Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema ushirikiano na wawekezaji wa kimatataifa hautawanufaisha wawekezaji hao pekee, badala yake unalenga kuwawezesha wafanyabiashara wa ndani kupata vifaa vya uzalishaji.
Vifaa hivyo vitatumika kuwasaidia kukuza biashara na kujipanga katika soko la kimataifa.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema hayo leo Ijumaa Aprili 11, 2025 katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla wakati wa utiaji saini mkataba wa ushirikiano kati ya Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa) na Benki ya Uwekezaji ya Ufaransa (BPI), shughuli iliyofanyika mjini Unguja.
“Ushirikiano huu unaoingia Serikali hautawanufaisha wawekezaji wa kimataifa pekee bali utawawezesha wafanyabiashara wa ndani kupata vifaa muhimu vya uzalishaji, ambavyo vitasaidia biashara zao na kujipanga katika soko la kimataifa,” amesema.
Amesema ushirikiano huo unalenga uwekezaji wa kifedha na kufungua milango ya uwekezaji kutoka nchi mbalimbali, kupeana taaluma na kubadilishana uzoefu wa kufanya kazi ambao utawaogezea uwezo wataalamu wa ndani.

Amesema kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano kati ya Zipa na Benki ya BPI kunadhihirisha utayari wa kushirikiana katika kukuza na kuendeleza miradi ya maendeleo nchini.
Kiongozi huyo amesema makubaliano hayo ya kimkakati ni ishara ya kuweka mlango wazi kwa wawekezaji kutoka Ufaransa na kubadilishana mifumo ya uchumi na biashara katika kupeana fursa za uwekezaji.
Dk Mwinyi katika hotuba amesema Serikali imekuwa ikiweka mazingira rafiki ya biashara ikiamini uchumi unakua na kufanikiwa kwa ushirikiano na kufanya uvumbuzi wa kitaaluma.
Kupitia makubaliano hayo, amesema yanadhihirisha utayari wa kufanya kazi kwa pamoja na kuleta matokeo chanya katika uwekezaji na ukuaji wa uchumi.
Mkurugenzi Mkuu wa Zipa, Saleh Saad Mohamed amesema benki hiyo ipo tayari kuisaidia Zanzibar kwa kuwezesha kifedha wawekezaji wa ndani na nje katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Amesema benki hiyo ipo tayari kuisaidia Zipa kutekeleza miradi katika maeneo huru ya uwekezaji vikiwamo viwanda, miradi ya maji, umeme, kuwajengea uwezo na kuwapatia fursa wawekezaji.
“Mkataba huu baina ya Zipa na Benki ya BPI utatumika katika kipindi cha miaka mitano ila ikimalizika tuna uwezo wa kuongeza muda,” amesema.
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara Ufaransa aliye Tanzania, Christophe Darmois amesema anajivunia kufanya kazi na Serikali ya Zanzibar.
Amesema mkataba huo utafungua milango ya biashara baina yao na Zanzibar.
Darmois amesema ushirikiano huo utakuwa endelevu kuhakikisha wananchi wananufaika na uwekezaji kutoka Ufaransa.
Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne-Sophie Ave amesema makubaliano kati ya benki hiyo na Zipa yamejikita katika sekta za mafuta na gesi, viwanda, miundombinu na utalii.