ZRA yavunja rekodi makusanyo ya mapato Januari

Unguja.  Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imekusanya Sh81.512 bilioni kwa Januari sawa na ufanisi wa asilimia 100.65, huku sababu za kufanya vizuri ikitajwa ni kuongezeka kwa matumizi ya mafuta kwenye vyombo vya moto vya barabarani.

Baadhi ya sherehe zilizofanyika ni kuadhimishwa kwa miaka 61 ya Mapinduzi, viongozi wakuu wa Zanzibar na Tanzania bara kushiriki kufungua na kuweka mawe ya msingi ya miradi ya maendeleo zaidi ya 190 Unguja na Pemba kuanzia Desemba 20 hadi Januari 12.

Makadirio yalikuwa ni kukusanya Sh80.984 bilioni katika kipindi hicho.

Kaimu Kamishna wa ZRA, Said Ali Mohamed amesema hayo leo Jumatatu Februari 3, 2025 wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari ofisini kwake Mjini Unguja.

Amesema makusanyo hayo ni ya kihistoria kwa kuwa, mamlaka hiyo pamoja na kuvuka lengo la makusanyo, imebadili namba hiyo kutoka kwenye digiti ya saba sasa imekwenda digiti ya nane.

“Ukusanyaji huu wa Sh81. 512 bilioni ni wa kihistoria katika ukusanyaji wa mapato ambayo yamewahi kukusanywa na ZRA,  kwa sababu tangu kuanzishwa kwa mamlaka hii, makusanyo yalikuwa kati ya Sh50 bilioni na Sh70 bilioni lakini leo tumefika Sh81 bilioni,” amesema Said.

Amesema makusanyo ya Januari ya mwaka 2024 yalikuwa Sh70 .180 bilioni yakilinganishwa na makusanyo ya Januari 2025 yanaonesha ongezeko la makusanyo ya Sh11.332 bilioni sawa na ukuaji wa makusanyo wa asilimia 16.15.

Said amesema hali ya makusanyo kwa miezi saba ya kwanza ya mwaka 2024/25 kuanzia Julai hadi Januari mwaka huu, ZRA ilikadiriwa kukusanya Sh500.187 bilioni, lakini imefanikiwa kukusanya Sh510.545 bilioni ambazo ni ufanisi wa asilimia 102.07 wa makusanyo ya mapato yaliyokadiriwa kukusanywa katika kipindi hicho.

Amesema kwa kulinganisha makusanyo ya Julai hadi Januari ya 2023/24, yaliyokuwa Sh421.949 bilioni, yanaonesha ongezeko la makusanyo ya Sh88.598 bilioni sawa na ukuaji wa makusanyo ya asilimia 21.00.

Ametaja sababu nyingine za kufanya vizuri ni kuimarika kwa uzuiaji wa kodi kunakofanywa na mawakala wa uzuiaji, hali inayotokana na utekelezaji wa sera na miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Uwekezaji mkubwa katika miundombinu na huduma za kijamii pamoja na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi Zanzibar, unatokana na utekelezaji wa sera nzuri za kiuchumi za Serikali ya wamu ya nane,” amesema.

Pia, amesema kumeongezeka uwajibikaji wa walipakodi katika matumizi ya mifumo ya ukusanyi wa mapato pamoja na mfumo wa kutolea risiti.

Baadhi ya wananchi wamesema pamoja na ongezeko hilo, bado wapo wafanyabiashara wanakuwa wagumu kutoa risiti za kieleketroniki, hivyo wakizidi kuwabana huenda kiwango hicho kitaongezeka zaidi.

“Wengi wanakuwa wagumu kutoa risiti za kielektroniki,  wanakuwa wasumbufu, kwa hiyo ZRA inapaswa kuwabana zaidi wafanyabiashara,” amesema Nasra Khatib.

Mmoja wa wafanyabiashara Mtendeni, Khalid Masoud amekiri kuwapo kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaogoma kutoa risiti huku akisifu utaratibu wa mamlaka hiyo kuwatembelea na kusikiliza changamoto zao.