Marekani kuingilia kati .
Lakini mnamo mwezi Agosti, aliunga mkono uteuzi wa Haydar al-Abadi kuwa waziri mkuu mpya akikata uhusiano na mwandani wake wa zamani Nouri Maliki.