
Unguja. Ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa, Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), Audrey Azoulay imetajwa kuleta neema Tanzania kwa shirika hilo kuongeza utaalamu na msaada wa kifedha kusaidia maeneo ya urithi wa dunia.
Tangu Machi mosi, Mkurugenzi huyo amefanya ziara Tanzania bara na Zanzibar kwa kukutana na viongozi wakuu wa nchi na kutembelea maeneo ya kihistoria.
Miongoni mwa maeneo aliyotembelea ni Mafia, Palese Musium, Beit Al Ajab, Majestic Sinema na Soko la Watumwa Kanisa la Mkunazini yenye historia muhimu.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa ziara hiyo kisiwani hapa leo Alhamisi, Machi 6, 2025 Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Unesco, Ali Jabir Mwadini, amesema mbali na ziara hiyo kuliweka Taifa katika ramani ya dunia, imeambatana na neema mbalimbali za kutoa msaada wa kiufundi na kifedha katika kuimarisha majengo kadhaa.
“Ziara kama hizi ni adimu kwani haendi tu kila mahali, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache Afrika ambazo zimesajili maeneo mengi katika urithi wa dunia ambayo yana hadhi na sifa ya kutambuliwa za kipekee duniani.”
“Inatuweka mahali fulani katika ramani ya dunia katika eneo la uhifadhi kwani nchi hii inajivunia katika vivutio vingi vinavyoambatana na uhifadhi,” amesema.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Unesco ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Professa Hamis Malebo, amesema ujio wa kiongozi huyo ni mwaliko aliopewa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Ameeleza ujio huo kuwa na faida mbalimbali kwa nchi ikiwemo kuendelea kuifungua Tanzania kimataifa, kupata fursa ya kinamama wanaozalisha mwani na kutengeneza bidhaa kushiriki kwenye maonesho ya siku ya Mwafrika yatakayofanyika Mei mwaka huu, Paris nchini Ufarasa.
Kwa Mji Mkongwe wa Zanzibar yapo majengo ya zamani yaliyo katika hali mbaya na mengine yana hitaji utaalamu wa hali ya juu ili yaweze kuboreshwa na kuimarishwa yasianguke.
“Unesco inaendelea kutoa utaalamu kwa kuleta wataalamu wa kuangalia majengo na kutoa ushauri wa kimawazo na wa kifedha,” amesema.
Amesema wanashirikiana kwa pamoja kutafuta fedha kwa ajili ya uhifadhi wa majengo ya kale yaliyopo Mji Mkongwe na kuwashika mkono kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe, Ali Said Bakar amesema ziara ya kiongozi huyo kuja Zanzibar imeonesha uhusiano mzuri baina ya nchi na Unesco.
“Unesco inaweza kusaidia kuleta wadau mbalimbali kufanya matengenezo makubwa baadhi ya majengo ndani ya Mji Mkongwe pamoja na miundombinu yake,” amesema.
Tayari Serikali imetenga Dola za Marekani milioni 5.5 kwa ajili ya kukarabati Mji Mkongwe.
Awali, Azoulay alipokutana na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, alishauri shirika hilo kuendelea kuisaidia Zanzibar hususani katika uchumi wa buluu kwani ni muhimu kwa ustawi wa wananchi.
Azoulay amesema shirika hilo litaendelea kuisaidia Zanzibar katika sekta tofauti akisema wapo tayari kutoa misaada ya kitaalamu, teknolojia na uzoefu kuimarisha sekta hiyo.