
Kyiv. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy amesema yuko tayari kuingia mkataba wa madini kati ya Taifa lake na Marekani licha ya kuingia katika mzozo na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano na viongozi wa Ulaya mjini London nchini Uingereza, usiku wa jana Jumapili, Machi 2, 2025, Zelenskyy amesema Ukraine iko tayari kuendelea na makubaliano hayo ili iweze kunufaika na msaada wa kijeshi kutoka nchini humo.
“Ni sera yetu kuendelea licha ya kile kilichotokea zamani. Sisi ni watu wa kujenga. Ikiwa tulikubaliana kuyasaini, tulikuwa tayari kuyasaini. Na kwa uaminifu naamini kwamba Marekani pia iko tayari,” amesema Zelenskyy alipokuwa katika Uwanja wa Ndege wa London Stansted tayari kuondoka nchini humo.
“Labda kuna haja ya kutoa muda wa kuchambua mambo fulani, lakini nataka tu msimamo wa Ukraine usikike. Lilikuwa jambo muhimu sana kwangu kwamba msimamo wa Ukraine usikike.”
Zelenskyy amesema ana imani uhusiano wake na Trump utarejea huku akidai anaamini Serikali ya Trump haitasitisha msaada kwa Ukraine.
“Nadhani uhusiano wetu utaendelea. Kwa sababu huu ni zaidi ya uhusiano wa wakati fulani. Tunapaswa kuwa wazi. Ukraine si nchi kubwa zaidi duniani lakini kila mtu anaona jinsi inavyopigania uhuru wake.
“Tunategemea msaada kutoka Marekani bila shaka,” amesema Zelensky.
“Nadhani kusitisha msaada kama huo kutamnufaisha tu Putin. Na kwa sababu hiyo, nadhani Marekani na wawakilishi wa dunia iliyostaarabika, viongozi wa dunia hii, hakika hawatamsaidia Putin,” amesema.
Matamshi ya Zelenskyy yalikuja mwishoni mwa ziara yake ya siku mbili nchini Uingereza, ambako viongozi wa Ulaya walionyesha mshikamano wao katika kuunga mkono Ukraine na kuunga mkono juhudi za kumaliza vita ya Ukraine dhidi Russia.
Katika mkutano muhimu Mjini London, Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer amesema nchi yake na Ufaransa zitasimamia na kuandaa mpango wa amani utakaowasilishwa kwa Rais Trump.
“Tuko katika njia panda ya kihistoria leo,” Starmer amesema huku akiwataka viongozi wenzake wa Ulaya kuchukua hatua wakati huu wa kipekee kwa usalama wa Bara la Ulaya.
“Huu si wakati wa maneno zaidi. Ni wakati wa kuchukua hatua. Wakati wa kusimama na kuongoza na kuungana kuzungumzia mpango mpya wa amani ya haki na ya kudumu,” amesema Starmer.
Trump alitarajia kuingia katika makubaliano na Zelensky siku ya Ijumaa. Mkataba huo ungeipatia Marekani fursa ya kunufaika na madini adimu ya Ukraine kwa lengo la kurejesha amani nchini humo na kuiwezesha kukabiliana na tishio la kuvamiwa na vikosi vya Russia ya Vladimir Putin.
Baada ya Zelenskyy kumkosoa Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance kuhusu madai yake kwamba diplomasia ilikuwa muhimu baada ya mbinu ya Rais wa zamani Joe Biden kufeli, Trump na Vance walimkemea kiongozi huyo wa Ukraine kwa kutokuwa na shukrani ya kutosha kwa msaada wa Marekani kwa namna ambavyo imefadhili vita hiyo.
Baada ya mvutano huo, Trump alifuta ratiba yote iliyosalia ya ziara ya Zelenskyy, ikiwa ni pamoja na hafla ya kutia saini makubaliano ya madini na kusema kiongozi huyo wa Ukraine anaweza kurudi atakapokuwa tayari kwa amani.
Baadhi ya wabunge wa Republican, akiwemo Seneta Lindsey Graham wa Jimbo la South Carolina, walipendekeza kwamba Zelenskyy anapaswa kujiuzulu ikiwa hawezi kujadiliana na Trump.
Jumapili, Zelenskyy alikataa wito wa Republican wa kumtaka ajiuzulu akisema ni kinyume cha demokrasia. Hata hivyo, aliwahi kunukuliwa akisema ataachia madaraka ikiwa Ukraine itapewa uanachama wa Jumuiya ya Kujilinda ya Nato.
“Hapo itamaanisha nimekamilisha misheni yangu,” amesema Zelensky.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.