Morogoro. Uchunguzi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro umebaini kwamba chanzo cha moto ulioteketeza vibanda vya wafanyabiashara kilikuwa ni kishungi cha sigara kilichotupwa na mtu asiyefahamika kwenye maranda kikiwa kinawaka.
Tukio la moto lilitokea Machi 21, 2025 ambapo vibanda vya wafanyabiashara wa samani za ndani viliteketea na kuwasababishia hasara kubwa huku wakiomba msaada ili waweze kurejesha biashara zao.
Akizungumza na Mwananchi leo Machi 30, 2025, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shabani Marugujo amesema wamefanya uchunguzi huo kwa kuwahoji wahusika waliokuwepo kwenye eneo hilo kabla ya tukio la moto.
Pia, amesema wamefanya uchunguzi wa kisayansi wa moto huo kwa kutumia nadharia ya sayansi ya moto katika kubaini chanzo cha moto huo kuwa ni kishungi cha sigara kilichotupwa kwenye Maranda y ambao.
“Kamati iliyofanya uchunguzi wa tukio hili la moto imebaini kuwa chanzo ni kishungi cha sigara kilichokuwa kinawaka kutupwa au kudondoshwa kwenye maranda ya mbao na kusababisha moto. Moto huo ulisambaa kwa kasi kutokana na mabanda hayo kuwa na vichocheo vya moto kwa wingi kama vile mbao na rangi,” amesema Kamanda Marugujo.

Muonekano wa sasa baada ya vibanda vya wafanyabiashara wa samani mtaa wa Ngoto Manispaa ya Morogoro kuteketea kwa moto Machi 21, mwaka huu. Picha Hamida Shariff
Kamanda huyo ameongeza kuwa: “Matokeo ya uchunguzi huu yamefikiwa baada ya kutumia njia mbalimbali za uchunguzi ikiwemo mahojiano na wamiliki, wafanyabiashara, mlinzi, mashuhuda na wazima moto.”
Leo, Machi 30, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala amekwenda kuwapa pole wafanyabiashara hao na kukabidhi bati 162 zilizotolewa na ofisi yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali mkoani humo kwa ajili ya kuezeka mabanda yao yanayojengwa upya.
Akizungumza na wafanyabiashara hao, Kilakala amesema Serikali imeguswa na tukio hilo ambalo limesababisha hasara kwa wafanyabiashara na hivyo amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuangalia uwezekano wa kuwapa mikopo wafanyabiashara hao ambao wengi wao ni vijana.
“Kwenye halmashauri zetu zote nchini, ipo asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani ambazo zinatokewa kama mikopo kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu, niwashauri mjiunge kwenye vikundi ili mpate mikopo hii na mimi nitafuatilia kwa karibu jambo hili,” amesema Kilakala.
Mkuu huyo wa wilaya ameahidi kufanya mazungumzo na taasisi za kifedha ambazo zimewakopesha baadhi ya wafanyabiashara hao ili waone namna wanavyoweza kuwavumilia katika urejeshwaji wa mikopo hiyo.
“Msaada huu siyo wa mwisho, bali sisi Serikali tutaendelea kutafuta wadau wengine waweze kuwashika mkono, yawezekana hizi bati zikapelea, basi tuwasiliane tuone namna ya kuongeza bati nyingine,” amesema Kilakala.
Hata hivyo, amewataka wafanyabiashara hao kuchukua tahadhari kuepuka majanga mengine yakiwemo ya moto huku akiwataka kutumia wataalamu wakati wa kujenga mabanda hayo ili yasikaribiane.
Mwenyekiti wa umoja wa wafanyabiashara hao, Shukuru Magari amesema bado wanaendelea na tathimini ya hasara waliyoipata lakini kwa makadirio si chini ya Sh40 milioni.
Magari amesema mabanda yaliyoteketea ni 16 pamoja na nyumba tatu ambazo zipo jirani na mabanda hayo ambazo ziliteketea kabisa kwa moto.
Mwenyekiti huyo ameishukuru Serikali kwa kulibeba janga hilo, pia, amelishukuru Jeshi la Zimamoto licha ya kuwepo kwa changamoto zilizojitokeza siku ya tukio.
Mmoja wa waathirika wa moto huo, Teddy Antony ambaye amepoteza nyumba yake, amesema baada ya kuunguliwa na nyumba hiyo, kwa sasa amefadhiriwa na rafiki yake.

“Sikuweza kuokoa kitu chochote, mimi na familia yangu tulitoka kama tulivyo, kikubwa tunashukuru tumetoka salama, tunaiomba Serikali ituangalie na sisi tuliounguliwa nyumba kwa kuwa hatuna mahala pa kuishi, tumefanya kusitiriwa tu na wasamalia wema,” amesema Antony.