
Washington. Rais wa Marekani, Donald Trump amefichua kuwa ofisi yake imepokea barua kutoka kwa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ikisema yuko tayari kwa mazungumzo na Russia na kusaini makubaliano ya madini adimu.
“Ukraine iko tayari kukaa kwenye meza ya mazungumzo haraka iwezekanavyo ili kuleta amani ya kudumu. Hakuna anayetaka amani zaidi ya Waukraine,” Trump amesema katika hotuba yake bungeni usiku wa kuamkia leo huku akinukuu barua hiyo.
“Mimi na timu yangu tuko tayari kufanya kazi chini ya uongozi thabiti wa Rais Trump ili kupata amani ya kudumu’,” Trump alinukuu maneno ya Zelenskyy.
“Si hilo lingekuwa jambo zuri?” aliuliza. “Ni wakati wa kukomesha huu upuuzi. Ni wakati wa kusitisha mauaji. Ni wakati wa kumaliza vita hivi visivyo na maana. Ukitaka kumaliza vita, lazima uzungumze na pande zote mbili,” amesema Trump.
Kauli hiyo ya Trump imekuja siku chache baada ya mvutano mkali kati yake na Zelenskyy katika Ofisi ya Oval iliyoko Ikulu ya White House, hali iliyosababisha Marekani kusitisha msaada muhimu wa kijeshi kwa Ukraine.
Kusitishwa kwa msaada huo kunaipatia nafasi kubwa Russia kuishambulia Ukraine kwani asilimia zaidi ya 60 ya silaha zinazotumiwa na vikosi vya Zelensky zimetolewa nchini Marekani.
Tangu wakati huo, Zelensky amekuwa akijaribu kumrudisha Trump upande wake, akichapisha kwenye mitandao ya kijamii kwamba mvutano wao ulikuwa wa kusikitisha na anataka kurekebisha mambo.
Akihutubia Trump pia alisema kuwa Ukraine iko tayari kusaini makubaliano ya madini adimu wakati wowote utakaofaa kwake (Trump) bila kutoa maelezo zaidi.
Ukraine inaaminika kuwa na akiba ya madini adimu ya kimkakati kama vile Titanium, Lithium na Manganese ambayo yanaweza kuwa na manufaa kwa sekta ya anga ya Marekani, magari ya umeme na utengenezaji wa vifaa vya matibabu.
Utawala wa Trump umekuwa ukisisitiza kuwa kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na Ukraine kupitia makubaliano yatakayoruhusu Marekani kupata madini hayo yenye thamani, kunaweza kuzuia Russia kuchukua hatua dhidi ya Ukraine katika siku zijazo.
“Kisha tunataka kusonga mbele haraka kupitia hatua zote zinazofuata na kufanya kazi na Marekani kukubaliana juu ya makubaliano thabiti ya mwisho,” alisema Zelensky.
Awali katika chapisho lake, Zelensky alisema mkutano wa Ijumaa haukwenda jinsi ulivyopaswa kuwa huku akiongeza: “Inasikitisha kwamba ilitokea hivyo,” aliandika.
“Ni wakati wa kurekebisha mambo. Tunataka ushirikiano wa siku zijazo na mawasiliano ya kujenga.”
Ukraine iliamka na habari ya kushtua Jumanne iliyopita kwamba Marekani imesitisha na inakagua msaada wake wa kijeshi kwa nchi hiyo, baada ya kuvunjika kwa diplomasia wiki iliyopita.
Katika chapisho lake, Zelensky alitoa tamko la wazi la shukurani kwa msaada ambao Marekani imetoa hadi sasa kwa nchi yake.
“Tunathamini sana kile ambacho Marekani imefanya kusaidia Ukraine kudumisha uhuru na mamlaka yake,” aliandika.
Ripoti ya Alan Fisher wa Al Jazeera kutoka Washington DC, ilisema tamko la Zelensky kwamba anataka kuka kwenye meza ya mazungumzo “linapendekeza kuwa kile kilichotokea Ijumaa hakikwenda kama alivyotaka.”
“Kulikuwa na shinikizo kwake (Zelensky) kufanya makubaliano. Na yuko tayari kukubali kile ambacho Donald Trump yuko tayari kutoa kwa sasa, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa madini adimu nchini mwake, badala ya kiwango fulani cha msaada wa Marekani,” aliongeza.
Wakati huohuo, Russia ilisema kusitisha msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine ni hatua bora zaidi kuelekea amani, ingawa ilikuwa ikisubiri kuthibitisha hatua ya Trump.
Kutokana na uamuzi wa Trump kusitisha misaada ya kijeshi kwa Ukraine, wabunge wa chama cha Democrats nchini humo, walionyesha ghadhabu kuhusu mwelekeo mpya wa Trump dhidi ya Russia, ambapo serikali za vyama vyote tangu miaka ya 1940 zimekuwa zikisimamia kuhakikisha ulinzi wa Ulaya dhidi ya Russia. Mataifa hayo yamekuwa katika uhasama wa muda mrefu.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.