Zeco yadai taasisi za Serikali, wateja wakubwa Sh64 bilioni

Unguja. Wakati miundombinu ya Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) ikitajwa kuchakaa na kuzidiwa, hivyo kusababisha upatikanaji hafifu wa umeme, shirika hilo linadai wateja wake wa ndani zaidi ya Sh64 bilioni.

Zeco inapokea umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupitia kebo tatu; mbili za Unguja na moja ya Pemba, inayopokea umeme kutoka mkoani Tanga.

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake Machi 30, 2025, Meneja Mkuu wa Zeco, Haji Haji, amesema licha ya changamoto hizo, Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha upatikanaji wa umeme unaendana na kasi ya uwekezaji unaofanyika Zanzibar.

“Tuna madeni ambayo yapo katika makundi mawili: tuna madeni ya taasisi za Serikali na madeni ya wateja binafsi. Kwa pamoja, madeni ya ndani yanafikia Sh64 bilioni,” amesema.

Amesema zipo taasisi za Serikali ambazo hazilipi madeni kwa wakati, akieleza kuwa huenda hilo linatokana na fedha kutokukidhi mahitaji, hivyo malipo ya umeme kuwekwa mwisho, kana kwamba si lazima kulipwa kwa wakati huo.

“Ingawa huduma hiyo ikiondoka, basi na shughuli zao zote zinasimama, bahati mbaya sana wakati wa kufanya malipo haipewi kipaumbele kinachostahili. Katika hali hiyo, lazima kuwe na utaratibu wa kukusanya madeni hayo,” amesema.

Bila kutaja deni hilo ni la tangu lini, amesema wamejaribu kwa njia za kawaida kukusanya madeni, lakini imeshindikana. Hivyo, shirika limeamua kupitia waraka wa Serikali wa Baraza la Mapinduzi kwamba, ifikapo Juni mwaka huu, mita zote za umeme ziwe katika mfumo wa kulipia kabla ya matumizi.

“Tumeshaagiza mita mpya na za wateja wakubwa, tunaendelea kuzifunga,” amesema.

Kwa wenye madeni, amesema watakatwa kidogo kwa muda utakaowekwa ili wakamilishe malipo.

“Tumeanza kufanya hivyo kwenye mita za taasisi za Serikali. Anapokwenda kununua umeme, tunakata kidogo mpaka deni linamalizika,” amesema.

Kwa madeni ya wateja binafsi, amesema kwa kutumia utaratibu huohuo wameanza kuwafungia mita za kulipa kabla ya kutumia, ingawa kulikuwa na changamoto ya baadhi ya wateja kuhofia kuwa iwapo umeme ukiisha, watapata wakati mgumu kupata huduma.

“Tumewahakikishia kwamba wakati wowote watakapohitaji huduma ya umeme, saa 24 watapata. Tumepanua wigo wetu wa uuzaji wa umeme kwa kutumia taasisi zingine za kibenki na mitandao ya simu ili kuhakikisha umeme unapatikana kwa wakati,” amesema.

Amesema kwa sasa mtu anaweza kutumia simu janja kununua umeme, au kama hana, anaweza kwenda kwa wakala. Zamani, ilikuwa lazima aende Zeco kulipia kwa fedha taslimu.

Amesema baada ya muda mfupi, watakusanya madeni ambayo kipindi cha nyuma yalikuwa hayalipiki kulingana na namna mfumo ulivyokuwa.

Changamoto ya Miundombinu

Akizuzungumzia kuhusu kukatika-katika kwa umeme, amesema sababu ni miundombinu duni ikilinganishwa na mahitaji.

Hata hivyo, amesema jitihada zinaendelea kufanyika, ikiwa ni pamoja na kuanzisha miradi mikubwa ya umeme.

Tangu Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, aingie madarakani, sera zake zimevutia uwekezaji mkubwa, hivyo kuongeza matumizi ya umeme.

Meneja wa Zeco, Haji, ametolea mfano wa hoteli inayojengwa, ambayo ikikamilika mahitaji yake ya umeme yatakuwa megavoti nne. Amefafanua kuwa transfoma yake ni kubwa zaidi ya zile za kawaida, ambazo hutumia kilovoti 1,000 au 2,000.

Unguja inatumia kebo mbili za baharini, na Pemba inatumia kebo moja kutoka Tanga, ambako wanapata megawati 20, huku matumizi yake ya juu yakiwa megawati 15.3.

Kwa Unguja, kebo moja iliwekwa mwaka 1980, na ni ya kizamani. Ili kuipoza, inatumia mafuta. Awali ilikuwa na uwezo wa megawati 45, lakini kutokana na uchakavu na kufanyiwa marekebisho, kwa sasa ina uwezo wa kubeba megawati 30 pekee.

Kebo nyingine ya mwaka 2013 ina uwezo wa megawati 100, ambayo kitaalamu inapaswa kuachwa nafasi ya asilimia 20. Hata hivyo, kebo hiyo imetumika hadi asilimia 93.7, hivyo nafasi iliyobaki (gap) ni ndogo.

Kwa sasa, Zeco inapata megawati 122 kutoka Tanesco, lakini mahitaji ya ndani ni megawati 135.

“Ni dhahiri umeme tunaoupata ni mdogo ikilinganishwa na mahitaji tuliyonayo, kwa hiyo lazima jitihada zifanyike. Kebo zetu zimeshafikia ukomo, hatuwezi kuongeza kiwango kingine cha umeme katika tulizonazo,” amesema.

Ni mtazamo wa wateja kuwa kama deni hilo lingelipwa, hata matatizo ya umeme yasingekuwepo.

Masoud Makame Said, mkazi wa Amani, Unguja, amesema uwepo wa deni hilo kubwa unaweza kuwa sababu ya kukosekana kwa fedha za kurekebisha miundombinu ili iwe imara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *