
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), kupitia Kamati yake ya Mashindano, limetangaza kufuatilia kwa kina tukio linalodaiwa Kikosi maalum cha Ulinzi cha Valantia Zanzibar kuvamia uwanja pamoja na kusababisha vurugu katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA CUP), kati ya Uhamiaji FC dhidi ya KVZ FC, huku ikilaani vikali tukio hilo na vitendo vilivyofanywa.
Inaelezwa kwamba, tukio hilo lilitokea katika mchezo huo uliochezwa Juni 11, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja, ukichezeshwa na mwamuzi Constable wa Polisi, Tobias Wariko, huku Uhamiaji FC ikipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya KVZ.
“Kitendo hicho cha kuingia uwanjani, ni kosa na hairuhusiwi kwa mujibu wa kanuni ya kuendesha mashindano 2024-25, sura ya ishirini (20), ambayo imezungumzia kuhusu kufanya fujo kiwanjani kabla, wakati na baada ya mchezo.
“Hivyo ZFF, kupitia kamati husika, inafuatilia kwa karibu tukio hilo na itatoa adhabu kulingana na ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya Mashindano 2024-25,” imeeleza taarifa iliyotolewa leo Juni 12, 2025 na Ofisa Habari wa ZFF, Mohamed Kabwanga.
Naye, Ofisa Ulinzi wa ZFF, Ramadhan Abdalla Bakari, amesema kitendo hicho kimevunja Sheria 38 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Amesema, hakuna klabu ambayo imetoa taarifa ya kuhusika na ulinzi na usalama katika mchezo hivyo kitendo kilichofanywa kimevunja Sheria na kanuni za mashindano.
Amesema utaratibu wa ulinzi unapaswa kufanya vikao kabla ya mchezo ambavyo vitatoa mipango ya ulinzi hivyo mtu yeyote anayefika uwanjani na sare za kikosi chochote huko ni kuvunja sheria na amani kwa mashabiki.
“Ili uje na sare uwanjani lazima nikupe mualiko maalumu, hivyo wao walikuja pale kama nani? Kwa sababu hatukuwa na taarifa nao hivyo kwa askari yeyote anayetaka kuingia kwa kuvaa sare lazima nimpe kibali maalumu,” amesema Ramadhan.
Kabla ya matamko hayo ya ZFF, mapema leo Juni 12, 2025, Uhamiaji FC ilitoa taarifa ya kulaani tukio hilo huku ikidai limesababisha majeraha ya wachezaji wao saba na viongozi kadhaa wa benchi la ufundi.
Taarifa ya Uhamiaji FC imeeleza kwamba: “Baada ya dakika 90 kumalizika wachezaji wa Uhamiaji FC walimfuata muamuzi kwa nia ya kuonesha hisia za kutokuridhishwa na maamuzi yake jambo ambalo ni kawaida michezoni kutokea.
“Baada ya wachezaji hao kufika kwa mwamuzi ndipo kikosi cha KVZ wakiwa na sare za kazi (Uniform) silaha za moto, Mabomu ya machozi na silaha za chuma ikiwemo Fyuru na minyororo wakiwa wameziba nyuso zao walivamia uwanja na kuanza kuwapiga wachezaji waliokuwa karibu na muamuzi huyo ambae alikuwa chanzo cha kutokea malalamiko hayo.
“Wachezaji 7 wa Uhamiaji FC na baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi waliumizwa vibaya na wameripoti kituo cha Polisi Madema na kupewa PF3 kwa hatua za matibabu,” imefafanua taarifa ya Uhamiaji FC iliyotolewa leo Juni 12, 2025 na Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo, huku KVZ wakiwa hawajatoa tamko lolote.