Zingatia haya ili kukuza biashara yako

Biashara ndogo ndogo ni mhimili wa kiuchumi kwa nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania. Inakadiriwa kuwa karibu ya robo tatu duniani wanategemea ama kuajiriwa na biashara ndogondogo.

Kwa biashara ndogo kabisa zinazoajiri mtu mmoja ama wawili changamoto kubwa sana ipo kwenye usimamizi wa fedha. Sababu kubwa ni kutokuwa na mpangilio wa kifedha, na mfanyabiashara kutokutambua kuwa yeye binafsi na biashara yake ni vitu viwili tofauti.

Ili kuwa na ufanisi wa kifedha na ili kuzingatia misingi ya usimamizi wa kifedha. Kutozingatia misingi ya usimamizi wa kifedha kwa biashara kunaweza kumfanya mfanyabiashara kufikiri kuwa kila kipato kinachotokana na biashara ni cha matumizi binafsi. Fuata misingi hii kama unataka usimamizi bora wa kifedha kwenye biashara yako.

Moja. Wekeza mtaji wa kutosha na linda mtaji wako. Mtaji ni muhimu sana kwa biashara yoyote ile. Ni vizuri kupata mchanganuo wa mtaji unaotakiwa kuanzisha biashara yako hata kama iwe ndogo kiasi gani. Usipokuwa na mtaji wa kutosha utafanya biashara ambayo haiwezi hata kulipa na hivyo kuishia kufilisika.

Pili. Tenganisha fedha za biashara na za kibinafsi. Hii ni muhimu na inafanya biashara kujitegemea na kujitenga na matumizi binafsi. Kutenganisha fedha au mauzo ya biashara na matumizi binafsi kunafanya biashara kujiendesha na kujitegemea. Kutokutenganisha fedha za biashara na za kibinafsi kunaweza kusababisha biashara kushindwa kukua au hata kufilisika ndani ya muda mfupi.

Tatu. Weka mfumo wa usimamizi wa fedha na biashara. Kwa kawaida biashara inapaswa kujiendesha yenyewe, na mfanyabiashara anapaswa kuwa na mfumo wa usimamizi wa kifedha ikiwemo kuweka muhtasari wa mapato na matumizi ya kibiashara na kufanya ukaguzi na tathmini ya mara kwa mara. Hii inasaidia kuelewa kama biashara ina tija au ufanisi ambao unategemewa.

Nne. Hakikisha biashara inalipa gharama zake. Ni mara nyingi sana mfanya biashara kutojipangia mshahara au kuhusisha watu wa familia kufanya kazi kwenye biashara bila malipo. Mara nyingine biashara inaweza kukodi nyumba au chumba ama eneo la biashara bila kulipa. Biashara zingine zinaweza kutumia umeme wa majumbani kwa ajili ya biashara. Hii inatokana na kukiuka msingi wa kuendesha biashara, tofauti na mambo binafsi.

Tano. Panga bajeti ya biashara yako. Ni muhimu kwa biashara kuwa na bajeti yake. Kuwa na bajeti inayojumuisha mapato na matumizi ya biashara ni hatua muhimu katika kusimamia fedha kwa ufanisi. Hakikisha unaorodhesha gharama zote muhimu za biashara kama kodi ya pango, gharama za bidhaa, usafirishaji, kodi na leseni za serikali, na mishahara ya wafanyakazi hata kama ni wewe ambaye ni mmiliki wa biashara. Ni vizuri pia kujua mtiririko wa gharama mathalani kodi za serikali zinalipwa kipindi fulani au kodi ya pango inalipwa lini.

Sita: Epuka Mikopo Isiyo na Mpangilio. Wafanyabiashara wengi huchukua mikopo kwa ajili ya matumizi binafsi wakitumia biashara zao kama dhamana. Hili linaweza kuwa hatari ikiwa mkopo hautaweza kurudishwa kwa wakati. Ni vyema kuchukua mkopo kwa madhumuni ya kukuza biashara tu, na si kwa ajili ya matumizi binafsi. Pia epuka kutoa mkopo kwa wateja, kuna utaalamu unatakiwa ili kuweza kutoa mkopo unaoweza kulipika.

Misingi ya kifedha kwa uendeshaji wa biashara ndogondogo ni muhimu katika kuendeleza biashara na kuweka uhimilivu kwenye biashara ili ziweze kuleta tija kwa wajarisiamali. Tafuta maarifa ya namna ya kuweza kutengeneza mfumo wa kifedha unaoweza kusaidia kuendeleza na kukuza biashara yako.