Zelensky kumuona Trump mjini Washington na kumuuliza ikiwa misaada ya Marekani ‘itasitishwa’

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema siku ya Jumatano Februari 26, 2025 analenga kukutana na mwenzake wa Marekani Donald Trump mjini Washington siku ya Ijumaa ili kukamilisha makubaliano ya mfumo wa uchimbaji wa madini ya Ukraine na kumuuliza kama anakusudia “kusitisha” msaada kwa Ukraine.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Ukraine anataka kukamilisha makubaliano ya mfumo wa uchimbaji wa madini ya Ukraine na kumuuliza mwenzake wa Marekani kama ana nia ya “kusitisha” msaada kwa Ukraine.

“Kuna tarehe ya kufanya kazi (…) Ijumaa,” Bw. Zelensky ameeleza wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko Kyiv. “Swali langu (kwa Bw Trump) litakuwa la moja kwa moja: je, Marekani itasitisha msaada huo au la? Je, tunaweza kununua silaha, ikiwa hakutakuwa tena na msaada?”

Kwa upande wake Rais wa Marekani Donald Trump amesema anaridhia ziara inayoweza kufanywa na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy nchini humo. Wanatarajiwa kusaini makubaliano yatakayoiruhusu Marekani kuchimba madini ya Ukraine.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi yake ya Oval, Trump amesema yuko tayari kukutana na Zelensky ambaye kulingana naye amesikia anakwenda Washington siku ya Ijumaa. “Ndiyo, nasikia anakuja Ijumaa, sina tatizo. Na atapenda kusaini na mimi. Na ninajua kwamba ni makubaliano makubwa. Na nadhani Wamarekani wanafurahia kwa sababu, Biden alikuwa anatapanya tu pesa kama pipi. Haya ni makubaliano makubwa. Yanaweza kufikia dola trilioni 1 na ni madini adimu sana duniani.” Amesema Trump.

Kulingana na Marekani na ripoti za vyombo vya habari, Ukraine tayari imekubaliana na toleo la mwisho la rasimu ya makubaliano hayo yaliyopendekezwa na Marekani siku ya Jumanne.